Simba SC waitwa kuandika historia

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:01 AM Mar 28 2024
Mashabiki wa Simba na Yanga kutoka sehemu mbalimbali jijini, Dar es Salaam jana wakihamasisha kuelekea michezo ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho.
Picha: Simba SC.
Mashabiki wa Simba na Yanga kutoka sehemu mbalimbali jijini, Dar es Salaam jana wakihamasisha kuelekea michezo ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho.

MABAO, mabao, mabao, hicho ndio kilio cha Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, kuelekea mechi ya robo fainali Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa kesho kwa kuwapa mbinu mpya safu yake ya ushambuliaji ili kuhakikisha wanapata ushindi na si matokeo mengine tofauti, imefahamika.

Simba watakuwa nyumbani kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kesho kuwakaribisha Waarabu hao wa Misri katika mchezo wa kwanza wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kuanzia saa 3:00 usiku.

Benchikha ameliambia Nipashe anataka kuona washambuliaji wake wanatumia vizuri kila nafasi watakayoipata katika mechi hiyo ili kumaliza 'kazi'.

ili kufikia malengo, kocha huyo ameamua kuifua upya safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Fredy Michael, Pa Jobe Omar na Mtanzania Kibu Denis, kwa kuwakumbusha kuongeza umakini katika mechi hiyo itakayowatengenezea historia mpya.

Kocha huyo amesema hataki kuona nyota wake wanapoteza nafasi kizembe kwa sababu mchezo huo ni wa maamuzi na wanahitaji kumaliza safari waliyoianza mapema.

Aliongeza malengo yake ni kuhakikisha kikosi hicho kinapata ushindi mnono na ili kufikia hapo, amelazimika 'kuvaa sura ya kazi' kwa kuwasisitiza wachezaji wake kujituma na kucheza kwa nidhamu wakifahamu wanacheza na moja ya timu ngumu Afrika.

Kocha huyo ambaye msimu uliopita aliipa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, USM Alger ya Algeria alisema anataka kuiona Simba ikipenya na kutinga hatua ya nusu fainali na hilo litafanikiwa endapo washambuliaji watazitendea haki nafasi watakazopata.

“Huu ni mchezo muhimu sana kwetu, tunatakiwa kufanya kila linalowezekana ili kupata ushindi mkubwa hapa nyumbani. Ukicheza na timu (Al Ahly) kama hii unatakiwa kutumia vizuri kila nafasi utakayoipata kwa sababu ni wazoefu, hawawezi kukuruhusu kutengeneza nafasi nyingi sana.

Kutokana na hali hiyo, ninaendelea kuwafua washambuliaji wangu, ninawasisitiza kila nafasi lazima tuitumie vizuri, tunatakiwa kumaliza mchezo hapa nyumbani, tukipata ushindi wa idadi kubwa ya mabao itakuwa ni faida kubwa sana kwetu,” kocha huyo alisema.

Aliongeza ili kuisuka vyema safu yake ya washambuliaji, ameendelea kuwapa mbinu tofauti tofauti sambamba na nyota wake wanaocheza eneo la ulinzi kuhakikisha hawaruhusu bao kwa sababu inaweza ikawagharimu mbele ya safari.

“Sio nahangaika na safu ya ushambuliaji peke yake, hapana, pia nimekuwa nikitumia muda mwingi kuikumbusha safu ya ulinzi hawatakiwi kufanya kosa lolote, kama safu ya ushambuliaji watakuwa wanafunga halafu safu ya ulinzi inaruhusu mabao kizembe itakuwa ni kazi bure,” alisema kocha huyo.

Naye  Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kikosi kilipokuwa Zanzibar, kilifanya mazoezi maalum katika kila idara ili kuboresha viwango vya wachezaji wao.

Ahmed alisema kipindi chote cha siku nane, kocha (Benchikha), alitenga muda wa mazoezi wa kila eneo kwa kuwapa mbinu za kukabiliana na Al Ahly.

“Zoezi hilo linaendelea, kikosi kina mabadiliko makubwa ya ubora katika idara zote, hatuna mashaka kabisa na eneo la ushambuliaji, kocha ameongeza makali,” alisema Ahmed.

Aliongeza wachezaji wote wako fiti huku kiungo Clatous Chama akiwa ameingia  kambini jana moja kwa moja ili kujiunga na wenzake kuendelea na maandalizi ya kuwavaa Al Ahly. 

“Mwaka huu tumedhamiria kumwondoa Al Ahly, Wanasimba sasa ni muda wao wa kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwa sehemu ya historia ya kumwondoa Al Ahly na Simba kuingia nusu fainali," alimaliza meneja huyo.