Jukwaa la viongozi Tanzania lachangia Mil 13.7 waathirika Hanang

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:05 PM May 09 2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dk. Jim Yinazi (kushoto) akikabidhiwa hundi ya msaada wa Sh. Milioni 13.7 na Mratibu Mkuu wa Kundi la Viongozi Tanzania Benjamin Thompson kwa ajili ya waathirika wa maaafa ya Hanang.
Picha: Mpigapicha Wet
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dk. Jim Yinazi (kushoto) akikabidhiwa hundi ya msaada wa Sh. Milioni 13.7 na Mratibu Mkuu wa Kundi la Viongozi Tanzania Benjamin Thompson kwa ajili ya waathirika wa maaafa ya Hanang.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonazi amepokea msaada wa Sh. Milioni 13.7 kutoka kwa wanachama wa kundi la viongozi Tanzania, kwa lengo la kwenda kuwasaidia waathirika wa maafa Hanang.

Akipokea msaada huo leo jijini Dodoma Dk. Yonazi amewashukuru wanachama wa kundi hilo kwa kujitoa kwao kwenda kwa waathirika wa maporomoko ya tope, mawe na magogo wilayani Hanang mkoani Manyara yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2023.

Dk. Yonazi amesema msaada huo, pamoja na misaada ya wasamaria wengine inaunga mkono jitihada za serikali zinazoendelelea katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika hao ikiwemo kujengea nyumba 108, ili wanaendelee kujitafutia riziki na kujiletea maendeleo.

“Tunawashukuru wenzetu wa kundi la Viongozi Tanzania kwa uzalendo waliouonyesha kwa ajili ya mchango huu mkubwa walioutoa, niwaombe Watanzania wenzangu tuzidi kushikana mkono hasa nyakati hizi ambako sehemu nyingi nchini kumetokea majanga mbalimbali, jambo jema kuendelea kushirikiana kuwasaidia ndugu zetu," amesema Dk. Yonazi

Miongoni mwa wajumbe wa kundi hilo Benjamin Thompson, na Mhandisi Archard Kato, wamesema kundi hilo linaundwa na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi za umma, sekta binafsi, wahadhiri vyuo vikuu, vyama vya siasa na wana diaspora.

Thompson amesema michango hiyo ilikusanywa kutoka kwa wanachama 145 kati ya 600 walioko kwenye kundi hilo, ambao ndio waliweza kuchangia kwa wakati huo.

“Mkusanyaji wetu alikuwa ni Zamaradi Kawawa,ambaye alifanya kazi nzuri sana na kwa uaminifu mkubwa. Baada ya kumaliza kazi hiyo, tulikubaliana kwamba aweke pesa hizo kwenye akaunti ya maafa,” amesema.

Naye, Mhandisi Kato amesema wanachama wa kundi hilo wameguswa na janga hilo la Hanang na hivyo kuona umuhimu wa kutoa michango hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na majanga kama hayo.

“Tunaahidi kwamba tutaendelea kuisaidia serikali kwa kidogo tulicho nacho katika kukabiliana na athari za majanga kama haya, na tungependa kuona hili jambo linaenea kwa watanzania wengi, yaani hata kabla ofisi yako haijafika au serikali angalau watanzania wenyewe wawe wanafanya jambo la mwanzo kwa uzalendo wao katika kukabiliana na mambo ya dharula,” amesema Kato.

Maafa ya Hanang yalitokea Desemba 3, mwaka huu, Manyara na kusababisha vifo ya watu zaidi ya 80, huku mamia wengine wakiachwa bila makazi, pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu.