Serikali yashauri mawakala mbolea kupewa mafunzo maalum

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 10:15 AM Apr 24 2024
Mbolea.
Picha: Maktaba
Mbolea.

SERIKALI imeshauri mawakala na wauzaji wa mbolea nchini kupatiwa mafunzo maalumu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, ili wasaidie kufikisha elimu hiyo kwa wakulima kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mbeya, Said Madito aliyasema hayo jana jijini Mbeya alipokuwa anafungua mafunzo ya matumizi ya mbolea za Kampuni ya Minjingu yaliyofanyika jijini Mbeya.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha mawakala wa mbolea kutoka katika mikoa minne ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Mbeya, Rukwa, Katavi na Songwe ambapo alisema mawakala hao ni kundi muhimu kwenye uboreshaji wa kilimo.

Alisema endapo wakipatiwa elimu sahihi itakuwa rahisi kuwafundisha wakulima matumizi sahihi ya mbolea kwenye mazao mbalimbali na kuongeza kiwango cha uzalishaji na hivyo kufikia malengo ya serikali ya kuifanya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo 2030.

“Wenzetu Mamlaka ya Udhibiti wa Viuatilifu na Afya ya Mimea (TPHPA) wameweka utaratibu kwamba hairuhusiwi kwa mfanyabiashara yeyote kuuza viuatilifu kama hajapata mafunzo, sasa na sisi huku kwenye mbolea tuanze kufikilia kwenda huko,” alisema Madito.

Alisema kuna baadhi ya maeneo nchini maofisa kilimo hawapo lakini hawa wauzaji wa mbolea wapo kila sehemu na hivyo wakipata mafunzo itakuwa rahisi kufanya kazi inayotakiwa kufanywa na maofisa kilimo.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Minjingu, Dk. Mshindo Msola alisema lengo la kampuni hiyo ni kuhakikisha inatoa mafunzo kwa mawakala kuhakikisha wanawauzia wakulima mbolea zinazokidhi mahitaji.

Alisema kila mbolea inayozalishwa inakuwa na malengo maalumu ikiwemo kujibu matakwa ya afya ya udongo ya shamba la mkulima pamoja na mazao ambayo mkulima anazalisha.

Alisema mbolea za minjingu zinafaa kwenye uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo ya muda mfupi na ya kudumu kutokana na kwamba ni mbolea za asili ambazo pia zinasaidia kulinda afya ya udongo.

Dk. Msola alisema kwa sasa serikali imefanya jitihada za kupima afya ya udongo katika maeneo yote nchini na ramani zimetolewa na hivyo ni rahisi wakulima kununua mbolea kulingana na afya ya udongo ya eneo lao.

“Sisi huu ni utaratibu wetu kila mwaka kukutana na mawakala wetu kufanya tathimini, kusikiliza kero zao na kuzitatua pamoja na kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, hawa sisi tunawaona kama ni maofisa ugani,” alisema Dk. Msola.

Hata hivyo aliwatoa hofu wakulima kuwa mbolea hazisababishi ugonjwa kwenye mazao kama ambavyo baadhi ya wakulima wa mpunga wilayani Mbarali walikuwa wanaamini kuwa ugonjwa wa virusi ulioshambulia mazao yao ulikuwa unasababishwa na mbolea.

Alisema ugonjwa huo ni wa siku nyingi na mpaka sasa umebainika kusumbua maeneo mengi nchini na hivyo akawataka wananchi kuendelea kuziamini mbolea hizo.

Baadhi ya mawakala walishukuru kwa kuanzishwa mafunzo hayo wakieleza kuwa yatawasaidia kuaminika kwa wakulima wanaonunua pembejeo kwao.

Mmoja wa mawakala hao, Diones Shonde alisema mara nyingi wakulima wamekuwa wakiwahoji maswali mbalimbali ambayo baadhi wamekuwa wakishindwa kujibu na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia kukidhi mahitaji ya wateja wao.

Kampuni ya Minjingu inaendelea kutoa mafunzo hayo kwa mawakala katika Kanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha elimu hiyo inasambaa nchi nzima.