Waziri Silaa anavyomaliza papo kwa hapo, Rais amkubali anavyotekeleza

By Joyce Lameck ,, Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 08:37 AM Mar 28 2024
Waziri Jerry Silaa, katika nyendo zake kutatua migogoro katika maeneo yenye matatizo.
Picha: Wizara ya Ardhi.
Waziri Jerry Silaa, katika nyendo zake kutatua migogoro katika maeneo yenye matatizo.

ARDHI katika jamii ni rasilimali muhimu, ambayo katika sura ya pili imekuwa ikibeba migogoro mingi ya kijamiii isiyoisha nchini. Hapo mtu anaweza kuhoji sababu zake.

Moja lililo wazi ni kwamba kutopatikana elimu sahihi ya usimamizi wake katika jamii, ikiwamo utambuzi wa mipaka sahihi. 

Ni sababu mojawapo inayomfanya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Jerry Slaa, anasimamia kuhakikisha kila haki na uhalali wake unachukua nafasi; kunavyotengwa maeneo sahihi ya ujenzi kama vile hospitali, shule, soko na viwanja vya michezo hukohuko penye mgogoro.

Nadharia iliyoko ni kama hadhira inaweza kujikita kwenye mifumo mbalimbali ya utafutaji pesa bila kusahau elimu inayotolewa, nayo inapaswa kuangukia katika darasa la mipango miji.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kimsingi, ina majukumu: Kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kusimamia upangaji wa miji na vijiji, kupima ardhi na kutayarisha ramani.

Pia, inatoa hati kumiliki na hatimiliki za kimila za ardhi; kusajili hati za umiliki ardhi na nyaraka za kisheria; kuthamini mali; kuhamasisha na kuwezesha wananchi kuwa na nyumba bora.

Eneo lingine linagusa kutatua migogoro ya ardhi na nyumba, kusimamia upatikanaji na utunzaji kumbukumbu za ardhi, kusimamia ukusanyaji maduhuli ya serikali yatokanayo na huduma za sekta.

Wizara pia inasimamia taasisi chini yake zikiwamo; Shirika la Nyumba la Taifa, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.

Mengine ni Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi; Wakala wa Uendelezaji Mji Mpya wa Kigamboni; na kusimamia uendeshaji vyuo vya ardhi vya Tabora na Morogoro.

Hadi sasa katika utekelezaji huo, kuna malalamiko mengi ya watu katika maeneo wanayoyamilikii yamechukuliwa au hitilafu kisheria. Moja ya sababu ni kuwa na ardhi ziko sehemu zisizo sahihi, zimeshapangiwa na serikali kwa matumizi mengine kama barabara.

Katika jitihada zake Waziri Silaa akiwa na wastani wa miezi sita, anatatua migogoro ya ardhi kitaifa akitumia staili kuwa mbele vitani na kikosi kamili chenye majibu ya tatizo, akitolea majibu hukohuko penye mgogoro sasa mafanikio yanaanza kuonekana kwa wananchi, haki zao kupatikana.

ALIVYOANZA KAZI

Ni mfumo wake tangu kuteuliwa amekuwa kiongozi asiyetulia ofisini, anatembelea mikoa mbalimbali akisikiliza kero za migogoro ya ardhi ambayo ni kilio kikubwa kitaifa, hasa kwenye suala la mirathi, hata kutokeza mikasa isiyo ya  kibinadamu.

Agizo lake kwa maofisa ardhi ikawa kuacha kuwa washauri kisheria kwa wananchi, bali watendaji kitaalamu. 

Kwa historia yake, Waziri Silaa alianza kazi Septemba mwaka jana katika wadhifa wa sasa akiahidi wizara yake “Itahakikisha kero zote za migogoro ya ardhi zinakwisha, ikiwamo jijini Dodoma.”

Akaitaja kuwa sehemu ya utekelezaji rasmi wa maagizo kwake ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni tamko lake la Novemba iliyopita, kwa wananchi waliofika katika alichokibuni ‘kliniki ya ardhi’ anayoiendeleza hadi sasa 

Waziri huyo akawaambia wananchi waliofika kupata huduma katika kliniki hiyo kuwa, atakuwa akifanya nao mazungumzo kila baada ya kumaliza ratiba za bunge, ili kujionea mwenyewe kero zinazowakabili za ardhi.

Silaa akawaelekeza watendaji wa sekta ya ardhi nchini, kuhakikisha ndani ya 100 kuanzia Septemba mwaka jana aingie katika jukumu hilo, wanatatua migogoro ya ardhi kwa nafasi zao.

Aidha, akawataka waliovamia maeneo ya wazi kuanza kuondoka mara moja huku akielekeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Ardhi wenye mamlaka ya kusimamia sheria katika maeneo mbalimbali, ya wazi.

Hilo akalitolea ufafanuzi, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga, akinena kuwa ‘Kliniki ya Ardhi, itakuwa mwarobaini wa changamoto nyingi zinazowakabili wananchi wengi,’ akitumia mfano wa jijini Dodoma.

Hapo ndipo akatangaza kutanua wigo na ziara za mbali, akiwa na ufafanuzi: “Kliniki ya Ardhi kwa sasa iko Dodoma na ni endelevu kwa mikoa yote. 

“Pia, wizara inakusudia kuweka mifumo rahisi ya kutoa huduma kwa wananchi, ikiwamo kufunga kamera katika ofisi za utoaji huduma ili kuepuka mianya ya ukiukwaji sheria.”

Kila anapokuwa ziarani kuendeleza mkakati huo, Waziri Silaa, amekuwa mbunifu kulingana na mazingira. Mathalan mkoani Kilimanjaro miezi kadhaa baada ya uteuzi wake, akiunda kamati za kukusanya taarifa kutatua migogoro ya ardhi katika vijiji vya Bangalala, Mwembe na Makanya vilivyopo wilayani Same.

Hiyo ni baada ya kufanya mkutano wa hadhara na wanakijiji, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni kutatua migogoro ya umiliki wa ardhi.

Ni kamati iliyoundwa na wawakilishi wa wananchi vijijini, Kamishna wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same na wataalamu ardhi, ili apate uamuzi sahihi lwa suala hilo.

 CHANGAMOTO ZINAZOMKABILI 

Katika ziara zake ambazo zinamng’arisha sasa kiutendaji Silaa, anakabiliwa na uhaba wa rasilimali watu na fedha, anakosa taarifa sahihi za miliki ya ardhi na uchelewashaji wa malipo ya fidia.

Mengine inatajwa ni kulimbikizwa kodi ya pango la ardhi, migogoro, uvamizi wa ardhi, kasi ndogo ya upangaji na upimaji ardhi, ikilinganishwa na uhitaji uliopo kwa kwa jili ya matumizi mbalimali.

Anataja hatia zake ni serikali inahakikisha viwanja vyote vilivyopimwa vinamilikishwa kwa wahusika, kukiongezeka kasi ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi, kuwekwa utaratibu bora mzuri wa mgawanyo wa fedha zinazohitajika kutumiwa.

MTAZAMO WA WADAU

Baadhi ya wananchi wanatoa maoni yao wakimpongeza waziri huyo wakitambua namna anavyotatua migogoro ya wananchi kwenye maeneo mengi, hata wanatoa rai aigwe na viongozi wengine.

Rashid Mkumba, anasema: “Kwa kweli anawasaidia sana watu ambao walikuwa kwenye migororo ya ardhi, amekuwa akifanya kazi bila kuangaalia mazingira mjini, vijijini kote. Anafanya kazi hivyo jitihada zake zimekuja na mafanikio kwa wengi.”

Mwingine Agustino Njana, anaunganisha: “Huyu ni kiongozi wa kuigwa kwa sababu anafanya kazi usiku na mchana, wakati wengine wanakaa kwenye ofisi zao bila kujali wananchi wana changamato kiasi gani, lakini Silaa anazungukua na kufuata migogoro ilipo na kuhakisha anawapa majawabu sahihi tena kwa haki.”

SIKU 100 KAZINI

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ikawa na ufafanuzi ufuatao siku alipotimiza siku 100 kazini, mnamo Desemba 21, mwaka jana, Waziri Silaa akafa ya kikoa na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi mikoa yote Tanzania Bara, kutathmini siku 100 za uongozi wake, kujitathmini katika kutekeleza maagizo ya Rais Dt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi bora ya ardhi. 

 "Hiki ni kikao kazi cha kutathmini siku 100 na kutengeneza mpango wa kutekeleza maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kutatua matatizo ya migogoro ya ardhi na kuwahudumia wananchi wetu," akatamka Waziri Silaa.

 Hapo akawasisitiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa, kwamba wana kazi ya kusimamia watumishi chini yao kujipanga vizuri na wana uwezo kubadilisha jinsi sekta ya ardhi inavyoendeshwa nchini kote.

Waziri Silaa akanena kuwa, Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wanachapa kazi katika mikoa yote na  utendaji wao ndio unatoa taswira inaopaswa kusonga, kutekeleza maelekezo ya viongozi wa kitaifa, kuleta tija kwa Watanzania.

Aidha, Waziri Silaa akawaambia kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, kupokea na kuheshimu ushauri wanaoutoa kuhusu shughuli za sekta hiyo nchini.

ANAVYOPOKEWA IKULU

Rais Samia Suluhu Hassan, mnamo wiki mbili zilizopita akizungumza Ikulu, Dar es Salaam, alieleza kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, kupita kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuzitatua paopo kwa hapo.

Akatamka: “Nafurahishwa na juhudi zinazochukuliwa sasa hivi na Wizara ya Ardhi kupita na kusikiliza kero na kuzitatua palepale lakini Wizara ya Ardhi ni moja... Wakuu wa Mikoa wasaidieni angalau wakija wanakuta mmeshafanya, wao wanatoa suluhisho.”