Watu saba wafariki, 15 wajeruhiwa ajalini Iramba

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 06:45 PM Apr 10 2024
Basi la Kampuni ya Lujiga Express lililopata ajali baada ya kugonga Lori kwa nyuma na kusababisha vifo vya watu Saba.

WATU saba wamefariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 15 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Kampuni ya Lujiga Express walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, kugonga lori la mizigo kwa nyuma ambalo lilikuwa limeegeshwa barabarani kutokana na kuharibika.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda, akizungumza kwa simu na Nipashe Digital leo Jumatano 10, 2024; amesema ajali hiyo imetokea leo saa 10:30 alfajiri katika Kijiji cha Malendi kilichopo Kata ya Mgongo, wilayani humo.

Amesema ajali hiyo imehusisha basi la kampuni ya Lujiga Express (hata hivyo hakutaja namba za gari hiyo), ambalo ilikuwa ikitokea mkoani Dar es Salaam kwenda Mwanza.

Amesema kati ya waliofariki wanaume ni sita na mwanamke ni mmoja na kwamba miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora.

DC Suleiman amesema majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika hospitali mbili, baadhi wakiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba (Kiomboi) na wengine katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga ambako wanaendelea na matibabu. 

Mkuu wa Wilaya amesema basi hilo lilipofika katika Kijiji cha Malendi, kulikuwa na lori la mizigo ambalo lilikuwa limeegeshwa pembeni ya barabara ambalo pia lilikuwa limetoka Dar es Salaam likielekea Mwanza, hivyo basi liligonga lori hilo na kusababisha vifo na majeruhi hao.