Simba Queens, JKT vitani

By Saada Akida , Nipashe
Published at 10:36 AM May 05 2024
Wachezaji wa Simba Queens.
PICHA: MAKTABA
Wachezaji wa Simba Queens.

VITA ya kuwania umalkia wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania itaendelea tena leo katika viwanja vitano tofauti, mabingwa watetezi, JKT Queens watakuwa ugenini kuwavaa Alliance Girls kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini, Mwanza wakati Simba Queens watawakaribisha Amani Queens.

Mechi nyingine za ligi hiyo itakuwa ni kati ya Bunda Queens dhidi ya Geita Gold Queens itakayochezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma wakati Ceasiaa Girls watakuwa nyumbani dhidi ya Yanga Princess na Fountain Gate Princess watawakaribisha 'majirani' zao Baobab Queens kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Simba Queens inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 37 ikifuatiwa na JKT Queens yenye pointi 28.

Kikosi cha Simba Queens kinahitaji pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha katika vita ya kutwaa taji la ligi hiyo huku JKT Queens wakiendelea kupambana kusaka ushindi na kufufua matumaini ya kulibakisha taji hilo.

Vita nyingine iliyoko katika ligi hiyo ni ya  kuwania nafasi ya tatu ambayo inawindwa na Ceasiaa Queens pamoja na Yanga Princess, kila timu ikiwa na pointi 24.

Alliance Girls yenye pointi saba na Geita Gold Queens iliyojikusanyia pointi sita zinaburuza mkia katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 10 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.