Benki ya NBC yaunga mkono jitihada kutokomeza Malaria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:51 PM Apr 24 2024
Mwenyekiti wa Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania (EMCT) Leodgar Tenga (Kushoto) akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi kufutia ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika utekelezaji wa pamoja wa adhima ya baraza hilo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania (EMCT) Leodgar Tenga (Kushoto) akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi kufutia ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika utekelezaji wa pamoja wa adhima ya baraza hilo.

Kuelekea Maadhimisho ya siku ya malaria Duniani yatakayofanyika kesho Aprili 25, 2024 mkoani Tabora, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeungana na Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania (EMCT) katika kutekeleza adhima ya baraza hilo inayolenga kutokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Hatua hiyo  inakuja wakati takwimu za serikali zikiibinisha kuwa jumla ya watu mil 3.5 waliugua malaria hapa nchini mwaka 2023 changamoto iliyosabisha vifo vya watu 1,900 miongoni mwao huku ripoti ya Shirika la Afya Duniani ikionesha kuwa vifo 95 kati 100 vya malaria duniani vilitokea katika nchi za Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo kilichoratibiwa na Benki ya NBC jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa baraza hilo Leodgar Tenga amesema licha ya dhamira ya kitaifa inayolenga kupunguza wastani wa maambukizi ya malaria kutoka asilimia 7.5 mwaka 2017 hadi chini ya asilimia 3.5 ifikapo 2025 na hatimae kutokomeza ugonjwa huo kabisa ifikapo 2030, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa rasilimali za kutosha kutekeleza afua muhimu za malaria.

“Jitihada za serikali na wadau mbalimbali katika kufanikisha hili zinaridhisha sana kwa kuwa imeendelea kuwekeza kwenye huduma za afya na elimu mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya malaria. Hata hivyo Baraza tunaona ipo haja zaidi ya wadau wengi zaidi wakiwemo wana Habari, viongozi wa sekta binafsi, serikali na asasi za kijamii katika ngazi zote kuunga mkono jitihada hizi kwa hari ana mali ili kufanikisha mpango huu… Malaria haikubaliki kabisa, Sote tuikatae na tuchukue hatua.’’ amesema Tengah uku akiipongeza benki ya NBC kuwa sehemu ya mkakati huo.

Akizungumzia baadhi ya hatua zinazozoweza kuchukuliwa ili kukabiliana na ugonjwa huo Tenga amesema kuwa ni pamoja na kuweka jitihada zaidi katika kuangamiza mazalia ya mbu, kutumia dawa ya viua wadudu sambamba na kuwapa nafasi wataalamu na viongozi mbalimbali kutoa elimu inayohusu ugonjwa huo kupitia vyombo mbalimbali vya Habari vinavyowafikia wananchi hususani wa pembezoni.

Awali akizungumza kwenye kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema ushiriki wa benki hiyo kwenye mkakati huo kwa kiasi kikubwa unalenga kukabiliana na athari za ugonjwa huo ikiwemo vifo kwa vijana, kina mama na watoto ambavyo vimekuwa vikiathiri nguvu kazi inayohitaji katika kukuza uchumi wan chi.

“Ugonjwa wa Malaria umekuwa ukisababisha watoto kutohudhuria masomo, wafanyakazi na wafanyabiashara kutofika kazini  sababu ya kuugua na hivyo kuathiri uzalishaji na hatimaye kuzorotesha ukuaji wa uchumi. Sisi kama benki tumeguswa na hili na tupo tayari kushirikiana na baraza hili katika vita hii muhimu kwa hali na mali,’’ amebainisha Sabi ambae pia ni mjumbe wa baraza hilo.

Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani yanatarajiwa kufanyika kitaifa kesho April 25 katika viwanja vya shule ya Uyui Mkoani Taboram ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambae pia ni Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania.