Kanisa lajitosa kukusanya taka, kutumia Sh.milioni 300

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 06:46 PM Apr 24 2024
Askofu wa Kanisa la Anglikana, dayosisi ya Morogoro, Godfrey Seheba.
Picha: Ashton Balaigwa
Askofu wa Kanisa la Anglikana, dayosisi ya Morogoro, Godfrey Seheba.

KANISA la Anglikana Tanzania dayosisi ya Morogoro, limetoa msaada wa zaidi ya Sh.Milioni 300 kwa ajili kuanzisha mradi unaofafahamika kama ‘Taka kwa Thamani,’ wenye lengo la kupunguza uchafu na taka ngumu zinazozalishwa katika Manispaa ya Morogoro.

Kanisa hilo kupitia shirika lake la Huduma Kamilifu ya Jamii (DDSCDO), limesema mradi huo wa miaka miwili unaoanza mwaka huu, utaendeshwa kushirikiana na manispaa hiyo na kwamba utasadia kutoa ajira kwa wanawake, vijana na makundi maalumu kupitia vikundi kazi pamoja na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi huo kwa wadau mbalimbali, Askofu wa kanisa hilo dayosisi ya Morogoro, Godfrey Seheba, amesema fedha hizo zimetolewa kupitia ufadhili wa Norwegian Church Aid (NCA) Tanzania.

Askofu Seheba ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya DDSCDO, amesema mradi huo una malengo ya kuchangia ufanikishaji wa sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, pamoja na vipaumbele vitatu ukusanyaji wa mapato, ukusanyaji taka na kuweka manispaa safi pamoja na usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Naye, Meneja Programu kutoka DDSCDO, Pius Ngirwa, amesema kuanzishwa kwa mradi huo kunatokana na uzalishwaji wa taka ngumu kwa wingi katika Manispaa ya Morogoro, ambapo imeelezwa kuwa, kwa siku; huzalishwa tani 377 za taka huku asilimia 30 pekee ndiyo hukusanywa.

Kwa mantiki hiyo, kiasi kikubwa cha taka hakikusanywi na hivyo kuwa kero na kusababisha uchafuzi wa mazingira.

“Mradi huu sasa unaenda kupunguza taka zote zilikuwa zikibaki katika Manispaa ya Morogoro, kwa kuwa matokeo ya taka ngumu yamekuwa yakisababisha kuharibu baadhi ya miundombinu na kuhatarisha maisha ya viumbe hai,” amesema Ngirwa.

Amesema mradi huo pia unaenda kuwezesha udhibiti wa taka endelevu kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo mashine itakayowezesha uchakataji wa taka hasa zile za plastiki.

Ofisa Miradi toka NCA Tanzania, Oscar Halazya, amesema taka hizo ikiwemo za plastiki zitaongezewa thamani na kutengeneza ajira kwa vijana kwa kwa kuzalisha chupa za maji na vitu vingine kama fagio.

Amesema zile taka zinazooza yatatengwa maeneo ambayo yatakuwa na uwezo wa kuchakata na kutengeneza mbolea ya mboji ambayo baadae itauzwa kwa wakulima ili kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo huku nyingine ikitumika kutengeneza vyakula vya wanyama.

Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti na Usafirishaji wa Taka katika Manispaa ya Morogoro, Samuel Kisubi, amesema wamefurahishwa na mradi huo, huku akiamini kuwa taka nyingi zinazozalishwa na za kuoza katika masoko makubwa kama ya Kingalu, Mawenzi na Mjimpya zinaweza sasa kutengezwa kuwa mbolea wakati za plastiki zitazalishwa vitu kama chupa za maji.