Ulaji ulivyo serikalini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:38 AM Mar 29 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 kutoka kwa CAG Charles Kichere, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma jana.

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 imekabidhiwa kwa Rais, ikiibua ulaji wa fedha za umma, huku utendaji katika baadhi ya taasisi ukiimarika.

Akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Ikulu, Chamwino, mkoani Dodoma jana, CAG Charles Kichere, alibainisha kuwa kwa mwaka huo wa ukaguzi, ofisi yake imetoa hati 1,209 za ukaguzi. Kati yake, hati safi ni 1,197 sawa na asilimia 99, hati zenye shaka ni tisa, hati mbaya ni moja na hati mbili za kushindwa kutoa maoni.

CAG alisema kuwa hadi Juni 30, 2023, Deni la Serikali lilikuwa Sh. trilioni 82.25 sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka Sh. trilioni 71.31 kwa 2021/22.

“Deni hilo linajumuisha Deni la Ndani Sh. trilioni 28.92 na la nje Sh. trilioni 53.32. Kipimo cha Deni la Serikali kinachotumia Pato la Taifa kinaonesha deni hili ni himilivu,”alisema.

CAG alifafanua kuwa uwiano wa kulipa madeni na mauzo ya nje ni asilimia 12.7, chini kidogo ya kiwango cha ukomo cha asilimia 15 na uwiano wa malipo ya madeni na mapato ni asilimia 14.3, chini ya kidogo ya kiwango elekezi cha asilimia 18.

Vilevile, alisema ukaguzi katika Mamlaka ya Mapato (TRA)umebaini makusanyo ya kodi Sh. trilioni 22.58 kwa mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia nane kulinganishwa na Sh. trilioni 20.94 mwaka 2021/22.

“Licha ya ongezeko hilo, makusanyo hayo yalikuwa chini Sh. trilioni 1.07 sawa na asilimia 4.5 ya makadirio,” alisema na kubainisha kuwa alibaini TRA inakabiliwa na tatizo la udhibiti wa bidhaa zinazopita nchini kuelekea nchi jirani kutokana na upungufu wa ving’amuzi vya kielektroniki ambao unadhoofisha ufanisi katika kuhakiki mizigo inayokwenda nje ya nchi.

Pia alibaini upungufu katika utoaji mizigo inayotokana na ving’amuzi kukosekana kwenye mfumo wa ECTS, kuwa na taarifa zisizo sahihi na kutowiana kwa taarifa kati ya vifaa saidizi na vifaa vikuu kwenye mfumo.

Kuhusu mapato yasiyo ya kodi, CAG alisema amebaini mashirika manane ya umma yalikusanya mapato ya Sh. bilioni 23.27 nje ya mfumo wa kielektroniki wa malipo ya serikali (GEPG), hivyo kukiuka Waraka wa Hazina Na. 3 wa Mwaka 2017.

MADUDU H'SHAURI

CAG alisema kuna mapato yasiyokusanywa ya Sh. bilioni 61.15 na mapato yasiyowasilishwa benki ya Sh. bilioni 6.19 kutoka vyanzo muhimu na vikubwa kwenye halmashauri, hali inayoathiri uwezo wa mamlaka za serikali za mitaa kutekeleza miradi na kutoa huduma bora kwa jamii.

Alisema mamlaka 184 za serikali za mitaa hazikutenga Sh. bilioni 20.23 za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shughuli za uendeshaji vijiji au mitaa.

Pia alisema uchunguzi umebaini kuwapo halmashauri 10 zilizolipa jumla ya Sh. bilioni 2.95 kwa kazi zilizotekelezwa bila kuwapo nyaraka zinazoonyesha ukubwa wa kazi.

“Na mamlaka nne zililipa Sh. milioni 346.69 kwa kazi ambazo hazikutekelezwa kutokana na kutokuwapo usimamizi unaoridhisha wa miradi. Hii inakawamisha juhudi, uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa malipo hasa kwenye utekelezaji miradi ya maendeleo," alisema.

DOSARI MSD

CAG pia alisema ukaguzi umebaini Bohari ya Dawa (MSD) imetoa zabuni ya vifaa vya maabara vya upimaji wa Uviko-19 na kubaini kampuni iliyopewa kazi hiyo haikuwa mtengenezaji wa vifaa hivyo kinyume cha masharti ya zabuni.

“Baada ya vifaa kufika, wataalamu walibaini havifai kwa mashine zetu na MSD ililipa fedha zote. Ninapendekeza hatua zichukuliwe kwa wahusika na kurejesha fedha hizo za umma,” alisema.

CAG Kichere pia alisema amebaini utaratibu duni katika utekelezaji miradi, akifafanua: “Taasisi kama TANESCO na taasisi za huduma za maji zinaingilia barabara zinazosimamiwa na TARURA. Kwa mfano, Arusha serikali ilitumia Sh. bilioni 194.53 katika mradi wa barabara lakini ukaharibiwa na kazi za mamlaka ya maji ambayo ilianza tu baada ya barabara kukamilika, hivyo wanatakiwa kuingia gharama nyingine kwa kuharibu miundombinu."

MITA TANESCO

CAG alisema ukaguzi wake katika mita za umeme umebaini mita 108,088 kati ya 602,266 zilibadilishwa na TANESCO kabla ya kipindi cha uhai wa matumizi yake kuisha. Kati yake, mita 13,493 zilibadilishwa ndani ya mwaka mmoja baada ya kufungwa kwake.

“Na mita 94,595 zilikuwa na muda mfupi wa matumizi kati ya mwaka mmoja hadi 15 kinyume cha muda unaokubalika wa miaka 20 kwa mujibu wa TANESCO wenyewe," alisema na kutoa angalizo kuwa kubadilisha mita mapema kunasababisha gharama kubwa kwa shirika.

Pamoja na hayo, CAG alisema amebaini TANESCO kuchelewa kutekeleza miradi ya kijamii (CSR) yenye thamani ya Sh. bilioni 262 toka Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Nyerere (JNHPP).

“Katika mradi huu, CSR ilikuwa ni kujenga kituo cha michezo na kuboresha barabara. Hata hivyo, ilitokea hali ya kutoelewana kati ya TANESCO na mkandarasi na kusababisha mabadiliko kadhaa ikiwamo kujenga vituo vya ufundi kwenye maeneo mbalimbali na mabadiliko haya yamesababisha kuchelewa kwa makubaliano ya kina kuhusu utekelezaji miradi ya kijamii na kuhatarisha uwezo wa mradi wa kuwapa faida na mradi wananchi,” alisema.

USIMAMIZI MIKATABA

CAG pia alisema uchunguzi umebaini matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma katika taasisi mbalimbali za serikali yanayosababisha hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 222.34.

“Hasara hii inatokana na kucheleweshwa malipo kwa makanadarasi wenye miradi ya barabara na hivyo kusababisha malipo makubwa ya riba," alisema.

CAG pia alisema amebaini katika miradi ya barabara, meli, vivuko, maji na umeme kuna matatizo yanayoathiri utekelezaji wake ikiwamo kuchelewa kukamilika kwa miradi na mingine kukamilika kwa kiwango cha chini na kuongeza gharama za ukamilishaji.

“Tulichukua miradi mitano ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS na tukagundua gharama zake ziliongezeka kwa Sh. bilioni 130, ukaguzi wa kiufundi wa udhibiti wa gharama umebaini kulikuwa na ongezeko la gharama Sh. bilioni 130.51 ambalo limesababishwa na upungufu mkubwa ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina usio sahihi umesababisha ongezeko la gharama Sh. bilioni 44.97 sawa na asilimia 34 ya gharama zote za ziada.

“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ilisitisha miradi ya miaka ya nyuma yenye thamani ya Sh. bilioni 26.68 kwa mwaka 2022/23 na ilitokana na tathmini iliyoonesha kwamba miradi hii haitekelezeki licha ya kulipiwa fedha na ilifutwa kama hasara,” alisema na kueleza kuwa uamuzi huo umetokana na usimamizi duni wa miradi na upembuzi yakinifu usiokidhi haja.

CAG pia alisema amebaini mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yamepata hasara ikiwamo Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepata hasara ya Sh. bilioni 56.64 sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya Sh. bilioni 35.24 iliyoripotiwa mwaka uliopita.

“Kampuni imetengeneza hasara hii licha ya kupokea ruzuku ya Sh. bilioni 31.55 kutoka serikalini na kuonesha kiasi cha Sh. bilioni 9.71 ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato kwa mwaka wa fedha 2022/23,” alisema.

HASARA YAPUNGUA

Alisema Shirika la Mawasiliano (TTCL) kwa mwaka 2022/23 limepata hasara ya Sh. milioni 894, ikipungua kwa asilimia 94 kulinganishwa na hasara ya Sh. bilioni 19.23 ya mwaka uliopita.

“Shirika limetengeneza hasara hii licha ya kupokea ruzuku ya Sh. bilioni 4.55 kutoka serikalini na kuonesha kiasi cha Sh. bilioni 4.4 ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato yake kwa mwaka 2022/23,” alisema.

CAG alisema Shirika la Reli Tanzania (TRC) limepata hasara ya Sh. bilioni 100.7 ambayo imepungua kwa asilimia 47.32 kulinganishwa na hasara ya Sh. bilioni 190.01.

“Hasara hii imetokea licha ya kupokea ruzuku ya Sh. bilioni 32.81 kutoka serikalini kwa ajili ya matumizi ya kawaida,”alisema.

CAG alisema kampuni ya uwekezaji ya TANOIL ilipata hasara ya Sh. bilioni 76.56 ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 68.72 kutoka hasara ya Sh. bilioni 7.84 kwa mwaka uliotangulia.

Alisema hasara ilitokana na mafuta kutoka nje kuzuiwa na TANOIL kushindwa kuwalipa wauzaji na gharama kubwa ya kuhifadhi mafuta Sh. bilioni 12.9 kulinganishwa na Sh. bilioni 6.1 ya mwaka uliotangulia.

Pia alisema mapato ya kampuni kutokana na mauzo ya mafuta yalipungua kwa Sh. bilioni 296 sawa na asilimia 49. Waliuza lita za mafuta milioni 112 kulinganishwa na lita milioni 264 kwa mwaka uliotangulia.

CAG alisema Shirika la Posta lilipata hasara ya Sh. bilioni 1.34 kulinganishwa na faida ya Sh. bilioni 16.21 kwa mwaka uliopita na faida hiyo ilitokana na mauzo ya mali za shirika si biashara.

ANGALIZO

CAG Kichere pia alitoa angalizo kwa serikali kuhusu kuunganisha mashirika yanayojiendesha kwa hasara na mengine kufutwa na kupendekeza zoezi hilo liwe shirikishi kwa taasisi zote muhimu za serikali ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika mchakato huo.

“Taasisi za kushirikishwa ni pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Mkurugenzi Msimamizi wa Mali za Serikali na Msajili wa Hazina. Ninatoa angalizo hili hasa linapokuja suala la kugawana mali na madeni ambapo huwa kuna changamoto,”alisema.

Alitolea mfano Sh. bilioni 2.6 zilizokuwa bakaa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyovunjwa hakijagawanywa hadi sasa tangu mwaka 2020/21.

“Hii inachangia kupotea kwa mali na fedha, ninaendelea kuangalia hizi fedha zipo wapi. Pia ninashauri Shirika la NDC kuangalia kwa umakini kutokana na unyeti wa mambo yake na serikali itoe mtaji wa taasisi kama hizi ili kuboresha utendaji wao,” alishauri.

CHETI KIMATAIFA

CAG pia alisema kuwa Januri 6, mwaka huu , Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ilipata cheti cha kutambulika kimataifa kwa mfumo wa usimamizi wa ubora kilichotolewa na taasisi ya kimataifa ya viwango vya ubora.

"Ofisi yangu pia imeendelea kukagua Kamisheni ya Usimamaizi wa Anga la Afrika ambayo makao makuuu yake yako mjini Dakar, Senegali kwa mkataba wa miaka mitatu utakaokamilika 2025, tunaendelea na mkataba wa kukagua Umoja wa Afrika, mkataba utakaokamilika mwaka huu 2024," alisema.

CAG alisema kwa kushirikiana na nchi zingine wanachama, ofisi yake pia inakagua Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi zake.

"Tumepata mkataba mwingine wa miaka sita wa kukagua mahakama maalum inayoshughulikia kesi za watu waliohusika na uhalifu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone. Mahakama hii iko The Hague, Uholanzi,”alisema.

NHIF

CAG pia alisema Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa ukipata hasara kwa miaka mitano iliyopita na kwa mwaka 2022/23 hasara ilikuwa Sh. bilioni 156.77, ikipungua kutoka Sh. bilioni 205. 95; michango ya wanachama imeongezeka kwa asilimia 14.6 na matumizi yameongezeka kwa asilimia 10.

Alisema kuna mambo yanaweza kuathiri uhai wa muda mrefu wa mfuko ikiwamo mikopo ya serikali ambayo haijalipwa ya Sh. bilioni 208 inasababisha mzigo mkubwa wa kifedha na serikali kwa mwaka 2024/25 imepanga kulipa Sh. bilioni 180.

“Wastaafu na wenza wao kunufaika bila kuchangia kunagharimu mfuko Sh. bilioni 84.7 kwa mwaka, kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza pia kunagharimu mfuko Sh. bilioni 137.8 kwa mwaka, hizi ni changamoto zinazoongeza shaka ya uhimilivu wa mfuko. Ninapendekeza mfuko ufikirie mikakati ya kuzalisha faida na serikali ilipe mikopo yake,”alisema.

CAG pia alisema Benki ya Maendeleo ya TIB inakabiliwa na tatizo la utoshelevu wa mtaji ambapo hadi Desemba 2023 ilikuwa na Sh. bilioni 88.12 wakati masharti yanataka iwe na mtaji wa Sh. bilioni 200.

“Serikali inapanga kutoa mtaji wa Sh. bilioni 118, hatua hii ni muhimu sana lakini haitoshi kwa kuwa TIB inamdai Msajili wa Hazina Sh. bilioni 37 tangu 2019,” alisema.

MFUMO WA MISHAHARA

CAG pia alisema amebaini tatizo kwenye Mfumo wa Pamoja wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ambao unaruhusu watumishi kupokea mishahara wakiwa likizo za bila malipo, kupandishwa vyeo bila kukidhi miaka mitatu ya utumishi, kushushwa vyeo bila mabadiliko ya mshahara na kuwapa watumishi wenye namba za utambulisho zinazofanana.

AFYA YA AKILI

Mdhibiti huyo pia alisema amebaini upatikanaji huduma ya afya ya akili una upungufu na kuathiri jamii; utambuzi wa wagonjwa haufanywi kwa ufanisi katika ngazi ya jamii.

Alisema utambuzi unaofanywa unalenga zaidi watumiaji dawa za kulevya, wazee, walemavu, watoto waliopata mimba na wanaoishi mazingira magumu na kupuuza wengine, hali inayotokana na upungufu wa wataalamu ngazi ya jamii kwenye vijiji na mitaa.

Pia alisema huduma za kisaikolojia hazipatikani kwa wakati kwa watu wenye uhitaji, hali inayowaathiri wagonjwa wa afya ya akili na makundi mengine.

Alisema Wizara ya Afya haina mpango wa kuajiri wataalamu wa afya ya akili na kutumia madaktari wenye utaalamu mwingine.

“Imebainika kati ya mikoa 28 ni mikoa mitano tu ina vituo vya utengano wa huduma za afya ya akili ambayo ni Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma. Ninapendekeza fedha ziongezwe kwenye huduma ya afya ya akili hasa katika jamii na kuajiri wataalamu zaidi wa afya ya akili,” alihitimisha.

CAG alikabidhi kwa Rais Samia ripoti kuu ya ukaguzi na ripoti za ukaguzi wa: Serikali Kuu; Mamlaka za Serikali za Mitaa; Mashirika ya Umma; Miradi ya Maendeleo; Ufanisi pamoja na ripoti za ukaguzi wa ufanisi katika maeneo 14, ikiwamo ukusanyaji wa madeni ya mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.