Utouh: Kuna ulegevu kisheria kuwajibisha wanaotajwa ripoti za CAG

By CAG Mstaafu Ludovick Utouh , Agency
Published at 02:24 PM Mar 27 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali Charles Kichere.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali Charles Kichere.

WATANZANIA waipendao nchi yao na wanaoitakia maendeleo chanya, wanasubiri kwa shauku kubwa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 zitakazowasilishwa bungeni mwezi Aprili 2024 na kuwa wazi kwa umma.

Katika ripoti za mwaka 2021/22 zilizowasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan Machi 29, 2023, mbali na kuwa kulikuwa na uboreshwaji mkubwa wa hati za ukaguzi zilizotolewa na CAG, bado kuliripotiwa vitendo vingi vya matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma. 

Akiongea baada ya kupokea ripoti hizo, Rais Samia alionesha kukasirishwa na hali hiyo na kuagiza wahusika wa vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.

“Nadhani tumezubaa kwenye “punitive measures”, hatuchukui hatua kwenye adhabu, ingekuwa tunachukua hatua haya yasingeendelea. CAG wewe majalada unampelekea Kamishna wa Mashtaka (DPP), ninaomba kasi ya adhabu za kisheria iongezeke," alisema Rais Dk. Samia siku hiyo.   

Mwishoni mwa mwezi Machi 2024, itakuwa ni mwaka mmoja umeisha tangu ripoti za CAG za mwaka 2021/22 zipokewe na Rais na kuwasilishwa bungeni. Sasa ni muda wa kupokea ripoti mpya za CAG za mwaka 2022/23. 

Shauku iliyopo kwa Watanzania ni je, hali ya mwaka huu itakuwa tofauti na miaka mingine? Je, maagizo ya Rais yametekelezwa? Je, hali ya uadilifu na uzalendo miongoni mwa watumishi wa umma imeongezeka, hivyo kusababisha kupungua kwa vitendo vya ubadhirifu, uwizi na ufujaji fedha za umma? 

WAJIBU (taasisi anayoiongoza) inaipongeza serikali kwa kuongeza uwazi zaidi kwenye hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na CAG.

Kwa uelewa wa WAJIBU, taarifa za CAG ni tathmini ya kina ya utendaji wa mifumo ya usimamizi ya ndani, utekelezaji sera na mipango pamoja na namna serikali ilivyokusanya na kutumia fedha za umma kwa kipindi kinachoripotiwa.

Hivyo, ni muhimu kwa maofisa masuuli na watumishi wengine wa serikali kuzichambua kwa kina ripoti za CAG kwa lengo la kuendelea kuboresha utendaji wa serikali kwa vipindi vijavyo.

WAJIBU imekuwa inafanya uchambuzi wa ripoti zinazotolewa na CAG kwa kipindi za miaka saba mfululizo (2015/16 hadi 2021/22). Katika uchambuzi wa ripoti hizo, WAJIBU imebaini mambo makuu saba yafuatayo:

Kwanza; kumekuwa na mwenendo hafifu wa utekelezaji mapendekezo ya CAG. Katika kipindi cha miaka saba cha uchambuzi wa ripoti hizo, utekelezaji wa mapendekezo yake umekuwa chini ya asilimia 50. 

Mara nyingi, ama bungeni au serikalini kumekuwa na kauli au migongano ya kimtazamo baina ya viongozi wa juu wanaohusika katika usimamizi wa utekelezaji mapendekezo ya CAG. Mara kadhaa, ama bungeni au serikalini yamesikika maneno ya kushuku juu ya usahihi wa mapendekezo au hoja zinazoibuliwa na CAG. 

Hali hii tunaamini inasababishwa na kutokuwa na uelewa au kuwapo ukakasi katika utaratibu unaotakiwa kufuatwa katika kuzishughulikia hoja za ukaguzi zinatokana na ripoti za CAG.  

Kwa mujibu wa Kanuni za Ukaguzi wa Umma za Mwaka 2009 (The Public Audit Regulations 2009), Kifungu cha 93 kinamtaka kila ofisa masuuli (accounting officer) kuandaa majibu ya hoja za CAG ndani ya siku 21 baada ya ripoti ya CAG kuwasilishwa bungeni na kuwa wazi kwa umma. Hivyo, kwa mujibu wa kanuni hiyo, maofisa masuuli ndio wenye mamlaka ya kutoa majibu juu ya hoja za ukaguzi na siyo mawaziri au wanasiasa.

Ushauri wangu juu ya hili ni kuwa, “TUSIWE MABINGWA WA KUPINGA HOJA ZA UKAGUZI BALI TUJITAHIDI KUWA MABINGWA WA KUZUIA HOJA ZA UKAGUZI KUJITOKEZA’’. Tukiliweza hilo, shughuli zote za serikali zitakuwa zinafanywa kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo ambapo hoja za ukaguzi zitapungua kwa kiasi kikubwa.

Pili; kumekuwapo uboreshaji mkubwa wa uandishi/utayarishaji hesabu za serikali katika ngazi zote za serikali kwa kuzingatia hati za ukaguzi zinazotolewa na CAG. 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inastahili pongezi za kipekee kwa kuona umuhimu wa uandaaji taarifa za fedha na hesabu za serikali kuzingatia viwango vya uhasibu vya kimataifa kuanzia mwaka 2004, uamuzi ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya uandishi wa hesabu za serikali nchini.

WAJIBU katika uchambuzi wake wa ripoti za CAG, na kupitia ripoti zake za "Hali ya Uwajibikaji wa Kifedha Nchini” (CASFAR) za mwaka 2019/20 na 2020/21, inaonesha maboresho makubwa ya hati za ukaguzi zilizotolewa na CAG. 

Kwa mfano, matokeo ya ukaguzi wa CAG kwa kipindi cha miaka mitatu (2019/20 – 2021/22) yanaonesha maboresho katika uandaaji hesabu kwa Serikali Kuu, mashirika ya umma pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hii imepelekea kuongezeka kwa idadi ya taasisi, Mamlaka za Serikali za Mitaa na mashirika ya umma yaliyopata hati safi. 

Kwa mwaka 2019/20, hati safi kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na serikali kuu zilikuwa asilimia 87, mwaka 2020/21 zilikuwa asilimia 95 na mwaka 2021/22 asilimia 96. 

Tatu; upungufu makubwa katika utendaji wa mfumo mzima wa ukaguzi wa ndani. Katika ripoti zote za CAG zimeonesha utendaji hafifu wa vitengo na mfumo mzima wa ukaguzi wa ndani kutokana na sababu mbalimbali kama kukosekana kwa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi, kutokuwa na ujuzi stahiki, utendaji duni wa kamati za ukaguzi na mfumo duni wa kutoa taarifa (reporting mechanism).

Upungufu wa utendaji wa mfumo mzima wa ukaguzi wa ndani pia unaweza kuonekana kwa kuwapo hoja zinazotokana na uzingatiaji duni wa sheria, taratibu na kanuni za utendaji katika utumishi wa umma.

Nne; ulegevu wa sheria na kanuni za usimamizi wa rasilimali katika kuwachukulia hatua watumishi waliohusika kwenye kuvunja sheria, taratibu na kanuni za utendaji katika utumishi wa umma. 

Kwa kipindi cha miaka minane nilichofanya kazi kama CAG (2006 hadi 2014), nilishuhudia ugumu uliopo wa kuwachukulia hatua watumishi wa umma waliofuja fedha za umma ama kuisababishia hasara serikali. 

Wasiwasi wangu huu umethibitishwa na kauli ya Rais Samia kwenye kauli yake aliyoitoa wakati akipokea ripoti za CAG Machi 2023 aliposema, “Nadhani tumezubaa kwenye 'punitive measures', hatuchukui hatua kwenye adhabu, ingekuwa tunachukua hatua haya yasingeendelea.“  

Hii inatokana na ukweli kwamba sheria zetu hazitoi taratibu bayana za kuchukuliwa hatua kwa watumishi wa aina hiyo na wakati mwingine taratibu zilizowekwa za kushughulikiwa mambo haya kiutawala huwa ni mrefu mno na si rahisi kutekelezeka “not effective”. 

Mfano, itakumbukwa kwenye miaka ya nyuma, Kamati ya Bunge ya Usimamizi wa Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), chini ya uenyekiti wa Agustino Mrema ilikuwa inaagiza maofisa masuuli na watumishi wa umma waliotajwa kuhusika na upotevu wa fedha za umma katika ripoti za CAG wakatwe asilimia fulani ya mishahara yao, ingawaje agizo hilo lilikuwa ni kinyume cha sheria na kanuni za utumishi wa umma. 

Hali hii ilitokana na kukosekana hatua stahiki zinazotosheleza kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa upotevu wa fedha na rasilimali nyingine za umma. Hali hii inaonekana ilikuwa ni tatizo hata kwenye nchi nyingine kama vile Marekani, Uingereza, Afrika ya Kusini na hata majirani zetu Kenya.

Kwenye miaka ya 2006 na kuendelea walilazimika kutunga sheria za kupambana na vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za umma (Fraud Acts) katika jitihada za kuimarisha utaratibu wa kisheria wa kushughulikia vitendo vya uwizi, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Tano; kumekuwa na wimbi kubwa la vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma. Baada ya kuchambua ripoti za CAG, Taasisi ya WAJIBU imekuwa inafanya tathmini ya miamala ambayo ina viashiria vya vitendo vya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu. Ingawa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, miamala hiyo imekuwa inapungua, bado jumla yake ni kiasi kikubwa cha fedha. 

Mathalani kwa mwaka 2021/22, ripoti za CAG zilizotolewa mwezi Machi 2023, zinaonesha jumla ya miamala ya Sh. trilioni 3.05 (Sh. trilioni 4.59 mwaka 2020/21) ina viashiria vya rushwa, udanyanyifu na ubadhirifu ambayo ni sawa na asilimia tisa (9) na 13 ya matumizi yote ya serikali, mtawalia. 

Vitendo hivi vya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu vinaendelea kuwapo kutokana na udhaifu wa utendaji kazi wa taasisi za uchunguzi na mashtaka kushindwa kuchunguza kwa wakati matukio ya rushwa, kupata ushahidi stahiki na kushtaki kwa wakati watuhumiwa wote wa vitendo hivi. 

Vilevile, kumekuwapo na tatizo kubwa la kupungua kwa uzalendo, uadilifu na kumekuwapo na tabia ya kutotii sheria, kanuni na miongozo inayotolewa kwa ajili ya kuendesha shughuli za serikali. 

Sita; katika ripoti zote za CAG za miaka saba iliyopita, imeripotiwa kuwa mashirika ya umma na taasisi za serikali zimekuwa na matatizo makubwa ya utegemezi kwa serikali, kushindwa kujiendesha, kutofikia malengo ya kuanzishwa kwake pamoja na kujiendesha kwa hasara. 

Katika uchambuzi wake, WAJIBU imebaini sababu mbalimbali zinazopelekea changamoto hizo, kubwa zikiwa ni; udhaifu katika uongozi wa taasisi na mashirika hayo, kuwapo mikataba na taratibu za kiutendaji zinazozuia ufanisi kati ya serikali na taasisi au mashirika hayo, uhaba wa mitaji na kuingiliwa kiuendeshaji na kiutendaji wa mashirika na taasisi hizi za umma na mamlaka mbalimbali za serikali na vyama vya siasa.

Saba; kumekuwa na uboreshwaji mkubwa wa usimamizi wa rasilimali za umma hasa kutokana na utekelezwaji wa Mpango Mkakati wa Kuboresha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP – programs) pamoja na uimarishaji mifumo ya kielektroniki (MUSE) uliofanyika hasa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

*Mwandishi wa makala hii ni CAG mstaafu, pia alishakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na Mhadhiri wa Uhasibu Chuo Kikuu cha Mzumbe.

FUATILIA KESHO USHAURI WAKE KWA SERIKALI..