Viongozi Afrika wasema Muungano umejenga uchumi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:53 AM Apr 27 2024
news
Picha: OMR
Baadhi ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa katika sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.

MARAIS na viongozi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU) wamesema dhamira ya waasisi wa Muungano unaotimiza miaka 60 hivi sasa, imechangia kuunganisha nchi na kujenga misingi ya kiuchumi na kijamii.

Wakitoa salamu zao jana kwa niaba ya marais wa umoja huo wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sherehe zilizofanyika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam, Rais wa Visiwa vya Comoro, Azali Assouman na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, walipongeza hatua iliyofikiwa.

Rais Assouman ambaye amemaliza muda wake wa uongozi AU, akitoa salamu kwa niaba ya umoja huo, alisema; “Ni furaha kubwa kuona ndoto na dhamira za waasisi waliounganisha nchi iliyojenga misingi ya kiuchumi na kijamii.”

Alisema Tanzania ni nchi wanayopakana nayo na ya mfano kwa amani, demokrasia na maendeleo.

“Tanzania imekuwa mwenyeji wa vuguvugu mbalimbali za kutafuta amani kwa nchi zetu barani Afrika ikiwamo nchi yangu na chama chetu.

“Sitaweza kuondoka hapa bila kuzungumzia udugu na ushirikiano kati yetu. Viongozi waliotutangulia wamejenga misingi ya kukaribisha nchi zetu kuwa na ushirikiano wa karibu, heshima kati ya nchi moja na nyingine na kutakiana mema kimaendeleo kati ya nchi zetu mbili,” alisema na kuahidi kuendelea kudumisha ushirikiano na ukaribu uliopo kati ya viongozi na wananchi kwa maslahi mapana ya mataifa hayo.

Rais wa Burundi, Ndayishimiye, akitoa salamu kwa niaba ya viongozi wa EAC, alisema: ”Kuna sababu kubwa iliyonitoa Burundi kuja na mke wangu  katika sherehe hii. Kabla ya wakoloni kufika kwetu, Waha, Wahangaza na Warundi walikuwa ndugu, walitembeleana.”

Alisema Warundi walikuwa wakienda Tanzania kuuza majembe na Waha walikwenda Burundi kuuza chumvi, hivyo si rahisi kuwatofautisha.

“Mkoloni ametutawala sote. Wakati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akipigania uhuru,  vivyo hivyo na mwana Mfalme walikwenda bega kwa bega na kupigania sambamba na kupata ushindi kwa pamoja, furaha ya watanzania ni furaha ya waburundi tupo kama mti na ganda,” alisema.

Rais Samia Suluhu Hassan, alisema Rais wa Kenya, William Ruto amemnong’oneza waluo na wamasai wa hapa na Kenya wapo sawa hawawezi kuwatofautisha, vivyo hivyo kwa Rais Zambia, Hakainde Hichilema, hawawezi kutofautisha wakifika mpaka wa Tanzania na nchi hiyo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema mambo mengi yaliyoangaliwa kama changamoto za Muungano yamepatiwa ufumbuzi na machache yapo katika hatua mbalimbali.

“Kwa niaba ya wananchi Zanzibar tunawaahidi watanzania wenzetu tutaendelea kuwa waumini wa Muungano kwa kuhakikisha unadumu na kuimarika kwa kizazi kitakachokuja baada yetu. Ninapongeza sekta zote kwa maendeleo iliyopata kwa miaka 60 ya Muungano,” alisema.