GHF kufichua yaliyofichika darasani ni kupitia vipaji

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 12:18 PM Apr 23 2024
Wanafunzi wa Kibiti wakisherehekea ushindi baada ya kupata cheki ya dhahabu.
Picha: GHF
Wanafunzi wa Kibiti wakisherehekea ushindi baada ya kupata cheki ya dhahabu.

VIJANA kukosa ajira ni janga pasua kichwa likigusa karibu mataifa yote, lakini tatizo ni kubwa zaidi katika mataifa maskini ikiwamo Tanzania.

Taasisi ya Great Hope Foundation (GHF) ya Dar es Salaam, imeliona hilo na kujitosa kulikabili, ikianzisha tuzo za Uwezo Award, kuhamasisha utambuzi wa vipaji na uwezo wa wanafunzi shuleni.

Mratibu wa tuzo hizo, Noelle Mahuvi, anazungumza na Nipashe, jijini Dar es Salaam, akieleza nia ya kuwafikirisha vijana wadogo waliopo shuleni ili watambue uwezo wa ziada, wajue namna wanavyoweza kuishi na kufikia malengo na ndoto zao wanapomaliza masomo.

Ikumbukwe wanaolia kukosa ajira ni makundi yote, wasomi  na wasiosoma  kutokana na sababu mbalimbali. Ila kwa wenye elimu kuna kitu wanakimudu nje ya taaluma yao ila inaonekana hawakukitambua mapema, anasema Noelle.

Kimbilio la wengi hivi sasa ni shughuli za kujiajiri, hata hivyo kwa Tanzania wanafunzi bado wanaendelea kusoma elimu iliyo vitabuni inayodaiwa kwa kiwango kikubwa haiwapi stadi za kujiajiri.

Kutokana na kutambua uwezo wa watoto nje ya masomo ya darasani, Noelle anasema maono ya GHF ni kujenga kizazi kipya kilichowezeshwa, kilichoendelezwa na chenye kuwajibika kinachoweza kuleta mabadiliko kupitia vipaji na ubunifu.

Anataka kuwa na kizazi chenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na kuondoka na kile kinachojaa unyonge kutokana na kutojua hatma yake.

 â€śTunaamini vijana wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii endapo, watawekewa majukwaa   yatakayowasaidia kuelewa na kutumia uwezo wao kikamilifu,” anasema Noelle.

Anasema GHF itaendelea kutekeleza programu za kibunifu, ambazo zinawasaidia vijana kupata ujuzi unaofaa ambao unaweza kuwasaidia kustawi katika soko la ajira kupitia kujiajiri au kuajirika kwa urahisi.

UJIO UWEZO AWARD

Noelle anasema Uwezo Programu ilianzishwa mwaka 2016 kwa  lengo la kuwasaidia wanafunzi wa shule za sekondari kujifunza na kuonesha uwezo wao ambao hauonekani kwa urahisi wakiwa darasani.

Anafafanua kuwa  programu hiyo imejikita  kuwapa wanafunzi jukwaa la kujifunza ujuzi wa kijasiriamali  wa karne ya 21, ukihusisha ubunifu, kujiamini, uongozi na  kutatua changamoto na kukabiliana na changamoto za soko la ajira, kujiajiri au  kuajirika kwa urahisi.

Noelle anasema wanafunzi wanufaika wa programu hiyo wamekuwa wakifanya vizuri katika maeneo mbalimbali baada ya kumaliza shule.

Anasema baadhi yao wamefanikiwa kufungua asasi za kijamii, na wengine wanafanya biashara zinazowaingizia kipato kikubwa na kumudu maisha yao na familia zao.

 Kwa mujibu wa Noelle programu ya uwezo ilianza ikiwa na mradi mmoja wa Uwezo Award mwaka 2016 ukizifikia shule 20 na mpaka sasa programu ina miradi minne na shule 250 zinanufaika kwa mwaka. Anaitaja miradi hiyo kuwa ni Uwezo Award, Uwezo Bonanza, Uwezo Kinara na Uwezo Klabu.

Kupitia Uwezo Award, wanafunzi hujifunza kwa kutatua changamoto zilizopo kwenye mazingira yao wakitakiwa kubuni na kutekeleza miradi ya kijasiriamali ambayo itatatua changamoto hizo.

Hutakiwa kuwa na vigezo vikuu vitatu, kwanza mradi wanaoutekeleza uwape fursa ya kutambua na kutumia vipaji vyao iwe kuimba, kuchora, kucheza, pili uwape fursa ya kujifunza ujuzi mpya  kuuza, ufundi na tatu mradi huo ulete matokeo chanya kwenye jamii, anasema.

Miradi bora hutambuliwa kwa kupewa tuzo na shirika kila mwaka, kwamba tangu mwaka 2016 mpango huo umewafikia wanafunzi takribani 1,200 walioko kwenye  shule zaidi ya 5,000 na za mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro, anasema.

Mratibu wa tuzo anasema mwaka 2023 sekondari tatu bora za juu za mkoani Pwani zilizoshindania tuzo za dhahabu,  nazo ni Kibiti mshindi wake akipata tuzo ya dhahabu na Sh. 1000,000.

Nyingine ni Sekondari ya  Kibaha  washindi wawili  walipata  Sh. 500,000 wakati  Victory  washindi watatu  walipata tuzo ya  Sh.300,000.

WANUFAIKA WAELEZA

Sarah Petro, mhitimu katika  Sekondari ya Kurasini mwaka 2019 ambaye kwa sasa ni mjasiriamali anayetengeneza keki, karanga, ubuyu na pipi anasema ujuzi wa kutengeneza bidhaa hizo aliupata akiwa shuleni kupitia Uwezo Award.

Anasema akiwa mwanafunzi alishiriki mashindano yaliyoandaliwa na GHF kupitia Uwezo Award na kwamba kwa kushirikiana na wanafunzi wenzake walilima mboga, walitengeneza karanga, ubuyu na pipi

“Fedha tulizozipata tulizitumia kwa kutembelea watoto yatima. Lakini kwa sasa ni mjasirimali ujuzi niliupata ujuzi nikiwa shuleni, ile miradi iliniwezesha nisiwe muoga, niwe kjasiri na siogopi nikikosea,” anasema Sarah.

Omary Baajun, mhitimu wa Shule ya Sekondari Mugabe mwaka 2016 kwa sasa ni mjasiriamali wa kuzalisha vitabu na vipeperushi anasema akiwa shuleni alishiriki mradi wa Uwezo Award akishirikiana na wenzake kwa kutengeneza mazuria ya vitambaa.

“Tulikuwa tunaokota vitambaa kwa mafundi cherehani  mitaani, tulitengeneza mazuria na kuwauzia walimu. Pia tulianzisha shamba na kulima bamia, mboga na kunde.  Kusema ukweli hivi sasa nalima pia nimejiajiri,” anasema Baajun.

Boaz Peter, mwanafunzi wa Tambaza Sekondari ya Dar es Salaam anasema ameshiriki tuzo za Uwezo Award mwaka jana kipengele cha mwimbaji bora wa kiume na kushika nafasi ya kwanza. Anasema mashindano hayo yaishirikisha shule zaidi ya 20 za  Dar es Salaam.

“Hii Programu ya Uwezo Award kupitia Tuzo za Uwezo Award zimenisaidia .Zimeniwezesha kusafiri kimataifa kwenda Rwanda na kushiriki matamasha mbalimbali. Pia zimeniwezesha kuimba katika matamasha ya Benki ya NMB na NBC, maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere niliweza kuimba. Pia Julai mwaka huu ninatajia Kwenda Liberia kuhudhuria mkutano wa Pan-Africanism” anasema Boaz.

Nancy Fausten kutoka Sekondari Zanaki mwaka 2020, kwa sasa ni mwasisi na mkurugenzi wa taasisi iitwayo binti hodari anasema akiwa shuleni alishiriki mradi wa kukarabati vyoo vya shule pamoja na mgahawa kupitia Programu ya Uwezo Award.

“Nilishiriki mara mbili, kwanza nikiwa kidato cha tano na pili nikiwa kidato cha sita. Tulishika nafasi ya pili kimkoa. Tulitengeneza shanga za mkononi na kuuza mtaani.Tuliandaa shughuli ya vipaji suleni. Pesa tulizozipata tulizitumia kukarabati vyoo na mgahawa wa shule,” anasema Nancy.

Anasema kikundi chao kilishika nafasi ya kwanza katika Tuzo za Uwezo Award mkoa wa Dar es Salaam ikishirikisha zaidi ya shule 100. Anasema walipewa zawadi ya Sh. 500,000 pamoja na kutembelea mbuga ya wanyama.

 Nancy anasema akiwa shuleni walianzisha kikundi walichokiita vikio ambacho kilikuwa kinafanya miradi ya kusaidia jamii ikiwemo kuwatembelea wenye mahitaji.

Anabainisha kuwa kupitia Program ya Uwezo amepata faida nyingi kimaisha mojawapo ni ujuzi wa kuwa kiongozi ambapo kwa sasa ameanzisha taasisi na kuwaongoza watumishi zaidi ya 10.

Anasema pia imemjengea uwezo wa kutatua matatizo na moyo wa kujitolea.