Watumishi wafundwa mbinu kabla kustaafu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:24 AM Apr 27 2024
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo, amewataka watumishi wa umma kutimiza majukumu yao kwa wakati na weledi na kuwekeza kwa ajili ya maisha ya uzeeni ili kuepuka usumbufu katika kipindi cha kustaafu.

Omolo alitoa wito huo juzi wakati wa Mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha mwaka 2023/24, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Natu Mwamba, katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam.

‘’Ni vyema ukamaliza majukumu yako kwa wakati husika ili angalau miezi miwili kabla ya kustaafu kila kitu chako kiwe sawa. Si mpaka siku chache kuelekea kustaafu bado una majukumu mengi hujayakamilisha”, alisema.

Omolo alisisitiza kuwa ni vyema watumishi wakawekeza wakati wakiwa kazini ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uwezo wa kuendesha maisha na kukidhi mahitaji yao muhimu baada ya kustaafu.

‘’Mada ya uwekezaji ni muhimu sana kama ilivyowasilishwa wafikishieni watumishi wote umuhimu wa kuwekeza, tunaweza kuwekeza UTT AMIS, bima na benki lengo ni kuhakikisha kuwa tunavyofanya kazi tuwe na namna ya kuwekeza kwa ajili ya familia zetu na kujiandaa kustaafu’’, alisisitiza.

Naibu Katibu Mkuu aliongeza kuwa kuwa uongozi wa wizara hiyo utahakikisha unatatua changamoto mbalimbali zinazoweza kukwamisha utendaji wa watumishi na kuhakikisha wanapata stahiki.

Pia aliwataka watumishi hao kushiriki kikamilifu katika kutekeleza bajeti iliyopitishwa kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali za kuleta maendeleo ya nchi.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha hufanyika kila mwaka ambapo hutoa fursa kwa watumishi kujadili  na kuwasilisha changamoto mbali mbali katika maeneo ya kazi ili ziweze kutatuliwa.