Nyumba kijiji cha wavuvi zabomoka

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:57 AM Apr 24 2024
Baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na mvua.
PICHA: MAKTABA
Baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na mvua.

WANANCHI wa Kijiji cha Wavuvi, Mtoni Chaurembo, Temeke mkoani Dar es Salaam, wako hatarini baada ya baadhi ya nyumba zao kusombwa na maji kutokana na sehemu ya mtaro uliojengwa maeneo hayo kubomoka.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, baadhi ya wananchi hao walisema tatizo hilo limechangiwa na namna mtaro huo ulivyojengwa.

Amani Mpakasini, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amesema shida iliyoko kuna Barabara za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) zilizojengwa ndani ya mitaa ambako maji ya mitaro yake imeelekezewa baharini waliko wao.

“Njia ya kwanza ya maji waliiacha wakatengenezea njia sehemu nyingine, lakini shida inayokuja ni kule maji yanakoelekea baharini. Mtaro umetengenezwa kwa zege wameweka kama milimita nane tu kisha wakajengea matofali ambayo yamesomwa na maji.

“Hali hii imesababisha maji kuathiri nyumba zilizoko eneo hili. Nyumba moja imedondoka yote na nyingine kibaraza kimeondoka na pia, kuna yadi imeathiriwa. Kama hakutathibitiwa mapema maana yake athari itakuwa kubwa zaidi,” amesema.

Amesema mkandarasi aliyejenga mtaro huo huku unakomalizikia ili maji yaende baharini ndiko kwenye shida kwa kuwa maji ni mengi yanayosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha.

 “Walikuja mbunge na diwani walituambia imetengwa Sh. milioni 11 lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea. Ujenzi huu haujamaliza hata mwaka. Una miezi saba kama sikosei,” amesema mwananchi huyo.

Mpakasini ameomba serikali kuangalia uwezekano wa kuukarabati mtaro huo haraka ili kupunguza athari kwao kwa kuwa, mvua zinazoendelea kunyesha zinasababisha maeneo hayo kuliwa na maji na udongo kumeguka kuelekea katika makazi.

Moja wa wafanyakazi wa yadi iliyoathiriwa na maji ya mtaro huo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema mtaro huo ulijengwa, ili kukusanya maji maeneo mbalimbali na kuyapeleka baharini.

“Kila siku tatizo linaongezeka. Shida kubwa ni waliotengeneza mtaro huu yawezekana kuna mahali walikosea unavunjika tu.

“Hili eneo kuna bahari kwa hivyo maji yanachimba na tayari kumetengeneza shimo ambalo linatokana na maji ya mtaro huu,” amesema.