ATCL yapokea ndege ya 14, Majaliwa aonya ukatishaji ruti

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:58 AM Mar 27 2024
Ndege mpya ya kisasa ya ATCL aina ya Boeing 737-9 MAX.
PICHA: HAKI NGOWI
Ndege mpya ya kisasa ya ATCL aina ya Boeing 737-9 MAX.

KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL), imepokea ndege ya 14 huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitoa maagizo saba likiwamo la kupunguza ukatishaji wa ruti za ndani.

Majaliwa ametoa maagizo hayo jana Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya kisasa aina ya Boeing 737-9 MAX.

Waziri Mkuu amewaagiza viongozi na watendaji wa shirika hilo kupunguza kukatisha ruti za safari za ndege nchini ili kuleta matumaini makubwa kwa watumiaji wa ndege hizo.

Pia amewaagiza kuhakikisha ndege zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya utafiti wa kutosha wa masoko kabla ya kuzipeleka.

Maagizo mengine ni wahakikishe mikoa yote inaunganishwa na safari za ndege na kuendelea kutafuta fursa za safari za kimataifa ili kuongeza fedha za kigeni.

Kwa upande wa Wizara ya Uchukuzi, Majaliwa ametaka kusimamia ipasavyo kampuni hiyo  ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaendelea kuleta matokeo chanya.

“Watumishi wetu ongezeni uzalendo na kila mmoja athamini kazi inayofanywa na serikali. Muwafichue  wale wote wenye nia ovu ya kuhujumu uwekezaji huu pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo katika maeneo yetu ya kufanyia mauzo,” ameagiza.

Kadhalika ameitaka wizara kuandaa mpango wa kuongeza watalaam wazalendo ambapo mbali ya kupeleka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), waje na ubunifu kupitia vyuo vingine vya ndani kwa fani zinazohusika.

Maagizo mengine ameyatoa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) akitaka waongeze udhibiti wa usalama wa ndege kwa kuhakikisha wahudumu na wahandisi wanakuwa na sifa za kuhudumu ndege za kimataifa.

“Saba, taasisi na wadau wote katika viwanja vya ndege wahakikishe wanashiriki kikamilifu na kuwa sehemu ya kuimarisha huduma hii,” aliagiza na kusema serikali itaendelea kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina ili iendelee kusimamia bodi za taasisi za serikali kufikia malengo.

“Hivi karibuni tutaanza safari ya ndege ya Dubai na Afrika Kusini. Katika kipindi cha miaka mitatu hatuwezi kuacha kuwaambia mafanikio ujenzi wa reli ya kisasa hivi sasa umefikia kilomita 2102,” amesema.

Amesema wakati serikali ikinunua ndege, wanaimarisha ujenzi wa viwanja vya ndege, kikiwamo cha Msalato kitakachounganisha safari za ndani na mataifa ya nje ya nchi na gharama za ujenzi Sh. bilioni 360 ambao umefikia asilimia 54.01 na unatarajia kukamilika Novemba 2025.

Pia amesema wanakiimarisha Kiwanja cha Julius Nyerere Dar es Salaam ili kukifanya kuwa kitovu cha usafiri wa anga Afrika Mashariki kwa kuongeza miruko katika mataifa mbalimbali.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya NIT ili kutoa mafunzo kwa marubani na kupunguza uhaba wao.

Pia amesema chuo hicho kimewezeshwa mitambo ya kisasa ili kuzalisha wahandisi na mafundi mchundo kuondoa uhaba wa wataalam katika sekta ndogo ya usafiri.

Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, amesema kampuni hiyo inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ulioanza 2022/23 na utamalizika mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema mpango huo unahusisha mpango wa tatu wa taifa wa miaka mitano 2021/22 -2025/26 na wanatarajia kuwa na ndege 20 ikiwamo hiyo iliyopokelewa ambapo hadi sasa ATCL ina ndege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji ikiwamo ndogo iliyokuwako kabla ya ufufuaji na kufanya kuwa na ndege 15.

Amesema ndege ya 16 ambayo ni ya masafa marefu inatarajiwa kupokelewa mwezi Aprili, mwaka huu, na ya jana ni kwa ajili ya safari za masafa ya kati.

Amesema uwapo wa ATCL umechochea matumizi ya usafiri wa anga na kufanya kutoonekana ni kitu cha anasa na mahitaji ya miruko ndani ya nchi ni makubwa na bado kuna uhitaji katika baadhi ya vituo vinavyotarajiwa kufunguliwa.

“Ajira zimeongezeka kutoka 175 wakiwamo marubani ni  13, wahandisi 27 na watumishi wengine 131 kwa mwaka 2016  hadi ajira 780 wakiwamo marubani 117, wahandisi 151 na watumishi wengine 512 kufikia mwezi Februari 2024,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Rais Samia anapotimiza miaka mitatu ya uongozi, wana kila sababu ya kutembea kifua mbele.

“Kwa niaba ya chama na nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa RC Dar es Salaam (Albert) Chalamila hapa, amenifurahisha. Kuna kasumba ya ujinga unaoendelea ya kutaka kumtofautisha Dk. Samia (Suluhu Hassan) na Dk. (John) Magufuli huwezi kuwatenganisha hawa watu.

“Na viongozi wengi wanafiki wanaotaka kujipendekeza kwa Rais Samia kila wakipata jukwaa wanataka kumfanya (Samia) kama si sehemu ya Dk. Magufuli.

“Kama msemaji wa chama, tuna ilani, kila anachofanya Dk. Samia ndicho alichofanya Dk. Magufuli, walizunguka nchini nzima kutafuta kura, huwezi kuwatenganisha na Waziri Mkuu wao yule pale, Kassim Majaliwa.

“Ningetamani leo iwe mwisho wa unafiki wa viongozi na wanasiasa uchwara wanaopambana kuwatenganisha viongozi hawa, mafanikio haya tunasherekea wote,” amesema Makonda.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Albert Chalamila, amesema ni heshima kwa Rais Samia kuendelea kuyafanya mambo ambayo waliyokwisha kuyafanya (Samia na Magufuli).