Azam yaifuata Yanga

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:22 AM May 05 2024
Wachezaji wa Azam FC.
PICHA: MAKTABA
Wachezaji wa Azam FC.

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la FA, Yanga kutoka Dar es Salaam inatarajia kucheza mechi yao ya hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya Ihefu Mei 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha, imefahamika.

Nusu fainali nyingine ya mashindano hayo itachezwa Mei 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza kwa kuwakutanisha Azam FC dhidi ya Coastal Union.

Ratiba ya mechi hiyo ilitolewa rasmi jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kukamilika kwa mechi za hatua ya robo fainali ambapo Azam FC ilipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Namungo kutoka mkoani Lindi, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam juzi usiku.

Bao la kwanza la Azam katika mchezo huo lilifungwa na Kipre Junior dakika ya 10 huku Idd Selemani 'Nado' akiandika la pili dakika tano baadaye wakati Feisal Salum 'Fei Toto' yeye alifunga goli dakika ya 19 huku Ayoub Semtawa akipachika bao kwa upande wa wageni dakika chache kabla ya kwenda mapumziko.

Dakika ya 52, Gibril Sillah alifunga bao la nne kwa Azam FC, ikiwa ni siku chache imetoka kuwafunga wenyeji hao wa Ruangwa mabao 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Licha ya kupata ushindi huo, Kocha Mkuu wa Azam, Yousuopha Dabo, alisema mechi hiyo haikuwa rahisi kutokana na aina ya wapinzani waliokutana nao.

"Baada ya kupata mabao ya kuongoza, tulionekana kupunguza kasi na kuwapa nafasi wapinzani wetu kupata bao moja. Alisema wachezaji wake walionyesha kiwango bora dakika 25 za mwanzo, hata hivyo kipindi cha pili wachezaji wake waliamka na hasa walipofunga goli la nne," alisema Dabo.

Ofisa  wHabari na Mawasilianoa TFF, Clifford Ndimbo, alisema jana mechi zote za hatua ya nusu fainali zitaanza kuchezwa kuanzia saa 9:30 mchana.

"Maandalizi ya mechi zote yanaendelea vyema, tunajua tumefika hatua ngumu ambayo kila timu inahitaji kucheza fainali," alisema Ndimbo

Ihefu yenyewe ilisonga mbele katika mashindano hayo kwa kuifunga Mashujaa FC penalti 4-3 baada ya kutoka suluhu dakika 90 za kawaida huku Coastal Union iliifunga Geita Gold bao 1-0.

Yanga yenyewe ilisonga mbele katika mashindano hayo kwa kuwafunga Tabora United mabao 3-0.

Fainali za mashindano hayo kwa mwaka huu zinatarajia kufanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite ulioko Babati mkoani, Manyara.