LSF, Smile wazindua msimu wa tatu wa mbio za Run For Binti

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:17 PM Mar 28 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng'wanakilala akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Smile Community, Flora Njelekela wakati wa Uzinduzi wa rasmi wa msimu wa tatu wa mbio za Run For Binti.
Picha: Elizabeth Zaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng'wanakilala akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Smile Community, Flora Njelekela wakati wa Uzinduzi wa rasmi wa msimu wa tatu wa mbio za Run For Binti.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Smile for Community(S4C), kwa kushirikiana na Shirika linalohusika na Uwezeshaji Kisheria(LSF), limetanagza msimu wa tatu wa mbio zinazojulikana kama Run for Binti zinazotarajiwa kufanyika Mei 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mbio hizo kufanyika kila mwaka kwa lengo la kuweka nguvu na rasilimali za pamoja katika kuwawezesha watoto wa kike kupata haki ya elimu na afya ya uzazi kwa kuhakikisha wanapata hedhi salama, na mazingira bora ya kusoma.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa msimu huo wa tatu wa mbio hizo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng`wanakilala, alisema katika kutekeleza mradi wa upatikanaji haki nchi nzima, ni vema kutumia mbinu mbalimbali kufikisha elimu kwa jamii juu ya namna ya kuwezesha upatikanaji haki nchini.

“Katika utekelezaji wa mradi wa upatikanaji haki, tumeona ni dhahiri kwamba wasichana na mabinti wadogo wanakabiliana na vizuizi visivyozuilika na vinavyozuilika katika kupata elimu, huduma za afya na haki zao nyingine za msingi,”amesema Lulu.

“Na ndio maana LSF na Smile tukaona tushirikiane pamoja na wadau mbalimbali ili kupunguza vikwazo na kutengeneza njia mpya itakayochochea kuwa na jamii yenye haki na usawa hususani kwa watoto wa kike.”

Mkurugenzi Mkuu wa Smile for Community, Flora Njelekela, alisema mbio hizo zitashirikisha wakimbiaji wa kilomita 21, 10 na tano.

Kadhalika, alisema siku hiyo kutakuwa na mbio nyingine zikiwamo za baiskeli za kilomita 55.

Alisema lengo la kukimbia mwaka huu ni kuwezesha watoto wa kike kupata mazingira bora ya elimu pamoja na afya ya uzazi na kwamba fedha itakayokusanywa itasaidia kujenga na kuboresha miundombinu kwa kujenga vyoo katika shule za sekondari, kusaidia upatikanaji wa maji kwa kujenga visima mashuleni. 

Kazi nyingine alisema zitasaidia kuboresha hedhi salama kwa kusambaza taulo za kike, kuchangia kwenye uhifadhi wa amzingira, kupitia upandaji miti na kutoa elimu juu ya kujilinda na kushughulikia ukatili wa kijinsia.