Mwanasheria adaiwa kutishiwa usalama

By Enock Charles , Nipashe
Published at 02:05 PM Mar 29 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga.
Picha: Maktaba.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga.

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimedai mwanasheria wake, Joseph Oleshangay, anayeishi jijini Arusha, ametishiwa usalama na watu wanaojitambulisha kuwa wanatoka katika Jeshi la Polisi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga, amesema hali ya mwanasheria huyo imekuwa hatarini kwa muda mrefu tangu 2023 kutokana na watu hao kumfuata mpaka nyumbani kwake kumuulizia bila kutoa sababu zozote.

“Hali ya usalama wa Joseph imekuwa hatarini kwa muda mrefu tangu 2023 na amekuwa anafuatiliwa ikiwamo kupigiwa simu na watu kumfuata huku wengine wakijitambulisha ni askari wa Jeshi la Polisi,” amesema.

Inadaiwa kuwa Machi 14 mwaka huu, Joseph alipata taarifa ya kufuatiliwa na watu wanaodaiwa kuwa wanatoka katika vyombo vya dola, hivyo kulazimika kuchukua tahadhari.

“Usiku wa kuamkia Machi 15, watu waliosema bila vitambulisho ni polisi walifika nyumbani kwake na kumkuta mke wake na kumwulizia Joseph bila kutoa sababu za kumtafuta,” alisema Henga.

Amesema mbali na watu hao kumkosa Joseph nyumbani kwake, waliweka kambi eneo la nyumbani kwa siku nne bila mafanikio.

Anna amesema matukio yote hayo yamekuwa yakimtia hofu Joseph pamoja na familia yake kwa sababu amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu, huku vitisho anavyopewa vikimsababishia kukosa uhuru wa kufanya kazi zake kama mwanasheria na wakili wa masuala ya ardhi.

Dk. Henga amesema baada ya kuona ujumbe mitandaoni kuwa Joseph ni mtu hatari walishangazwa sana japo hawakupuuzia na kwamba wanaendelea kufuatilia na watachukua hatua stahiki pale watakapojiridhisha usalama wake,  familia yake, jamii ya wamasai wanaoishi Ngorongoro na wafanyakazi wenzake wa kituo hicho. 

“Wakili Joseph Oleshangay ni Mmasai kwa asili, amezaliwa na kukulia katika Kata ya Endulen wilayani Ngorongoro na sasa ni mfanyakazi wa muda mrefu wa kituo hicho.  Kutokana na taaluma na nafasi yake ya kazi amekuwa akitoa msaada wa kisheria na ushauri kwa jamii yake ya kimasai hasa kwa wale wanaoishi ndani ya Mamalaka ya Ngorongoro (NCAA).

“Tangu mwaka 2022 serikali imekuwa ikiendelea kuwahamisha wananchi kutoka eneo la Ngorongoro na serikali imekuwa ikiliita ‘la hiari’, Joseph amekuwa akiisaidia jamii  yake kuhusu uelewa wa zoezi hilo,” amesema.

Alipotafutwa kuhusu madai hayo, Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna  Msaidizi Mwandamizi (SACP) Justine Masejo, simu yake ilipokelewa mtu aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake na kusema kuwa bosi wake alikuwa kwenye kikao, hivyo atafutwe baadaye. Hata hivyo, alipotafutwa baadaye, simu iliita bila kupokewa. Nipashe Digital inaendelea kumtafuta kamanda huyo.