Rais Samia awa mbogo kuvuja kwa mapato halmashauri, ataka ubunifu

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 10:45 AM Apr 24 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
PICHA: MAKTABA
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amekemea vitendo vya uvujishaji mapato vinavyoendelea katika mamlaka za serikali za mitaa nchini, huku akiwatwisha mzigo mamea, wenyeviti wa halmashairi na wakurugenzi kubuni vyanzo vipya vya mapato kwenye maeneo yao.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jana visiwani hapa, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alisema halmashauri lazima zibuni vyanzo vipya vya mapato  ili kujenga ufanisi pamoja na kuleta maendeleo ya wananchi.

“Lazima watendaji tuwe wabunifu katika halmashuri zetu. Lazima  tubuni mbinu na njia ambazo tutahakikisha tunasimamia kwa asilimia kubwa katika kukusanya mapato na kwa matumizi yaliyopitishwa kwa maendeleo ya wananchi,” amesema.

Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri na watendaji kuwa waadilifu katika ukusanyaji wa mapato ya serikali hasa katika matumizi ya mifumo ya kisasa.

Amesema kuna  taarifa za matumizi  ya mashine feki ya ukusanyaji mapato jambo ambalo linaikosesha serikali mapato mengi.

“Tunazo taarifa uwepo wa mashine feki za kukusanyia mapato. Lakini pia kuna  mashine ambazo taarifa za  mapato haziingii lakini pia zipo mashine zinazimwa, hivyo watu hawa ambao si waadilifu watachukuliwa hatau stahiki,” amesema.

Aidha amewataka wakurugenzi wa halmashauri kusimamia vyema miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao ili ikamilike kwa wakati.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuna miradi kama vile ya afya , elimu, maji na miundombimu ya barabara inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali, hivyo haina budi kusimamiwa  kwa kufika katika maeneo ya miradi hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa na Idara Maalum ya SMZ, Masoud  Ali Mohamed, amesema  ALAT kwa Tanzania Bara na ZLGA kwa Zanzibar ni taasisi muhimu katika nchi na kwamba kufanikiwa kwazo ni mafanikio ya serikali.

Amesema kutofanya vizuri kwa taasisi hizo kunasababisha kufeli  kwa kila sehemu ya  serikali kwa  kuwa serikali inaanzia ngazi za chini. 

“Unaweza kuwa na sheria nzuri, posho nzuri lakini kama hakuna utashi wa kisiasa basi hatutafanikiwa, hivyo ni vyema tukawa na msingi mzuri wa utendaji kazi katika mamlaka za serikali za mitaa,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa ALAT, Murshid Ngezi, akitoa taarifa ya jumuiya hiyo, amesema kitendo cha serikali kuongeza posho kwa wakurugenzi, madiwani na watendaji wa serikali za mitaa ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi zao ni cha kupongezwa.

Amesema nyongeza hiyo ya posho itasaidia watendaji hao kufanya kazi kwa ufanisi lakini pia kujitegemea katika halmashauri zao.

Pia ameipongeza serikali kwa hatua ilizochukua katika kuleta mabadiliko kwenye  halmashauri na kuzifanyia kazi changamoto zilizoko.

Kadhalika,  amezipongeza halmashauri zote  ambazo zimefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuziomba zingine ambazo hazijafanya vizuri, kuiga mfano wa hizo 

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo, amesema benki hiyo itendelea kuisaidia serikali katika ngazi za chini kwenye miradi mbalimbali ya kijamii.

Amesema benki hiyo inachopata kutoka kwa wananchi, inakirejesha kupitia miradi mbalimbali ikiwamo kusaidia mikopo kwa vikundi vya ujasiriamali.