Aweso awataka wataalamu wa wizara kunusuru Bwawa la Nanja kwa haraka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:57 AM Apr 19 2024
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiongozana na Mbunge wa Monduli, Fred Lowassa kutembelea Bwawa la Nanja lililoanza kumeguka kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amefika Wilaya ya Monduli kunusuru Bwawa la Nanja ambalo ni tegemeo la Vijiji 30 katika chanzo maji pekee baada ya kumeguka kingo kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Akiwa katika eneo hilo, amesisitiza kwamba pamoja na ugumu wa kukarabati bwawa hilo wakati likiwa na maji maamuzi magumu yafanyike wataalamu wa Wizara ya Maji watumie utaalamu wao kulifanikisha hilo kwani hakuna namna nyingine.

Akizungumza na mamia wa wananchi wa Kata za Lepruko, Sepeko, na Makuyuni Aweso, ametoa maelekezo kwa Wataalamu wa Wizara kama kutumia taaluma zao kuhakikisha Bwawa hilo linakarabatiwa kwa dharula haraka kuanzia leo Aprili 19,2024 kudhibiti maji kuendelea kupotea, pili kufanya usanifu wa kina nyakati za kiangazi kusudi bwawa hilo liweze kukarabatiwa kwa uhakika zaidi.

Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fred Lowassa amesema Bwawa hilo ndio tegemeo la wana Monduli kwenye matumizi ya maji kwa Binadamu, mifugo na wanyamapori hivyo ameiomba Serikali ione namna ya kukarabati bwawa hilo kwa dharura.

Aidha, Wakizungumza katika nyakati tofauti madiwani wa kata zinazoguswa na bwawa hilo wameishukuru serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kuwafikia kwa haraka na kutafuta suluhu ya utatuzi ya changamoto hii.