Simba yaivaa Azam fainali ya Muungano bila Chama

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:30 AM Apr 27 2024
news
Picha: Maktaba
Clatous Chama

FAINALI ya Kombe la Muungano inatarajiwa kuchezwa kwa mara ya kwanza leo baada ya miaka 20 kupita, wakati Simba itakapokwaana na Azam FC kwenye Uwanja wa New Amani Complex, mjini Zanzibar.

Simba iliingia fainali kwa kuichapa KVZ mabao 2-0, huku Azam, ikiishindilia KMKM mabao 5-2, mechi zilizochewa kwenye uwanja huo huo.

Itakuwa ni nafasi nzuri ya timu zote kutwaa taji hilo, ambapo kama Simba ikishinda itakuwa imejiwekea kibindoni taji la pili msimu huu, baada ya kutwaa Ngao ya Jamii, Agosti 13 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ilipowafunga watani zao wa jadi, Yanga kwa mikwaju ya penalti 3-1 na litakuwa taji la kwanza kwa Azam msimu huu.

Katika fainali ya leo, Simba itakuwa na pigo la kumkosa mmoja wa wachezaji wake tegemeo kwa ufungaji na utoaji wa pasi za mwisho, 'asisti', Clatous Chama, aliyeumia katika mechi iliyopita dhidi ya KVZ.

Mbali na mchezaji huyo, pia itawakosa Henock Inonga, aliyeumia katika mechi ya dabi, kati ya timu hiyo dhidi ya Yanga, iliyochezwa, Aprili 20, na Saido Ntibazonkiza.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola, amesema mechi haitokuwa nyepesi, si kutokana na ubora wa Azam tu, bali huwa wakikutana mchezo huwa mgumu.

"Haiwezi kuwa fainali nyepesi, ni ngumu na nzuri kwa sababu zinakutana timu zenye uwezo, ziko vizuri, ukiangalia Azam ina kiwango kikubwa msimu huu.

Katika mechi hii sisi tumejipanga, pamoja na ubora na uzuri wao, tumejiandaa kupambana kupata ushindi katika mechi ya fainali, tutaingia kwa tahadhari na heshima kubwa kwa Azam kwa sababu tukikutana shughuli huwa pevu, ila tunawaahidi mashabiki wetu matokeo mazuri," alisema Matola.

Matola pia aliwataja wachezaji ambao wataukosa mchezo wa leo, lakini akawatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa waliobaki wako fiti na wameahidi kuipigania nembo ya Simba.

"Tuna majeruhi ambao ni Inonga, Saido, ambao wameanza kurejea taratibu mazoezini, lakini pia katika mechi iliyopita tulizalisha mwingine ambaye ni Clatous Chama ambaye msitarajie kumuona katika mchezo huu, waliosalia wapo tayari na mchezo," alisema.

Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein 'Tshabalala', amesema kutokana na maandalizi waliyofanya wanatarajia ushindi.

"Nafikiri kutokana na maandalizi tuliyoyafanya, inatupa mwanga mzuri, naamini tutafanya vizuri, najua Azam ina wachezaji wazoefu kwenye michuano yote, kwa hiyo hakuna mechi nyepesi tukicheza nao, ni kupambana tu," alisema.

Kocha Bruno Ferry, ametabiri mechi kuwa nzuri kutokana na aina ya soka la timu zote mbili na kiwanja kitakachochezwa kuruhusu 'boli' kutembea.

"Simba ni timu kubwa nchini na ina historia ndefu, hivyo tunajua kuwa tutakuwa na mechi nzuri na ngumu, nafikiri kwa sababu timu zote zinaweka mpira chini, na uwanja ni mzuri, watu watainjoi.

Ila nimewaambia wachezaji wangu kuwa kwa sababu tunacheza na timu kubwa, tunachotakiwa kufanya ni kuwa na umaliziaji mzuri wanapokuwa ndani ya eneo la hatari," alisema kocha huyo.

Mchezaji wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda alisema wachezaji wenzake wako tayari kutoa walichonacho kuhakikisha wanatwaa ubingwa.

"Tupo vizuri, kila mchezaji yupo tayari, sisi tunauona ni mchezo mkubwa, hivyo kila mchezaji atatoa alichonacho, tunautaka ubingwa," alisema.