Mbisa arejea uwanjani baada ya msimu mmoja

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:35 AM Apr 24 2024
Golikipa wa timu ya Prisons, Mussa Mbisa.
Picha:Maktaba
Golikipa wa timu ya Prisons, Mussa Mbisa.

GOLIKIPA wa timu ya Prisons, Mussa Mbisa, juzi alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo msimu huu tangu alipoumia Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Akizungumza baada ya kurejea uwanjani, alisema anashukuru kuwa amekaa langoni baada ya muda mrefu na hakuruhusu bao katika mechi ambayo timu yake ilitoka suluhu dhidi ya Kagera Sugar, mechi ikichezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

"Nashukuru nimerejea, nimekaa langoni baada ya muda mrefu na sijaruhusu bao, kikubwa kilichobaki ni kuwa na mwendelezo mzuri, kufanya vema katika michezo itakayokuja mbele kila nitakapopewa nafasi kwa sababu hapa Prisons, magolikipa wote sisi watatu ni wazuri, kila mmoja ana kitu chake kimoja ambacho anawashinda wenzake, kikubwa kila anayepewa nafasi aitendee haki kwa sababu nyuma kuna wengine.

"Kwangu mimi niliona kama kocha amenipa deni kubwa, nimetoka kwenye majeraha, lakini amenipa namba, nimekaa langoni kwa uangalifu mkubwa ili nisije nikamvunja moyo kocha wangu, Ahmad Ally, aliyeniamini," alisema Mbisa ambaye amewahi kuzidakia Klabu za Mwadui na Coastal Union.

Kipa huyo aliumia katika mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita katika mechi ambayo timu yake ilicheza dhidi ya Singida Big Stars na kulazimika kutolewa nje na kukimbizwa hospitali, tangu hapo alikuwa akiuguza jereha la mguu.

Katika mechi yake ya kwanza ambayo ametoka na 'clean sheet', ameisaidia timu yake kupata pointi moja na kufikisha  31, ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku timu iliyocheza nayo, Kagera Sugar ikiwa nyuma yake nafasi ya saba, ikikusanya pointi 29.