Jeshi la Polisi lakaa mguu sawa kuelekea Sikukuu ya Pasaka

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 01:08 PM Mar 29 2024
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna, David Misime.

JESHI la Polisi limeonya wananchi kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyoathiri imani iliyopo, wakati dunia ikielekea katika sherehe ya Sikukuu ya Pasaka, ambayo itatanguliwa na ibada ya Ijumaa Kuu.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna, David Misime, viongozi wote wa dini watakaoendesha ibada ya usiku katika makanisa yao, wanapaswa kutoa taarifa kwa jeshi hilo katika maneo yao, ili kuimarisha ulinzi na usalama.

“Jeshi la Polisi tumejipanga kikamilifu kuhakikisha sherehe za Sikukuu ya Pasaka zinafanyika katika hali ya amani, utulivu na usalama wa kutosha. Tumejipanga kufanya doria katika mitaa na barabara zote kuu ili kuzuia uhalifu au uvunjifu wowote ule wa amani.

“Kwa viongozi wa madhehebu ya dini za kikristo, ambao watakuwa na ibada ya Ijumaa Kuu, zikiwemo za usiku katika kipindi hiki wasisite kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote.” alisema Kamanda Misime.

Kamanda Misime alisema jeshi hilo litaimarisha ulinzi mkali kwa kufanya doria katika nyumba zote za ibada nchini, wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu na Mkesha wa Pasaka, ambayo hukusanya watu wengi mchana na usiku.

Alisema doria hizo zitafanyika kwa siku nne mfululizo usiku na mchana, kuanzia Machi 28 hadi Jumatatu ya Pasaka ya Machi 31.

“Niwatake madereva wa vyombo vya moto kuepuka kuendesha vyombo hivyo, wakiwa wamelewa ama kujaza abiria kupita kiasi, alisema. 

Pia, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na kujiepusha na marafiki wa mitandaoni na matapeli wanaojitangaza kuwa wanatoa mikopo kupitia mitandao.

“Niwaombe wananchi kujiepusha na tabia ya kuwa na marafiki kwenye mitandao ya kijamii, ili kuepuka matapeli wanaojitangaza kuwa wanatoa mikopo, kwa njia ya mtandao na kuwatapeli wananchi,” alisema.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi nchini kuendelea kuzingatia kanuni ya kiusalama inayosema ‘Usalama unaanza na mimi mwenyewe’.