Vitabu kufundishia, kujifunzia na mitaala mipya vyasambazwa

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:09 AM May 10 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Picha: Maktaba
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

SERIKALI imechapisha nakala 9,818,251 za muhtasari, vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu na kuvisambaza katika shule za msingi zinazotumia mtaala mpya kujifunza na kufundishia darasa la kwanza na la tatu.

Pia katika mwaka 2023/24, serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu, ili kukidhi hitaji la ongezeko la wanafunzi nchini na kuboresha elimu .

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Andrew, aliyehoji serikali ina mpango gani wa kuwezesha upatikanaji wa vitabu katika shule za msingi ambazo zimeanza mtaala mpya wa kingereza kuanzia darasa la kwanza.

Amesema katika nakala hizo, 509,582 ni za muhtasari na mtaala ulioboreshwa wa elimu ya awali, msingi na sekondari, 8,069,826 ni za vitabu vya kiada vya maandishi ya kawaida kwa darasa la awali, darasa la kwanza na la tatu kwa shule zinazotumia Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia.

Prof. Mkenda pia amesema nakala 43,785 ni  vitabu vya maandishi yaliyokuzwa 6,990 ni  vitabu vya breli na nakala 1,183,568 za viongozi vya mwalimu vikiwa vimesambazwa kwa uwiano kati ya 1:2 hadi  1:4.

Akijibu  swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Nora Mzeru  aliyehoji ni  lini serikali itaajiri walimu wa kutosha kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema inatarajia kuajiri walimu 12,000 kukidhi mahitaji hayo.

Amesema pia serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari akitolea mfano kuwa katika  mwaka 2020/21 hadi 2022/23, iliajiri walimu 29,879 wakiwemo 16,598 wa shule za msingi na 13,281 wa shule za sekondari.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Janejelly  Ntate, amehoji lini serikali itaajiri watalaam wa maabara katika shule za sekondari ili kuwapunguzia mzigo walimu wa sayansi kufanya kazi kama watalaam wa maabara.

Akijibu swali hilo, Mchengerwa amesema kati ya mwaka 2020/21 hadi 2022/23 serikali iliajiri wataalam wa maabara 165 ambao walisambazwa katika shule mbalimbali za serikali kadri ya mahitaji hata hivyo itaendelea kuajiri wataalam wa maabara kila mara nafasi za kuajiri zinapotolewa kulingana na upatikanaji wa fedha.

“Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa wataalam wa maabara shuleni. Wataalam wa maabara ni wasaidizi muhimu wa walimu wa masomo ya sayansi hasa katika kufundisha kwa vitendo,” amesema.

Amewapongeza walimu ya sayansi nchini kwa kazi kubwa wanayoifanya kwani  kwa sasa wamekuwa wakitumika kuandaa vifaa na kemikali kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo na mitihani kwa wanafunzi.