Viongozi wazembe waonywa kukwamisha usawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:44 PM Mar 28 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi.
PICHA: MWANDISHI WETU
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi.

WANAWAKE wasiowajibika katika nafasi mbalimbali walizonazo wameonywa kuwa chanzo cha kukwamisha lengo la kufikia usawa wa kijinsia katika uongozi.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, Lilian Liundi, alitoa onyo hilo wakati wa mafunzo kwa wanawake vijana yenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi na maamuzi.

Lilian alisema ni lazima kwa wanawake kuonyesha utofauti wa uongozi kati yao na wanaume ili kuongeza idadi ya viongozi wanawake nchini.

"Usitarajie kuwa wa kawaida halafu uzalishe kitu cha tofauti, hutaweza yaani kama wewe ni wa kawaida utazalisha kitu cha kawaida, lakini kama una utofauti utazalisha kitu cha tofauti" alisema.

"Kitu cha kwanza cha kufikiria ni jinsi gani kama mwanamke unajitofautisha na wengine usiende kwenye shirika fulani ukafanya 'business as usual' (kufanya jambo kwa mazoea) wewe fikiria unafanyeje iwe 'business un usual' ili uonekane tofauti".

Mafunzo hayo ya siku tatu yalishirikisha washiriki 97 wengi wao wakiwa ni viongozi wanawake katika serikali za wanafunzi katika vyuo vikuu 11 ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu Mzumbe.

Pamoja na mambo mengine, Lilian alisema kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mabunge la Dunia (IPU) zinaonesha kuwa kuna wanawake 21 wakuu wa nchi na wakuu wa Serikali, huku kwa upande wa Afrika pakiwapo na wanawake watano waliowahi na waliopo katika nafasi ya urais.

"Tumeshawahi kuwa na marais watano tu Afrika ambao ni wanawake aliyekuwa Rais wa Malawi, Joyce Banda (Aprili 2012 -Mei 2014), aliyekuwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf (Januari 2006- Januari 2018) aliyekuwa Rais wa Mauritius, Ameenah Gurib Fakim (Juni 2015 -Machi 2018" 

Wengine ambao bado wapo madarakani mpaka sasa ni Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde na Rais Samia Suluhu, huku idadi ya wanawake waliowahi kushika nafasi ya Spika wa Bunge ikiwa ni asilimia 20.9.

Hivyo aliwataka wanawake wenye nia ya kuongoza kujitokeza ili wapewe msaada wa kile kinachohitajika badala ya kujificha na kukaa kimya na vipaji vyao vya uongozi.

Akitoa takwimu za idadi ya wabunge wanawake nchini alisema katika wabunge wa kuchaguliwa wanawake ni 26 tu kati ya wabunge wa kuchaguliwa 264, huku wa viti maalum wakiwa ni 113 na kwamba jumla ya wabunge wanawake ni 141.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (MUHAS), Vanessa Lutabana akieleza uzoefu wake na magumu aliyopitia kuipata nafasi hiyo alisema bado jamii inamtazamo hasi kuhusu viongozi wanawake, huku akisema wanawake wenyewe wanahofia kukutana na ugumu huo na hivyo kuipongeza TGNP kwa kuandaa semina kama hiyo.