RIPOTI YA TAKUKURU 2022/23: Yafumua wizi mabilioni ndani ya serikali

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:45 AM Mar 29 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka 2022/2023 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, CP Salum Hamduni, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma jana.

RIPOTI ya mwaka 2022/23 ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeibua udhaifu kiutendaji na vitendo vya rushwa katika taasisi za serikali, baadhi ya vigogo wakifikishwa mahakamani na hata kuhukumiwa kifungo gerezani.

Miongoni mwa ‘madudu’ yaliyobainika, ni malipo ya fedha za utekelezaji miradi ilhali miradi yenyewe haijatekelezwa, ujenzi holela wa vituo vya mafuta na nyaraka feki kudhibitisha malipo ya safari za nje.

Akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu, Chamwino, Dodoma jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna Salum Hamduni, alitaja miradi iliyofuatiliwa ni pamoja na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa utaratibu wa Force Account na miradi 12 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yenye thamani ya Sh. bilioni 107.4 katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Tabora na Mbeya.

Alisema matokeo ya ufuatiliaji yalionesha kuwapo mianya ya rushwa, baadhi ya miradi ilionekana kutosajiliwa na Bodi ya Usajili ya Makandarasi na Wakala wa Usalama Mahali Pa Kazi na ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi.

“Matokeo mengine ni malipo kufanyika pasipo kufanyika baadhi ya kazi, malighafi za ujenzi kutopimwa ubora wake kinyume cha mkataba na kutozingatiwa kwa sheria na kanuni za ununuzi wa umma na kuwapo kwa nyongeza ya kazi pasipo kufuata utaratibu," alisema.

HATUA TAKUKURU

Kamishna Hamduni alisema TAKUKURU ilichukua hatua ikiwamo kuhakikisha marekebisho kwenye miradi husika yanafanyika ili serikali isipate hasara, pia kutoa elimu na kushauri wasimamizi wa miradi na mamlaka husika namna bora ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Alisema katika ufuatiliaji wa miradi 1,800, miradi 171 yenye thamani ya Sh. bilioni 143.3 ilibainika kuwa na utekelezaji hafifu na kuanzisha uchunguzi. Miradi hiyo ni ya sekta za ujenzi, fedha, maji, kilimo na majengo.

"Mapendekezo 3,668 yalitolewa ili kurekebisha kasoro zilizobainika katika ufuatiliaji huo kuhakikisha marekebisho kwenye miradi husika yanafanyika kwa fedha ya mkandarasi au fedha iliyofujwa inarejeshwa serikalini.

“Jumla ya mapendekezo 2,740 yalitekelezwa sawa na asilimia 89.4 ya utekelezaji mapendekezo yaliyotolewa na TAKUKURU.

“TAKUKURU ilifanya kazi 790 za uchambuzi wa mifumo ya utoaji huduma kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna ya kuziba.

“Kwa ujumla uchambuzi ulibaini baadhi ya watendaji waliokuwa wanasimamia miradi ya Force Account kutokuwa na uelewa au kuwa na uelewa mdogo kuhusu taratibu za ununuzi.

“Ukiukwaji sheria na miongozo wakati wa kuunda kamati za usimamizi, ukiukwaji sheria wakati wa kufanya ununuzi na usimamizi wa miradi, kutokuwapo mfumo wa uthibiti wa weledi na taaluma katika utekelezaji miradi inayotumia Force Account.

“Upungufu wa wataalam, ukosefu wa fedha za usimamizi na ufinyu wa muda wa utekelezaji miradi na kutokuwapo kwa ukomo wa matumizi ya njia ya Force Account," alisema.

Kamishna Hamduni alisema ili kuondokana na upungufu huo, TAKUKURU iliwasilisha mapendekezo Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

VITUO MAFUTA

Bosi huyo wa TAKUKURU alisema taasisi hiyo pia ilifanya uchambuzi wa uzingatiwaji mfumo wa taratibu za ujenzi wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

“Uchambuzi huu ulihusisha vituo vya mafuta 38. Asilimia 79 ya vituo vilivyofikiwa katika uchambuzi vilizingatia sheria kwa kuwa na vibali vya ujenzi kutoka katika halmashauri ambako uwekezaji umefanyika.

“Asilimia 21 ya vituo vilivyofikiwa havikuwa na leseni wakati ufuatiliaji unafanyika. Tulibaini kuwapo ongezeko la maombi ya ubadilishaji matumizi ya ardhi kutoka yaliyopangwa awali na kuwa vituo vya mafuta.

“Pia tulibaini tatizo la ujenzi wa vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu; vinaongezeka na kuleta hofu na usalama kwa wananchi. TAKUKURU imewasilisha mapendekezo namna ya kukabiliana na upungufu huo na kuwasilisha kwa mamlaka husika," alisema.

RUSHWA MSITUNI

Kamishna Hamduni pia alisema walifanya tathmini ya hatari ya rushwa katika uvunaji na usafirishaji mazao ya misitu na yenye hatari ya rushwa ni kwenye uundwaji kanuni na miongozo ya uvunaji na usafirishaji mazao ya misitu, usimamizi wa uvunaji, usafirishaji, upatikanaji leseni na mfumo wa ukusanyaji kodi ukionekana kuwa na udhaifu.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2022/23, kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi, TAKUKURU imeokoa Sh. bilioni 87.59, ikiwa ni pamoja na Dola milioni 33 (Sh. bilioni 76.34) kupitia uchunguzi wa Mkongo wa Taifa.

Katika hilo, Kamishna Hamduni alisema ilibainika Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano ulijenga miundombinu ya mawasilinao kinyume cha makubaliano na kuikosesha serikali mapato kutokana na huduma zao kutopita katika Mkongo wa Taifa.

“Kupitia mkataba wa makubaliano katika ya Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, umoja huo ulikubali kulipa Dola milioni 20 katika kipindi cha miaka mitano na kulipa pamoja na riba ya asilimia 3.5 kwa mwaka na Dola milioni 13 zitalipwa kwa njia ya uwekezaji kati ya serikali kupitia wizara husika,” alisema.

Uokoaji mwingine aliutaja ni wa Dola milioni 2.971 (Sh. bilioni saba) zilizotokana na mkataba ulioingiwa mwaka 2007 kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Pangea Minerals Limited.

Alisema pia wameokoa Sh. bilioni nne za halmashauri zilizochepushwa na kupitia uchunguzi, zilirejeshwa katika halmashauri na sekretarieti za mikoa.

“Vyama vya ushirika tumedhibiti na uokoaji fedha milioni 248.8 zilizofanyiwa ubadhirifu, zilirejeshwa katika vyama.

“TAKUKURU pia imechunguza na kukamilisha majalada 900 yakiwamo 21 ya rushwa kubwa, yakihusisha ubadhirifu na hasara kwa serikali ikiwamo wa Sh. bilioni 8.9 zilizokusanywa kwa njia ya mashine za POSS na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

“Fedha hizi hazikupelekwa benki, lakini watuhumiwa walighushi nyaraka wakionesha zimepelekwa benki. Uchunguzi wa ubadhirifu wa Sh. bilioni nne zilizotokana na makusanyo ya TANAPA, Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Bodi ya Utalii umefanyika," alisema.

SAFARI HEWA

Kamishna Hamduni alisema uchunguzi mwingine ni wa safari hewa nje ya nchi zilizosababishia NCAA hasara ya Sh. bilioni 1.3 na uchunguzi wa upotevu wa Sh. bilioni 14 uliofanywa na iliyokuwa menejimenti ya DART.

“Uchunguzi kuhusu ukodishaji wa maghala ya UDA kinyume cha utaratibu na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 20.5 umefanyika pamoja na upotevu wa vipuri vya UDART uliosababishia serikali hasara Sh.  bilioni 3.29.

“Pia tumefanya uchunguzi wa Sh. bilioni nne uliohusu ukiukwaji wa taratibu za ununuzi katika Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) kwenye Bandari ya Dar es Salaam wakati wa ununuzi wa mfumo wa Enterprises Resources Plan uliofanywa na kampuni ya Zimbabwe.

“TAKUKURU pia imefanya uchunguzi wa Sh. bilioni 1.6 zilizochepushwa na kufanyiwa ubadhirifu Bandari ya Kigoma ambako watuhumiwa walighushi saini wakishirikiana na watumishi wa benki na kufanikiwa kutoa fedha hizo," alisema.

RIPOTI CAG

Kuhusu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kamishna Hamduni alisema walizipitia na kufungua majalada 375 yenye viashiria vya rushwa na jinai.

Alifafanua kuwa majalada 156 yalifungwa kwa kukosa ushahidi na jinai na majalada 73 walibaini watendaji wa serikali walikiuka taratibu, lakini hawakupata ushahidi wa jinai, bali wa kuwachukulia hatua za kinidhamu.

“Mashauri 114 yalifunguliwa mahakamani na 41 yaliamuliwa na kati ya hayo, mashauri 40 tulishinda na kupoteza shauri moja. Majalada 160 uchunguzi unaendelea,” alisema.

Kamishna Hamduni alisema TAKUKURU pia ilifanyia kazi majalada yanayotokana na Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge ambapo kwa mwaka jana miradi 20 ilikataliwa.

Kwa ujumla, katika mwaka huo, kesi mpya 600 zilifunguliwa mahakamani. Kati yake, 594 zilifunguliwa mahakama za chini na sita Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

“TAKUKURU na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inachunguza na kuweka zuio za mali zinazodhaniwa kupatikana kwa rushwa ambazo ni magari 15, mashamba sita, hoteli tatu, nyumba za kulala wageni nne, viwanja 29, nyumba za makazi 25, baa mbili, fremu mbili za maduka na shule moja,” alisema.