PAC yataka majibu zaidi mradi wa maji Buchama - Tinde

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:59 PM Mar 28 2024
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali PAC Japhet Hasunga akizungumza kwenye ziara ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria wilayani Shinyanga.
PICHA: MARCO MADUHU
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali PAC Japhet Hasunga akizungumza kwenye ziara ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria wilayani Shinyanga.

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya hesabu za Serikali (PAC), inaweza kuiweka Wizara ya Maji ‘kikaangoni’ baada ya kubaini baadhi ya vijiji katika mradi wa tenki la maji kutoka Ziwa Victoria wa Buchama - Tinde, wilayani Shinyanga; havina maji.

Ndipo hoja ya kutaka kujiridhisha kama mradi huo unalingana na dhamani ya fedha Sh.bilioni 24 zilizotolewa kugharimia mradi huo, ikaibuliwa na Japhet Hasunga, ambaye ni makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, baada ya kamati yake kuutembelea mradi huo leo Marchi 27,2024.

Kwa mujibu wa Hasunga, mradi huo ulikusudia kufikia vijiji 34 vikiwemo 22 kwa upande wa Shinyanga na 12 Sherui, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji karibu na hivyo kumaliza tatizo la changamoto hiyo.

“Sisi ukituambia mradi huu ulikuwa ni kusanifu na kujenga maana yake ni kwamba hakutakuwa na fedha za nyongeza, kazi yetu ni kuona fedha zilizotolewa Sh.bilioni 24 zimetumikaje katika mradi huu na kama vijiji vingine havina maji tutapata majibu kutoka Wizarani,” amesema Hasunga.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Tito Alex ambaye ni mhandisi kutoka Wizara ya Maji, amesema mradi huo umekamilika kwa awamu ya kwanza na unatarajia kutoa huduma kwa watu zaidi ya laki moja ili kusogeza huduma karibu kwa wananchi.

Naye mjumbe wa kamati hiyo Ravia Faina ambaye pia ni Mbunge wa Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja, amesema wananchi wa kijiji lilipojengwa tenki la maji Kijiji cha Buchama, wanapaswa kupewa kipaumbele cha huduma na siyo kupitwa na Mradi huo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tinde, Jafari Kanolo ameiomba kamati hiyo kusaidia ili wananchi wa Kijiji cha Buchama, wapate huduma ya maji safi na salama, kwa kuwa mradi huo umejengwa katika eneo hilo na wao ndiyo waangalizi wakuu.