Itungwe sheria ya kudhibiti ubadhirifu fedha za umma

By CAG Mstaafu Ludovick Utouh , Agency
Published at 01:31 PM Mar 28 2024
CAG Mstaafu, Ludovick Utouh.
PICHA: MAKTABA
CAG Mstaafu, Ludovick Utouh.

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii ya kiuchambuzi, niliainisha mambo saba yanayokwamisha utekelezaji wa hoja za ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hata kufanya kasoro hizo kuendelea kujirudia.

Kuhusu nini kifanyike kufutwa kasoro hizo, kwa kutumia uzoefu wangu, ninapendekeza hatua sita zinazoweza kuwa msaada mkubwa wa kufikisha ukomo wa dosari hizo. Endelea...

Kutokana na mambo makuu hayo saba niliyoeleza katika toleo la jana lililozama zaidi katika kasoro endelevu zinazojitokeza kwenye utekelezaji hoja za CAG, ninapenda kuhitimisha kuwa, pamoja na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma, bado kuna maeneo kadhaa yanayohitaji nguvu zaidi kama ifuatavyo:

Moja; Ili kuongeza utekelezaji mapendekezo yanayotolewa katika ripoti za CAG, WAJIBU (taasisi anayoongoza kwa sasa) inashauri Katibu Mkuu Kiongozi kupitia uchambuzi ambao umefanyika, kuwataka watumishi wote ambao wanapaswa kuchukua hatua wajieleze ni hatua gani wamechukua na endapo ikibainika kuwa hawajachukua hatua, basi wachukuliwe hatua wao kwa kushindwa kuchukua hatua. 

Ni vyema Katibu Mkuu Kiongozi akafuata mtiririko wa kiutumishi wa kuwajibisha wahusika ili kuimarisha mfumo huo.

Mbili; pamoja na mikakati inayoendelea ya kuboresha mifumo ya ukaguzi wa ndani ikiwamo kuipatia kasma Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani, WAJIBU inaishauri serikali kuboresha mfumo wa utoaji ripoti za utendaji wa Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kwa kuitaka idara hiyo kuwasilisha ripoti zake kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali kama ilivyo sasa, lakini ripoti hiyo iwasilishwe kwa Katibu Mkuu Kiongozi ili iwasilishwe katika vikao vya Baraza la Mawaziri.

Ikumbukwe kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani anakagua mifumo ya usimamizi ya ndani ya serikali yote na si ya Wizara ya Fedha pekee, ndio maana kuna umuhimu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani kuifikia serikali yote kupitia Baraza la Mawaziri.

Kwa kufanya hivyo, kutaifanya serikali, hasa Rais ambaye ndiye kiranja mkuu wa serikali kujua udhaifu wa utendaji wa mifumo ya ndani ya usimamizi wa fedha za umma na kuchukua hatua mapema kabla ya kutolewa ripoti za CAG.

Tatu; ili kuimarisha mfumo wa sheria na kanuni zinazosimamia ukusanyaji na matumizi ya fedha za umma, WAJIBU inashauri serikali kuja na Sheria ya Ubadhirifu wa Fedha za Umma (Fraud Act) kama zilivyofanya nchi nyingi mbalimbali duniani mwaka 2006. 

Kupitia sheria hii, serikali irahisishe utaratibu wa kutambua wahusika wa vitendo vya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu pamoja na kuelekeza hatua mahsusi za kuchukua kwa watumishi hao. 

Kupitia sheria hii, serikali ipunguze hatua za kiutawala/kinidhamu za kushughulikia vitendo hivi, badala yake iweke hatua za kisheria mahsusi za kushughulikia wahusika wa vitendo hivyo vya ufisadi dhidi ya fedha na rasilimali nyingine za umma. 

Sheria kama hii ni sheria mpya iliyobuniwa na  nchi mbalimbali kwenye miaka 2000 (hasa 2006) baada ya kupitia adha ya fedha na rasilimali nyingine za umma kurubuniwa na watu wasio waaminifu katika utumishi wao serikalini. Sheria hii hivi sasa inatumika katika nchi mbalimbali kama vile Afrika Kusini, Uingereza, Marekani na Kenya.

Nne; ili kuongeza kasi ya kupambana na rushwa, udanganyifu na ubadhirifu katika sekta ya umma, WAJIBU inashauri serikali kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuharakisha uchambuzi wa ripoti za CAG ili kubaini maeneo yenye rushwa, udanganyifu na ubadhirifu wa rasilimali za taifa ili wawafikishe kwenye vyombo vya sheria watumishi wote waliohusishwa na vitendo hivyo. 

WAJIBU pia inashauri ripoti ya mwaka ya utendaji kazi wa TAKUKURU inayowasilishwa kwa Rais sambamba na ripoti za CAG kila mwishoni wa mwezi Machi, iwasilishwe bungeni kama ripoti za CAG zinavyowasilishwa na baadaye kufanywa wazi kwa umma. 

Kuifanya ripoti hii kuwa wazi kwa umma kutawezesha wananchi kuwa na uelewa wa juhudi zinazofanywa na serikali kupitia TAKUKURU katika kupiga vita na kuzuia vitendo vya rushwa nchini, hivyo kupanua nafasi ya ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa. 

Kufanya hivi pia kutaongeza imani ya wananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Tano; ili kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma, WAJIBU inashauri pamoja na mambo mengine, viongozi wa mashirika na taasisi hizo wapatikane kwa njia ya kiushindani kwa kuzingatia weledi wao katika sekta husika ya shirika/taasisi hizo na malengo mahususi ya shirika/taasisi hizo. 

Viongozi watakaopatikana kwa njia za kiushindani wawekewe malengo ya kiutendaji kwa kuzingatia faida inayotarajiwa pamoja na malengo mengine mahsusi ya kuanzishwa kwa shirika au taasisi husika. 

Vilevile, kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha mashirika yaliyoanzishwa kwa malengo ya kufanya biashara kwa madhumuni ya kutengeneza faida na kulipa gawio serikalini, yapewe mitaji ya kutosha ya uendeshaji kibiashara. 

Jitihada zote zinazofanywa hivi sasa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina za kuyapanga upya mashirika ya umma nchini (restructuring) zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wote pamoja na wadau wa maendeleo ya nchi yetu.

Sita; Serikali iendelee kutilia mkazo utekelezaji Mpango Mkakati wa Kuboresha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP – VI) pamoja na kuongeza kasi ya uundwaji mifumo ya kielektroniki kwa kutumia wataalamu wazawa. 

Vilevile, serikali iongeze juhudi za kuvutia sekta binafsi hasa wafanyabiashara na taasisi za kiraia katika kuchangia kwenye uboreshaji mifumo ya usimamizi wa fedha za umma.

Watanzania tuna kila sababu ya kusubiri kwa shauku kubwa ujio wa ripoti za CAG za mwaka 2022/23 ambazo zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa mwezi huu wa Machi 2024 na baadaye kuwasilishwa bungeni mwezi Aprili 2024. 

Serikali na Bunge zitakuwa zimefanya kazi zake za usimamizi wa utekelezaji mapendekezo ya CAG kama ilivyokuwa inahimizwa na Mheshimiwa Rais na viongozi wengine wakuu wa serikali, tutarajie kuwapo uboreshwaji katika hoja za ukaguzi katika ripoti za mwaka huu kulinganishwa na miaka iliyopita.

Vinginevyo, kama hali itakuwa mbaya kuliko ilivyokuwa mwaka jana, basi serikali ione umuhimu wa kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa hapo juu na Taasisi ya WAJIBU - Institute of Public Accountability.

*Mwandishi wa makala hii ya kiuchambuzi ni CAG mstaafu, pia alishakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na Mhadhiri wa Uhasibu Chuo Kikuu cha Mzumbe.