Mwinyi alivyosaidia wachezaji Simba kuzawadiwa Magari

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:30 AM Mar 03 2024
Hayati
PICHA: MTANDAO
Hayati

RAIS wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia juzi akiwa na miaka 98 atakumbukwa kwa mengi katika nyanja mbalimbali, huku mashabiki wa michezo wakimkumbuka kwa kukuza na kuendeleza sanaa na michezo nchini.

Wakati wa utawala wake ndicho kipindi ambacho klabu ya Simba ilifanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mwaka 1993 na kufungwa mechi ya fainali mabao 2-0 dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Novemba 27, 1993, na yeye kuwa mgeni rasmi.

Mwinyi ndiye aliyewavisha wachezaji wa timu zote mbili medali, Simba wakivalishwa medali ya fedha na mabingwa wakipata ya dhahabu.

Katika mechi ya kwanza, Simba ilitoka suluhu ugenini, lakini kwa namna ya kushangaza ilipoteza nyumbani mbele ya Rais Mwinyi wakati huo.

Awali Simba iliahidiwa kupata magari aina ya Kia kila mmoja wakati huo kutoka kwa mfadhili wao wakati huo, Azim Dewji, lakini ahadi ilikuwa imekufa baada ya kufungwa, lakini chini ya utawala wake, akaona haikuwa vyema wachezaji wa timu hiyo kutopata chochote kwani walifanya kazi kubwa hadi kufikia hatua hiyo.

Ndipo kwa kushirikiana na mfadhili huyo, wakaamua kuagiza na kuwazawadia wachezaji 30 wa Simba magari aina ya Toyota Corolla, wakati huo magari hayo yalikuwa kisasa kabisa.

Serikali ya Mwinyi iliondoa kodi ili kupunguza gharama nyingi zilizokuwa zikihitajika, na kwa kiasi kikubwa yaliwasaidia sana baadhi ya wachezaji waliokuwa wanastaafu mwaka huo kujikimu kimaisha kwa kuyageuza kuwa taxi.

Kutokana na kipigo hicho, na baada ya hapo kukawa na mfululizo wa matokeo mabaya ya timu ya taifa yaliyomchukiza Rais Mwinyi na kufikia kusema soka la Tanzania ni kama kichwa cha mwendawazimu kiasi kwamba hata mlevi anajifunzia kunyoa.

Msemo huo aliufuta miaka mingi baadaye, na hiyo ni baada ya kuona mambo yanabadilika na angalau klabu za Tanzania zinafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ pia ikionekana kuamka.

Mwaka mmoja baadaye, 1994 chini ya utawala wake, Tanzania Bara ilifanikiwa kutwaa Kombe la Challenge nchini Uganda.

Kwa upande wa muziki, kipindi cha Mwinyi ndicho bendi nyingi zilianzishwa ukiacha zile kongwe na hii ilitokana na urahisi wa upatikanaji wa vyombo vya muziki ambavyo awali ilikuwa ngumu kuvipata na kusababisha bendi nyingi kufa.

Rukhsa ya mzee Mwinyi, mbali na vitu vingine kuruhusiwa kuingia nchini, pia vyombo vya muziki viliruhisiwa kwa wingi kiasi cha bendi nyingi kuanzishwa na kuleta upinzani na ushindani mkali, muziki wa Tanzania ukazidi kuja juu.

Pia Hayati Mwinyi alikuwa mwanamichezo, yeye mwenyewe alisema alipokuwa kijana alikuwa akicheza beki wa kati, na moja kati ya vitu vilivyomfanya aishi miaka mingi ni mazoezi ya kukimbia, maarufu kama 'Jogging'.

Alikuwa akiwashinda hata wale wenye umri mdogo ambao walikuwa wakiishia kati na yeye kumaliza mzunguko wote wa mbio zilizopangwa.

Hivi ndivyo wasanii, wanamuziki na wanamichezo wanavyomkumbuka Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Mzee Rukhsa.