Baba wa binti aliyeuawa kisha kufukiwa chumbani afunguka

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 11:28 AM Mar 30 2024
Mwili wa Beatrice Mgongolwa (32), baada ya kufukuliwa katika nyumba ambayo alikuwa akiishi na mume wake aliyemuua na kisha kumzika ndani.

BABA mzazi wa marehemu Beatrice Mgongolwa (32), Mzee Talius Mgongolwa, ambaye mwanawe anadaiwa kuuwawa na kufukiwa katika chumba alichokuwa anaishi na mwanamume, ameeleza namna alivyomtafuta binti yake zaidi ya mwaka bila mafanikio.

Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na mwanamume wake, Januari Mosi, mwaka huu, katika Kijiji cha Kimamba A, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, na kugundulika mwezi Machi 22, mwaka huu.

Mgongolwa akizungumza na mwandishi wa habari hii, alisema tangu Machi, 2022, alikuwa anamtafuta binti yake bila mafanikio.

Alisema alifanya jitihada mbalimbali za kumtafuta mtoto wake ikiwamo kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha TPC, kilichoko kijiji wanachoishi cha Magogini mkoani Kilimanjaro bila mafanikio.

Mgongolwa alisema baada ya taarifa  hiyo polisi waliendelea kumtafuta katika vijiji vya karibu na eneo analoishi hakufanikiwa kupata taarifa kwa zaidi ya mwaka.

“Hakuwa na simu ndio maana nilikuwa ninapata shida ya mawasiliano naye. Mwaka jana nilikata tamaa nikasema basi huko alipo siku moja atarudi maana anapajua nyumbani.

“Nimemtafuta sana tatizo hakua na namba za simu. Hatimaye taarifa ya kifo cha binti yangu nikazipata kupitia kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mselesi iliyoko Wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

“Binti wa marehemu aliulizwa huko Kilosa mlikuwa mnakaa kijiji gani (Moshi) akawajulisha na shule aliyokuwa anasoma ndipo wakamtafuta Mwalimu Mkuu wa Shule hii.

“Mwalimu Mkuu naye aliulizwa kama anaifahamu familia ya marehemu (binti yangu) ndipo alipokwenda kwa Mtendaji wa Kijiji kuniulizia akapatiwa namba zangu akanipigia simu akaniambia ninahitajika kwa huyo mwalimu,” alisema.

Alisema wakati akipokea taarifa hizo alikuwa katika shughuli zake za kilimo na alipoitikia wito ndipo alipoelezwa habari za kifo cha mtoto wake.

“Tukio hilo lilinishtua nikajiandaa kwenda Kilosa ambapo zilifanyika taratibu na kunipatia mabaki ya mwili wa marehemu na kuzika Machi 25, mwaka huu,” alisimulia.

Alisema awali (binti yake) ambaye ni wa pili kuzaliwa kati ya watoto wanane alionao, alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha sukari cha TPC kilichoko mkoani Kilimanjaro.

Baada ya kugundulika kwa mauaji hayo Machi 22, mwaka huu, siku tano mbele mtuhumiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro akikabiliwa na mashtaka manne.

Mashtaka hayo ni kuua, kubaka, kuwachoma watoto na vitu vyenye ncha kali katika miili yao ikiwamo sehemu za siri.