Madereva wadai kutozwa faini bila risiti

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 06:14 AM Apr 27 2024
Madereva bodaboda.
Picha: Maktaba
Madereva bodaboda.

MADEREVA na wamiliki wa bajaji na pikipiki za abiria, maarufu kama bodaboda, katika Manispaa ya Singida wamelalamikia kutozwa faini ya Sh. 30,000 katika kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya maegesho na mfanyabiashara aliyepewa zabuni na halmashauri bila risiti za malipo.

Madereva na wamiliki hao waliwasilisha kilio hicho juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ambaye alikuwa akizungumza nao katika viwanja vya Bombadia kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi. 

Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Manispaa ya Singida (CHAMWAPITA), Abiud Mlowezi, alisema: “Kero kubwa kwetu ni kuandikiwa faini ya maegesho ya Sh. 30,000 wakati hapa manispaa hakuna ‘parking’." 

Naye Mwenyekiti wa  CHAMWAPITA, Abdi Mitigo, alisema tatizo la kutozwa faini hizo za maegesho lilianza tangu 2022 na kitendo cha kutopewa risiti kinatia shaka huenda fedha hizo zinaingia kwenye mifuko ya watu. 

Kutokana na  hali hiyo, Dendego, alipiga marufuku madereva hao kulipa tozo yoyote bila kupewa risiti  kwa kuwa ni kinyume cha utaratibu wa serikali.  

Alisema ni jambo la aibu kwa watendaji wanaokusanya mapato ya serikali na kutotoa risiti wakati msisitizo mkubwa wa serikali ni kuwa malipo ya aina yoyote lazima mnunuzi apewe risiti halali ili serikali ipate mapato kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

 “Haiwezekani  kwa serikali tuwe wa kwanza kutotoa risiti hilo halipo na haitawezekana tunataka haki bin haki. Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida ukakae na mzabuni ili muweke utaribu wa kutoa risiti kama Serikali inavyoelekeza,” alisema.

 Dendego pia alimwagiza mkurugenzi wa manispaa kukaa na viongozi wa madereva hao kuwasaidia kuanzisha Chama cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili kukopa fedha kwa ajili ya kununua vyombo vyao vya usafiri badala ya kuendesha vya watu hali ambayo itawasaidia kuboresha maisha yao.

 Alisema kwa sasa chama chao ambacho kina zaidi ya wanachama 4,000 kinaweza kukopeshwa na kurejesha mikopo kwa haraka kama watendaji watawasaidia kuanzisha SACCOS yao.