Ummy Mwalimu aona changamoto maeneo ya 'kupasha' mwili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:21 PM Apr 24 2024
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

WAKATI Tanzania ikieleza namna inavyoungana na mataifa ya Afrika, kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD's), Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema miundombinu kwa ajili ya mazoezi ni kikwazo.

Amesema mara kadhaa, amepokea malalamiko kutoka kwa wadau wa mazoezi ya kupasha mwili 'jogging', hususan maeneo ya mijini, wakieleza jinsi wanavyopata vikwazo. 

*Mara kadhaa nimepokea malalamiko kutoka kwa wanaofanya mazoezi ya mwili, hawa jogging, wanasema Waziri wakati unahamasisha tufanye mazoezi kuepuka NCD's maeneo ni kikwazo.

"Wanasema wanalazimika kutumia barabara ambazo pia hutumika kwa ajili ya vyombo vya moto na kuwa hatari kwao. Hivyo NCD's ni suala mtambuka, Wizara ya Ujenzi, nao wanaguswa," anasema Ummy.

Ummy, amesema hayo jana, jijini Dar es Salaam, akifungua kongamano la kimataifa barani Afrika dhidi ya NCDs ‘PEN Plus’, lililokutanisha washiriki 300 kuazimia mbinu kukabili, kisukari aina ya kwanza, selimundu na magonjwa ya moyo kwa watoto 

Amesema kwamba nchini NCD's, huchangia takribani asilimia 70 ya magonjwa mengine kama vile figo na moyo, akisema asilimia tisa ya Watanzania wanaugua kisukari huku asilimia 15 wanaugua presha.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini, Dk. Charles Sagoe-Moses, alisema NCD's, husababisha mamilioni ya vifo kwa mwaka, ambavyo vingeweza kuepukika, kutokana huduma duni kukabili magonjwa hayo.

“Takribani vifo 100,000 husababishwa na sababu nne; kisukari aina ya kwanza, selimundu, magonjwa ya mfumo wa hewa na moyo kwa watoto. Katika nchi nyingi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, huduma za matibabu kwa NCD's hupatikana tu kwenye hospitali za rufani.