KMC kukomalia nafasi ya nne

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:19 AM May 06 2024
 Kocha Mkuu wa KMC FC, Abdihamid Moalin.
Picha: Maktaba
Kocha Mkuu wa KMC FC, Abdihamid Moalin.

BAADA ya kusuluhu dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Mkuu wa KMC FC, Abdihamid Moalin, ameweka wazi kuwa malengo yake na klabu anayoifundisha ni kumaliza katika nafasi tano za juu, kwa sasa akihitaji poiti 15 katika michezo mitano iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

KMC FC juzi ililazimishwa suluhu nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, mchezo ukipigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe jana, kocha huyo alisema kuelekea mwishoni mwa msimu ligi imekuwa na ushindani mkubwa na malengo yao ni kumaliza wakiwa nafasi tano za juu.

Alisema ili kufikia malengo hayo watalazimika kupambama kushinda kila mechi licha ya ugumu wa ligi kwani kila timu kwa sasa inahitaji kufikia malengo huku wengine wakipambania kujinasua katika kushuka daraja.

“Kila mechi kwetu tunahitaji kupata pointi muhimu kwa sababu malengo yetu ni kuona tunamaliza katika nafasi ya nne ambayo tupo kwa sasa, lazima tufanye vizuri katika michezo iliyosalia kuweza kukusanya alama katika kila mechi na si kupoteza zote,” alisema Moalin. 

Aliongeza kuwa anaimani na vijana wake kufanya vizuri na kufikia malengo hayo ya kuhakikisha wanatafuta pointi katika kila mechi iwe nyumbani ama ugenini.

“Tunaendelea kukisuka kikosi kujiandaa na mchezo wetu ujao, tumekuwa makini katika kila idara safu ya ushambuliaji kutumia nafasi zinazopatikana na ulinzi kutoruhusu bao kwa wapinzani tunanaocheza nao mechi zilizosalia,” alisema.

KMC FC inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi, baadaya kukusanya alama 33, kwa kushinda mechi saba, sare 12, kupoteza sita katika michezo 25 ambayo tayari imeshacheza.