Rais Samia mgeni rasmi maadhimisho miaka 85 ya kanisa la TAG

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 05:53 PM May 09 2024
news
Picha: Pili Kigome
Mchungaji Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dk. Barnabas Mtokambali (katikati) akizungumza na wanahabari hawapo pichani.

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya miaka 85 ya Kanisa la Assemblies of God (TAG).

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mchungaji Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dk. Barnabas Mtokambali amesema, maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Julai 14 mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Askofu Mtokambaliw amesema katika maadhimisho hayo wamejikita katika maeneo makuu matatu muhimu ya kumshukuru Mungu ikiwemo Agizo Kuu, Kuzaa na kulea viongozi na Miradi na Maendeleo.

Akifafanua kuhusu Agizo Kuu amefafanua kuwa, katika miaka hiyo 85 TAG imejitahidi kutekeleza  agizo la Mungu kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kuwezesha kuwa na wamishionari toka Tanzania wanaotumika nchini na nje ya nchi ambazo ni Madagascar, Msumbiji, Malawi, Zambia, Congo, DRC, Burundi, Uganda, Kenya na Rwanda.

Kuwa na ongezeko la wachungaji na watumishi wa Injili ambao wametumika kwa bidii katika kuhubiri na kufundisha neno la Mungu kote nchini, kuenea kwa makanisa nchini kote pamoja kuleta mabadiliko ya kiroho katika maisha ya watu.

Katika Kuzaa na Kulea Viongozi amesema TAG limethamini sana kazi ya kuzaa na kulea viongozi wa kiroho na kuleta mafanikio makubwa kupitia program za mafunzo na uongozi ambazo zimewawezesha waumini kujitokeza na kujitoa katika kazi ya ufalme wa Mungu.

Pia wamefanikiwa kujenga vyuo tisa(9) vya Theolojia na Uongozi vyenye matawi 71 nchi nzima na maadhimisho hayo yanawapa tafakuri juu ya mchango wa viongozi kuweka mikakati endelevu ya kuendeleza kizazi kijacho cha viongozi.3

Askofu Mtokambali amefafanua dhima Kuu ya Maadhimisho hayo ni kumshukuru Mungu kwa uaminifu wake kuwezesha kubaki imara kama Kanisa na taasisi kwa miaka yote hiyo bila ya kutetereka.

Pia yanalenga kurithisha kwa kizazi kijacho kupokea kijiti cha kumwishi Mungu katika zama zijazo ili Mungu aendelee kutenda makuu.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya Tanzania ya awamu zote kutupa uhuru wa kuabudu, kutupatia misahamaha ya kodi kwa ajili ya vifaa vyetu vya kanisa kila mara”alisema

Amesema kupitia maadhimisho wanataka kuweka historia mpya kuthibitisha dhamira ya kuendelea kuwa chanzo cha  matumaini, amani, upendo na mabadiliko chanya katika jamii.

Amesema kuelekea kilele hicho TAG wamedhamiria kuwafikia vijana zaidi ya elfu kumi(10,000) wenye umri wa chini ya miaka 34 kutoka nchini katika kutoa elimu kukabliana na majanga ya mmomonyoko wa maadili kuwapa mafunzo na elimu ikiwemo ya kiroho na kuwajenga kuwa viongozi bora wa baadae.

Aidha wamelenga kuwafikia watoto wa kike(wasichana) takribani elfu sita (6000) wa shule za msingi kugawa taulo za kike, kushiriki katika shughuli za kijami ikiwemo na uchimbaji wa visima vya maji safi katika shule za msingi na Sekondari za jijini Dar es Salaam katika jitihada za kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kumtua mama ndoo kichwani.

“Katika kilele hicho tutakuwa na mkutano mkubwa wa injili na viongozi mbalimbali wa kiroho na serikali waliokuwa kupitia kanisa letu watashiriki, tayari Spika wa Bunge Tulia Akson na Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko wamethibitisha kushiriki na viongozi wengine wengi” amefafanua