Mwinyi aahidi kuwapunguzia wananchi hali ngumu ya maisha

By Suleiman Omar , Nipashe
Published at 11:53 AM Mar 29 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Ikulu Habari.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kukabiliana na hali ya ugumu wa maisha ili kuwapunguzia mzigo wananchi wake.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo Ikulu ya Pagali, Pemba alipozungumza na Wazee wa CCM.

Rais Mwinyi amesema kupanda kwa gharama za maisha kunachangiwa na changamoto nyingi za uchumi duniani, ikiwamo vita, kupanda bei kwa bidhaa za nje na baadhi ya mataifa duniani kuzuia kuuza bidhaa zao kwa mataifa mengine, akitoa mfano nchi ya India iliyozuia kuuza bidhaa zake kwa mataifa mengine duniani.

Alisema, hali hiyo huchangia kuzorotesha uchumi wa mataifa mengi na bei kupanda maradufu.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya kila linalowezekana kustawisha uchumi na hali za wananchi kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuimarisha hali ya uchumi kwa wananchi.

Akizungumzia changamoto ya bandari ya mkoani na hali ya kupanda kwa bei za bidhaa nchini, Rais Mwinyi aliwahakikishia wazee na wananchi wa kisiwa cha Pemba kwamba serikali ina nia ya kuleta meli ya moja kwa moja kutoka Bandari ya Mombasa hadi Bandari ya mkoani kwa ajili ya kushusha bidhaa ili kupunguza gharama za maisha na mfumko wa bei za bidhaa hizo.

Pia, Rais Mwinyi aliwaomba wazee kuendelea kuiombea dua nchi ili amani iendelee.

Wazee hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa hatua kubwa ya maendeleo ya nchi ilivyopiga ndani ya muda mfupi.

Aidha, wazee hao walipongeza hatua ya serikali kuendelea kuwalipa pensheni jamii, na kumshukuru, Rais Mwinyi kwa kuwaongezea kima cha pensheni hiyo.

Pia, walimpa pole Rais Mwinyi kwa msiba wa baba yake mzazi uliotokea hivi karibuni.