Bashungwa ataka majina ya mameneja wazembe

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 10:54 AM Apr 24 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
PHOTO: MAKTABA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala, kumpatia majina ya mameneja wa kanda na mikoa wa TEMESA ambao wameshindwa kuwahudumia wananchi.

Ametoa agizo hilo jijini Dodoma baada ya kupokea malalamiko ya mara kwa mara kuhusu huduma zinazotolewa na TEMESA ikiwamo huduma ya kivuko cha Mv. Tanga, kuwa alimuagiza Katibu Mkuu kuingilia kati kubaini changamoto zinazokwamisha kivuko hicho.

“Mambo mengi ya kiutendaji yanaletwa kwa waziri na Katibu Mkuu wakati watendaji mpo na tumewaamini kusimamia taasisi zenu, hasa jambo hili lipo TEMESA. Mtendaji Mkuu kama kuna upungufu wa wasaidizi wako bora uje kwa Katibu Mkuu useme huyu hatufahi aondoke kuliko kukaa nao, maana hatimaye jumba bovu litakuangukia wewe,” amesema Bashungwa.

Pamoja na mambo mengine, Bashungwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha Amour, kuangalia namna bora ya usimamizi wa TEMESA katika huduma ya vivuko nchini ili kuleta manufaa na uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ziimarike.

Aidha, amesema TEMESA inaendelea na mikwamo na kutotekeleza majukumu yake kwa uharaka pindi tatizo linapogundulika katika vivuko na hivyo kusababisha kuzorota kwa huduma hiyo katika baadhi ya maeneo.

“Changamoto ya marekebisho ya kivuko cha Mv. Tanga yanaendelea zaidi ya siku 10 sasa, lakini leo naulizia vifaa bado havijafika, kama ‘parts’ ziko Dar es Salaam inachukua saa ngapi hadi kufika Tanga? Na sio Tanga pekee ni maeneo yenye vivuko.” 

Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, amekiri kuwapo changamoto hiyo katika kivuko cha Mv. Tanga akisema timu ya wataalam inaendelea na marekebisho ya kivuko hicho ili kuboresha huduma zake.

Katika hatua nyingine, Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha Amour kuzisimamia taasisi za Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuhakikisha zinaunda mabaraza ya wafanyakazi.