Lissu aibua sakata bei sukari kupanda

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 07:01 AM Apr 27 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, akiongoza maandamano Babati.
Picha: Jaliwason Jasson
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, akiongoza maandamano Babati.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, ametishia kutaja hadharani vigogo wanaosababisha bei ya sukari na bidhaa zingine kuwa kubwa.

Amebainisha kwamba vigogo hao wanawabana waagizaji wa bidhaa waongeze cha juu kwa maslahi yao. 

Lissu alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi wa Babati mara baada ya kushiriki maandamano. 

"Waagizaji wa sukari  wanaambiwa wakiagiza kila kilo moja iwepo Sh. 200 ya kiongozi  kutoka Ikulu," alidai na kusema endapo watabisha hilo, kuna  siku atawataja wote wanaohusika, hivyo  kusababisha bei ya sukari na bidhaa zingine kupanda.  

"Bei ya sukari inaongezeka kwa kuwa bidhaa zote zinaongezwa cha juu kwa ajili ya viongozi ndiyo maana tunaumia kwa bei za bidhaa kupanda,” alisema. 

Pia alisema tozo na unyanyasaji unaofanyika kwa wananchi unaanzia serikalini kwa kuwa hakuna kinachopitishwa na Bunge bila kuanzia huko akitolea mfano tozo za simu. 

Kuhusu kikokotoo alisema  kitaendelea kuwaumiza wafanyakazi kwa kuwa hawawezi kugoma kwa sababu Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limerithiwa kutoka iliyokuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA) iliyokuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Lissu alisema iwapo katiba ingekuwa nzuri, wafanyakazi wasingeingia  kwenye matatizo ya kikokotoo. Alisema katiba mpya ndiyo itaondoa umungu mtu na kuleta Bunge ambalo litakuwa huru. 

Katibu Mkuu wa zamani wa CHADEMA,  Dk. Willibroad Slaa, akihutubia mkutano kwa njia ya simu, alisema licha ya kuwa na miaka 60 ya Muungano bado mjamzito akienda kujifungua anaambiwa alipie Sh. 100,000. 

Dk. Slaa aliwaomba radhi kwa kutokushiriki maandamano kutokana na shida ya miguu inayomsumbua. Aliwaomba kujiandikisha kwa njia ya kidijitali ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa. 

Wakili Boniface Mwabukusi aliibua sakata la bandari kwa kusema wapende wasipende bandari iliyouzwa itarudishwa. 

Mwabukusi alisema wataandaa maandamano ya kurudisha bandari ambayo itarudishwa kwa nguvu ya umma.