Askofu Bagonza aibua uvundo wa mafarakano

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:12 AM Mar 28 2024
Askofu Dk. Benson Bagonza.
PICHA: JAMBO TV
Askofu Dk. Benson Bagonza.

ASKOFU Dk. Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, ametoa salamu za Pasaka, akilalamika kumea uvundo wa mafarakano serikalini hadi kanisani.

Kutokana na hali hiyo, Askofu Bagonza amependekeza kuwapo suluhisho la upatanisho kwa njia ya kufungua milango ya kuvumiliana, kubadilika na kujenga upya palipoharibika, huku kanisani akielekeza taasisi zake kuua alichokiita "Moshi wa chuki kuliko upendo". 

Katika salamu zake hizo za Pasaka zilizo kwenye ukurasa mmoja wenye aya tano, Askofu Bagonza anataja mambo manne yanayohitaji kufanywa na mihimili ya Bunge, Serikali na Mahakama, huku akitaja upatanisho kama msingi wa Tanzania kustawi.

Askofu huyo katika salamu hizo amezitoa , zikiongozwa na neno kutoka kitabu cha Walawi 16:29-30, Dk.Bangoza alisema nchi inahitaji upatanisho ili kufungua milango ya kuvumiliana, kubadilika na kujenga upya palipoharibika.

Neno alilonukuu Askofu Bagonza kutoka Kitabu cha Walawi 16:29-30, linasema: "Hili ni sharti ambalo mnapaswa kulifuata milele: Siku ya 10 ya mwezi wa saba, ninyi wenyewe na hata wageni wanaoishi miongoni mwenu, ni lazima mfunge siku hiyo na kuacha kufanya kazi. Mtafanya hivyo kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ambayo mtafanyiwa ibada ya upatanisho, msafishwe dhambi zenu, nanyi mtakuwa safi mbele ya Mwenyezi-Mungu." 

Katika salamu zake, Askofu Bagonza anasema: “Kila eneo katika taifa letu kuna uvundo wa mafarakano. Mihimili karibu yote-Bunge, serikali na mahakama kumejaa mafarakano na kuishi kwa tahadhari kubwa na hofu ya kuwindana. Ndani ya taasisi za dini kuna moshi wa chuki kuliko upendo. Mwathirika mkuu wa mafarakano haya ni mpendwa wetu haki.

"Hatuwezi kutenda wala kusimamia haki ikiwa uamuzi wetu umejaa hila, chuki, ubinafsi, rushwa, visasi na kuongozwa na itikadi, dini na makundi maslahi."

Dk. Bagonza ambaye ni mwanafalsafa na mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii, anasema Kristo anayeadhimishwa mateso, kifo na ufufuko wake, alitumika kupatanisha wanadamu na Mungu na kati ya mtu na mtu.

“Asiyekubali kupatanishwa hawezi kupatanisha wengine. Asiyepatanishwa na wengine wala kuwapatanisha wengine, amefarakana na Mungu. Upatanisho unawezesha kufungua milango mingine kufunguka. Milango hiyo ni kuvumiliana, kubadilika na kujenga upya palipo haribika.

“Agano jipya na la kale yanakubaliana kwamba damu (eshagama), ni alama ya ukombozi na upatanisho. Damu isiyo na hatia isipokomboa inalaani. Damu ya Bwana Yesu ilikomboa na kutupatanisha na Mungu. Kwa kuwa haikuwa na hatia, walioimwaga wanaalikwa kupatana na Mungu ili kuiepuka laana. Wanaoendelea kumwaga damu isiyo na hatia wanaalikwa kutubu na kupatanishwa na Mungu," anasema.

Askofu Bagonza anaongeza kuwa: “Mienendo yetu isiyofaa kama rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ukatili dhidi ya watoto, ukatili dhidi ya mazingira, udini, itikadi, biashara ya kuuza na kununua haki na dhulma dhidi ya taifa letu vinatokana na roho za mafarakano zinazokataa upatanisho.

“Kristo amefufuka, ninawasihi mpatanishwe. Rudini meza ya mapatano na madhabahu za kupatanishwa kwa sababu amri hii ni ya milele," Askofu Bagonza anahitimisha salama zake.

Wakristo nchini wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha Pasaka kuanzia kesho (Ijumaa Kuu) hadi Jumatatu (Jumatatu ya Pasaka).