Udhibiti wa EWURA bei za nishati, maji ulivyoleta nafuu kwa watumiaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:36 AM Mar 28 2024
Rais Samia Suluhu Hassani, akikata utepe kuzindua Ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, ambayo huandaliwa na EWURA.
Picha: EWURA
Rais Samia Suluhu Hassani, akikata utepe kuzindua Ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, ambayo huandaliwa na EWURA.

MAFANIKIO ya kiuchumi ni mchakato wa mabadiliko kutoka chini kwenda juu ambao unatokana na ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi ikiwamo kutumia fursa za kiuchumi zilizopo kwa wakati husika.

Maendeleo ya kiuchumi katika nchi huletwa na mambo mengi lakini kubwa zaidi ni watu kufanya kazi kwa bidii pamoja na taasisi za kimaendeleo, zikiwemo za serikali na za binafsi, kuwawezesha wananchi kutambua na kuzitumia vizuri fursa zilizoko katika maeneo yao.  

Moja ya taasisi za serikali ambazo zinachangia katika kuleta maendeleo ni mamlaka za usimamizi kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambazo zimepewa jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote za kiuchumi na kijamii. Lengo ni kuhakikisha huduma hizo zinawafikia moja kwa moja wananchi. 

Mamlaka hizi zinahusika moja kwa moja na kusimamia na kuratibu shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwamo kudhibiti wa kiufundi na kiuchumi. Udhibiti  wa kifundi ni pamoja na unadhifu wa miundombinu na ubora wa huduma kupitia utoaji wa leseni na  udhibiti wa kiuchumi ni pamoja na kulinda mitaji ya watoa huduma na maslahi ya watumiaji huduma ikiwamo upangaji wa bei za huduma.

 EWURA ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ya mwaka 2001 (Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania) pamoja na majukumu mengine, kupewa majukumu chini ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 (Sura ya 392) kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na wa chini wa petroli (mafuta na gesi asilia) Tanzania Bara.

 Kazi kubwa ya mamlaka hiyo ni kutoa leseni za uendeshaji wa shughuli za nishati na maji nchini, mapitio ya gharama za uendeshaji wa huduma, kufuatilia utekelezaji wa viwango vya ubora, usalama, afya na mazingira. Pia ina wajibu wa kukuza na kuendeleza ushindani wenye tija kiuchumi, kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma pamoja na kuendeleza upatikanaji wa huduma zilizowekwa kwa watumiaji wote wa kipato cha chini, watumiaji wa vijijini na wasiostahili katika sekta zilizosimamiwa.

 EWURA pia inadhibiti shughuli za gesi asilia zinazojumuisha usafirishaji, uhifadhi na usambazaji. Miundombinu ya gesi asilia kama mitambo ya kusindika gesi, mabomba ya upitishaji na usambazaji pia vinadhibitiwa na mamlaka ili kuhakikisha kunakuwa na ubora wa huduma huku utunzaji wa mazingira ukipewa kipaumbele cha hali ya juu.

 Mamlaka inajitahidi kuboresha ustawi wa jamii ya Tanzania kwa kukuza ushindani mzuri na ufanisi wa uchumi, kulinda maslahi ya watumiaji, kulinda uwezo wa kifedha wa watoa huduma ili kusambaza bidhaa kwa ufanisi.

 Pia ina jukumu la kukuza upatikanaji wa huduma zilizodhibitiwa kwa watumiaji wote pamoja na wenye vipato vya chini, watumiaji wa vijijini na wanyonge, kuzingatia umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira, kuongeza uelewa kwa umma juu ya huduma zinazodhibitiwa. 

 ILIVYOKUWA KABLA 

Kabla ya kuanzishwa mwaka 2006, taasisi kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira na kampuni zinazofanya  biashara ya mafuta, zilikuwa zikipanga bei ama kwa utashi wa wafanyabiashara au menejimenti ya taasisi husika.

 Kutokana na kukosekana kwa udhibiti, bei za huduma kwa rejareja kama mafuta, zilipanda holela, hivyo kuwaumiza watumiaji huku wafanyabiashara wakitumia mwanya huo kuwakandamiza wateja. 

 Kwa mfano, baada ya kuona kuwa bei za mafuta zinapanda holela pengine hata mara tatu kwa siku, Januari 2009, EWURA iliingilia kati kwa kuanza kutoa bei kikomo.  Dar es Salaam bei zilishuka kutoka Sh. 2,000 hadi Sh. 1,233 kwa lita ikiwa ni punguzo la asilimia 62. Kwa mikoa ya mbali kama Kigoma, bei ilishuka kutoka takribani Sh.  2,400 hadi Sh. 1,642 kwa lita ikiwa punguzo la asilimia 52. 

 Kuanzishwa kwa EWURA kuliwezesha taasisi zote kuheshimu sheria, kanuni na taratibu na kufuata hatua mbalimbali ikiwamo kushirikisha wadau, hususan watumiaji wa bidhaa husika kama vile umeme na maji.

 Kwa sasa, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, TANESCO au kampuni binafsi ya kuzalisha umeme, kama  inataka kurekebisha bei ni lazima ipitie hatua mbalimbali ikiwamo kuwasilisha maombi EWURA, kufanya mikutano na wadau ili kuwashirikisha kuhusu nia ya kurekebisha gharama ya huduma na wadau kutoa maoni yao kama ni kupinga au kukubali.

Taasisi husika pia ni lazima ieleze sababu za kusudio la kurekebisha bei. Katika kufuata hatua hizo, TANESCO imeshuhudiwa ikianzisha mchakato wa kutaka kupandisha bei za umeme kwa wateja wake. Shirika hilo lilifuata taratibu zote ikiwamo kufanya mikutano na wadau kupitia Baraza ya Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA-CCC).

 Mikutano hiyo iliyofanyika maeneo mbalimbali nchini, ilitoa fursa kwa watumiaji wa huduma hiyo kupinga nia ya kupandisha bei ya umeme. Kwa mantiki hiyo, taasisi inapotaka kupandisha bei ni lazima ihusishe wadau ili nao watoe maoni kabla ya hatua zaidi kufuata ili kutimiza lengo lililokusudiwa.

 Hata bei za mafuta, kutokana na udhibiti makini wa EWURA, zimekuwa zikitangazwa kila mwezi huku zikionyesha wakati mwingine kushuka kulingana na sababu mbalimbali kama vile bei katika soko la dunia kushuka. Kuwepo kwa EWURA pamoja na mabadiliko ya bei za mafuta kumepunguza maumivu kwa watumiaji wa mafuta kwa asilimia 30 ikilinganishwa kama EWURA isingekuwepo.

 Kuwapo kwa udhibiti huo, kumesaidia kuwapunguzia mzigo wananchi wanaotumia mafuta kwa shughuli mbalimbali na kuwabana wafanyabiashara waliokuwa wakifanya njama za kupanga bei kwa utashi wao, hivyo kuwaumiza watumiaji wa mafuta.

 Pia kuwapo kwa EWURA kumewafanya wafanyabiashara waliokuwa wakigoma kuuza mafuta wakisubiri mafuta yaadimike ndipo wapandishe bei, kutofanya hivyo na wale waliokiofanya hivyo walikumbwa na fagio zito la chuma kwa kupewa adhabu kali. 

 EWURA ina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo hapa nchini kwa mfano, kwa utoaji wa bei kikomo kwenye mafuta, Watanzania wanapata nafuu kwa bidhaa ukilinganisha na kabla ya uwepo wa EWURA. Kwa hiyo fedha iliyobaki inatumika kwenye matumizi mengine ya kimaendeleo. 

 FAIDA VINASABA 

Uanzishaji wa kuweka vinasaba kwenye mafuta umeifanya serikali kupata faida kubwa.  Utafiti  wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam ulionyesha kuwa kati ya mwaka 2010 na 2013 ulibaini ongezeko la mapato ya serikali (kodi) kwa Sh. bilioni 468.50 ikiwa ni Sh. bilioni 146.5 (2010/11), Sh. bilioni 129.8 (2011/12) na Sh. bilioni 192.2 mwaka 2012/13. 

 Katika mapambano dhidi ya soko holela la mafuta, udhibti wa ubora wa mafuta ya petroli na gesi asilia, EWURA imeendelea kudhibiti wa uuzwaji holela wa bidhaa za mafuta aina ya petroli, kwa wanaofanya biashara hiyo kinyume cha sheria.

 Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, anasema EWURA haitavumilia wanaofanya biashara ya mafuta katika vituo bubu na maeneo mengine yasiyoruhusiwa.

 “Kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na adhabu yake ni kulipa faini kiasi kisichozidi Sh. milioni tano au kifungo cha miaka mitatu jela,” anasema. 

 EWURA pia imepania kuendelea kudhibiti mkondo wa chini wa sekta ya petroli kwa kuhakikisha inaondoa mianya yote ya wizi, watumiaji wa bidhaa hizo wapate huduma iliyobora, kulinda afya pamoja na mazingira kwa maendeleo. 

 Katika mwendelezo wa jitihada hizi za kupambana na soko holela la mafuta, EWURA imeviadhibu vingi vya mafuta kwa kufanya biashara bila leseni ya EWURA, kujengwa bila vibali na kutokidhi viwango vya ubora vya utoaji huduma ya mafuta.

 “Usione vituo vya mafuta siku hizi vinapendeza sana hata ukitoka eneo la kituo hujulikani tofauti na huko nyuma ambapo ungekuwa unanuka mafuta. Ubora huu umetokana na usimamizi mzuri wa EWURA”, anasema Dk. Andilile.

EWURA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya mafuta kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya ubora, kulinda afya na kuzingatia usalama wa afya na mazingira ya Watanzania kwa kuchukua hatua vituo vinavyokwenda kinyume cha taratibu.

 Uuzaji wa mafuta yasiyo na vinasaba ni mwanya wa ukwepaji kodi na ni uhujumu uchumi wa nchi, hivyo EWURA imekuwa ikisimamia suala hili kwa umakini mkubwa. Udhibiti wa ubora wa mafuta ya petroli.

 Moja ya majukumu ya msingi ya EWURA ni kuhakikisha wafanyabiashara ya mafuta wanafuata sheria, kanuni na kukidhi viwango vya ubora katika utoaji huduma za mafuta nchini.

 Sheria ya EWURA na Sheria ya Petroli zinaipa EWURA mamlaka ya kudhibiti masuala ya kiufundi, kiuchumi na kiusalama katika sekta ya petroli.

EWURA husimamia wauzaji wa jumla na rejereja wa mafuta ili kuhakikisha wanatoa huduma yenye ubora na viwango vinavyostahili na kwa gharama ambayo watumia huduma hiyo wanaimudu.

 Mamlaka pia ina jukumu la kuhakikisha kuwa mafuta yanayotumika nchini yanakidhi viwango vya ubora kama vilivyoanishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kabla mafuta haliyopokewa kutoka nje ya nchi hayajaingia katika matumizi. Wafanyabishara ya mafuta nao wana wajibu wa kuhakikisha kuwa bidhaa zao wakati wote zinazingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.

 Hilo hufanyika kwa kufanya ukaguzi kujiridhisha kuwa taratibu za kisheria na kanuni za uendeshaji biashara zinafuatwa kikamilifu. Mamlaka huchukua sampuli za mafuta ili kujiridhisha endapo bidhaa za mafuta zilizo sokoni zinakidhi viwango vya ubora na ni salama kwa matumizi.

 Pia hufanyika kwa kupima wingi wa vinasaba katika mafuta ya soko la ndani ili kujiridhisha kuwa hakuna uchakachuaji, udanganyifu au ukwepaji wa kodi za Serikali. Unapobainika ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za kiufundi na kiusalama katika uendeshaji wa biashara ya mafuta, EWURA huchukua hatua kali dhidi ya mhusika.

 Hatua hizo zinaweza kuwa faini, kifungo au vyote. EWURA hufanya ufuatiliaji kwa umakini wa hali ya juu wa uendeshaji wa biashara ya mafuta nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma inayotolewa inamlinda mtumia huduma dhidi ya madhara ya kiafya, kiusalama na kimazingira.

Ubunifu wa vituo vya Mafuta kuhudumia vijijini Ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za mafuta kwa Watanzania walioko maeneo ya vijijini, EWURA imerekebisha masharti ya leseni kwa wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza vijijini. hadi sasa, zaidi ya vituo 400 vinapatikana vijijini ili kuondokana na uuzaji wa mafuta ya petroli katika mazingira hatarishi yasiyozingatia vigezo na ubora.

 Nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika hivyo, EWURA imrekebisha kanuni za ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini ili kupunguza uuzaji holela wa mafuta kutokana na kushamiri kwa usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda.