Maafa ya mvua: Apishana na gari lake likisombwa na maji

By Godfrey Mushi ,, Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 11:25 AM Apr 12 2024
Mwonekano wa juu wa eneo la Kisongo, kata ya Matevesi, wilayani Arumeru, mkoani Arusha, baada ya mvua kubwa kunyesha usiku wa kuamkia jana na kusababisha mafuriko yaliyofanya uharibifu wa vitu mbalimbali.

HAKUNA kilichobaki. Ndivyo inavyoweza kuelezwa, baada ya mvua iliyonyesha kwa saa saba katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, kusababisha maafa ya mafuriko yaliyosomba magari, vyakula na vyombo vya ndani, mashamba na kuacha watu bila makazi, huku mtoto mwaka mmoja na nusu, akiokolewa kwa kutupwa juu ya bati.

Wafanyabiashara wamepoteza mali, bidhaa za ujenzi madukani, maghala ya kuhifadhia mazao na pembejeo za kilimo baada ya kusombwa na mafuriko hayo.

Baadhi ya madaraja eneo hilo la Kisongo, Kata ya Mateves, yamejaa miti na mawe makubwa yaliyotokea milimani. Magari yaliyokuwa yameegeshwa kando ya maduka na barabarani nayo yamesombwa na maji na kuharibiwa.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Marko Ng'umbi, amethibitisha hadi sasa kaya 157 zimeathiriwa na mafuriko hayo.

Kati ya familia hizo, kaya moja yenye watu zaidi ya 10, hawana makazi baada ya nyumba yao kubomoka ukuta wa upande mmoja huku upande mwingine ukiwa na nyufa.

"Hii ni hatari kuendelea kuishi hapa, wameenda kwa ndugu zao eneo la Murombo kuishi kwa muda wakati wakipisha kipindi hiki cha mvua kiishe," alisema Ngumbi anayekaimu nafasi hiyo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Emanuela Kaganda.

Pia, ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwenda kuzibua kalavati zote zilizozibwa na uchafu ili kuruhusu maji.

WAATHIRIKA WAFUNGUKA 

Mkazi wa Kisongo, Tatu Kisaburi, amesema mafuriko hayo yamesababisha apoteze kila kitu kilichokuwamo kwenye nyumba yao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Ojung’u Salekwa, amesema mvua hiyo ilioanza kunyesha saa 2:30 usiku, Aprili 10.

"Kuna familia moja ya mtoto mchanga, iliokolewa na msamaria mwema, ambaye aliwaokoa mama na mtoto. Hali ya mtoto huyo kwa sasa sio nzuri na wamekimbizwa hospitalini," amesema.

Aidha, amesema sababu nyingine za mafurikio hayo kwenda makazi ya watu ni baadhi ya watu kujenga kwenye njia za maji, na wengine kutupa taka kwenye njia za maji na kuziba mitaro.

Salekwa amesema, watachukua hatua kuanzia sasa za kuwashawishi watu wote waliojenga kwenye njia za maji na makorongo kuondoka kwa hiari.

Moja ya magari yaliyoharibiwa na mvua.
Diwani wa Kata ya Kisongo, Godson Loning’o, amesema mafuriko hayo yameacha hasara kubwa katika eneo hilo la Kisongo, baada ya kusomba gari la Mwenyekiti wake wa Serikali ya Kijiji.

Nipashe ilipozungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Engorora, Justine Joel, amesema gari lake lenye namba za usajili T.134 DFK, aina ya Toyota IST ilisomba na kukutana nayo kwenye njia panda, akitoka ofisini kwake kurudi nyumbani.

"Tulipovuka eneo la ofisi ya kijiji, ghafla nilikutana na maji mengi, ambayo sijawahi kuyaona eneo hili tangu nizaliwe, ambayo yalisababisha gari langu kuzima," amesema.

Amesema milango iligoma kufunguka, hali iliyowalazimu kutokea kwenye madirisha ya gari na kusombwa na maji, wakiwa wameshikana yeye na abiria wake Godwin Mollel.

Mmoja wa wafanyabiashara waliopoteza bidhaa, Wilson Pelo, alisema alikuwa ameshusha malori mawili yaliyokuwa na shehena ya mifuko ya saruji juzi. “Nalia kwa sababu nimebaki masikini, Shilingi milioni 10 zimeteketea," amesema. 

SIMULIZI MAMA ALIYEOKOLEWA NA MTOTO

Lidya Mollel, mkazi wa Kijiji cha Ngorbob, amesema yeye na mwanawe mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu waliokolewa na msamaria mwema baada ya kumpandisha juu ya ukuta na kumrusha mtoto wake juu ya bati, ambako alinyeshewa na mvua hadi ilipokatika.

“Nilikuwa nimelala na mwanangu kitandani, kidogo nikaona maji yameingia ndani, nikaanza kupiga kelele uwii! mtoto wangu, ghafla maji yakajaa kitandani mtoto akaanza kuelea kwenye maji. Nilikuwa nalia nisaidieni mtoto wangu jamani, nakufa na maji na mtoto.

“Saa hiyo maji yalikuwa yamejaa ndani na vitu vyote vimesombwa; nguo na godoro vyote vimetolewa na maji nje.” 

Siku nne zilizopita, watu wawili wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Ilkirevi, Kata ya Olturoto, Wilaya ya Arumeru, walipoteza maisha, baada ya nyumba waliyokuwa wamelala usiku wa manane kuangukiwa na uzio wa jirani yao, baada ya mvua kubwa iliyonyesha kusababisha ardhi kumong’onyoka na kuleta maafa.

Waliopoteza maisha ni baba mzazi wa familia hiyo, Loriv Noah na mwanaye Glory Noah, huku mama wa mtoto huyo (jina lake halijatambuliwa) akinusurika baada ya kuangukiwa na ukuta.

Juzi, pia, Mbunge wa Arumeru wa Magharibi (CCM), Noah Lembrice, akizungumza na wakazi wa Ngaramtoni, alipokea taarifa za watu wengine wawili kusombwa na mafuriko kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Olevolosi kilichoko Kaya ya Kimnyak.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Emanuel Ngailuva, amemweleza Mbunge huyo kuwa wamepata changamoto ya kumpoteza kijana wao, baada ya kusombwa na mafuriko katika Mto Seliani, ambao umefurika na hauna kivuko.

Lakini pia kwenye Kata ya Ilkidinga katika Jimbo la Arumeru Magharaibi mwananchi mwingine anadaiwa kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo.