ACT Wazalendo yataka tathmini mafuriko Rufiji

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:10 AM Apr 24 2024
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu.
PICHA: MAKTABA
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kufanya tathmini ya kina ya athari za mafuriko kwa wananchi wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kutafuta suluhisho la haraka.

Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa chama hicho, Doroth Semu, wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, katika ziara yake na ujumbe wake ya kutoa mkono wa pole kwa waathirika wa mafuriko Rufiji.

Amesema lililowatokea wananchi hao ni kubwa kutokana na athari hizo, hivyo kufanyika tathmini hiyo ya athari itajibu maswali yote ambayo wanaulizwa kuhusu mafuriko hayo na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

"Kwa hiyo sisi kama chama cha siasa ambacho pamoja na mambo mengine tuko kwa ajili ya wananchi, tutafurahi sana endapo hili la tathmini ya kina litafanyika na waathirika wakasaidika," amesema Doroth.

Doroth amesema chama kikiwa kinaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa, kimeamua kutembelea waathirika hao wa mafuriko wilayani Rufiji.

Amesema miongoni mwa misaada waliyoitoa ni vyakula, nguo, sabuni, mafuta ya kula, vyombo na kwamba jumla ni tani tatu na thamani ya Sh. milioni 6.5.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amesema kwa tathmini ya awali ya athari za mafuriko kwenye mkoa huo mpaka sasa vifo ni watu tisa.

"Na vifo hivi sio vimetokea kwenye nyumba zilizozingirwa hapana, vyote vimetokea wakati watu wakivuka na mitumbwi," amesema Kunenge.

Amesema mpaka sasa wamepiga marufuku wananchi kutumia usafiri wa mitumbwi na badala yake usafiri unaotumika kwa sasa ni boti ambazo zimepelekwa na wadau mbalimbali.

Kadhalika, amesema tathmini ya kina kwa ajili ya athari hizo za mafuriko inaendelea kufanywa.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, amesema kwa wilaya, vifo vilivyotokana na mafuriko hayo ni saba ambavyo vyote vimetokea wakati wa kuvuka kwa mitumbwi.

Meja Gowele, alisema mpaka sasa kata 12 kati ya 13 zimeathirika na mafuriko hayo wilayani Rufiji.

Amesema zaidi watu elfu 89,000 wameathirika na mafuriko hayo, kaya zikiwa ni 23,360 zilizozingirwa na maji na nyumba zilizoathirika ni 628.

"Lakini tunawashukuru Rais Samia Suluhu Hassan, ametuletea chakula cha kutosha, wadau mbalimbali na kwakweli wamejitahidi kutuletea misaada ya chakula na kinagawiwa kwa waathirika wote, tunashukuru sana," amesema Meja Gowele.

"Niwashukuru sana ACT-Wazalendo, kwa kuja kutushika mkono, naomba na vyama vingine vya siasa navyo vije, sisi wote ni Watanzania na tunawasaidia ndugu zetu hawa bila kuangalia dini wala itikadi ya vyama vyao."

Meja Gowele amesema wamepokea misaada ya fedha kutoka kwa viongozi na watu mbalimbali na mpaka sasa fedha waliyopatiwa ni Sh. milioni 107.7 ambayo wataitumia kusaidia wananchi hususani kwenye kilimo.