NIDA yatoa vitambulisho milioni 20

By Enock Charles , Nipashe
Published at 07:26 AM Apr 27 2024
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geoffrey Tengeneza,
Picha: Maktaba
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geoffrey Tengeneza,

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesajili zaidi ya watu milioni 24 tangu kuanza kwa mchakato wa usajili wa vitambulisho hivyo mwaka 2012 huku zaidi ya watu milioni 20 wakipatiwa namba ya utambulisho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geoffrey Tengeneza, alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika mchakato huo, mamlaka imesajili asilimia 79 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

Tengeneza alisema NIDA ilibadilishana takwimu na taasisi 96 za umma na binafsi kutoka Tanzania Bara na taasisi tatu kutoka Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za watu binafsi na kuwahudumia wananchi kwa urahisi.

“Hadi kufikia Februari, mwaka huu, NIDA imefanikiwa kusajili watu 24,495,804 ambao ni asilimia 79 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea katika watu 31,477,938  wenye sifa za kusajiliwa.

“Lakini pia tumefanikiwa kutoa namba za utambulisho wa taifa (NIN) kwa watu 20,832,225 ambao ni sawa na asilimia 85 ya watu waliotambuliwa na kusajiliwa. Mamlaka pia imezalisha vitambulisho 20,286,420 ambavyo ni asilimia 97.4 ya watu waliokuwa na namba ya utambulisho,” alisema.

Tengeneza alisema mamlaka hiyo imejitahidi kuwapunguzia wananchi tatizo la upatikanaji kadi za NIDA kwa kuzalisha vitambulisho kwa kasi zaidi sasa na kupunguza tatizo la upatikanaji wake jambo ambalo alikiri kuwa ni changamoto ya muda mrefu.

“Sote tulishuhudia jinsi wananchi walivyokuwa wakilalamikia kutopatikana kwa kadi hizo hali inayowakwamisha kupata huduma mbalimbali za kijamii. Tumefanikiwa kukabiliana kabisa na tatizo hili kwa kuhakikisha tunazalisha na kutoa kadi kwa watu wote waliojiandikisha.

“Kama mamlaka tulijipanga kuhakikisha tatizo la uhaba wa kadi za NIDA linapatiwa ufumbuzi kabisa kabla ya kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuweka mikakati miwili  ambayo ni utengenezaji wa vitambulisho vya NIDA kwa wingi na usambazaji kwa wingi wa vitambulisho hivyo. ,” aliongeza.

Alisema NIDA imewapa wafanyakazi wake utaalamu wa kuunda na kuzalisha kadi ili kuokoa gharama na kuokoa muda unaohitajika kutatua matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza wakati wa awamu za uzalishaji walipokuwa wakitegemea wazalishaji kutoka nje ya nchi.

“Uendelezaji wa uwezo wa ndani wa kiufundi ulituwezesha kujikwamua kutegemea makandarasi wa kigeni kuja kutatua matatizo yetu. Kwa bahati nzuri, sasa tunaweza kufanya kila kitu. Tumewawezesha wataalam wetu kujifunza jinsi ya kuboresha mifumo yetu na kuunda rejista ya kielektroniki yenye taarifa za watu,” alisema