Makonda anyooshewa kidole kauli kuhusu haki mahakamani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:16 PM Feb 14 2024
Paul Makonda.
PICHA :Na Mtandao
Paul Makonda.

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) na wadau wengine wa haki na utawala bora, wameitaka Mahakama kutoa tamko kuhusu kauli ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) - Itikadi na Uenezi, Paul Makonda dhidi ya chombo hicho.

Mimi mwenyewe hapa kuna mtu alinidhulumu nyumba, halafu wajanja wakaniambia 'nenda mahakamani'. Nikapiga mahesabu mahakamani kwa jinsi huyu mtu alivyo na hela (fedha) nitatoboa? "  amesema Makonda.

Makonda aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli, ananyooshewa kidole kutokana na kauli yake kwamba wananchi waache kukimbilia mahakamani, badala yake wapeleke kero zao kwa wateule wa Rais.

Akiwa katika ziara ya chama chake mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwanzoni mwa mwezi huu, Makonda aliwataka wananchi kupeleka kero zao kwa wateule wa Rais, akiwamo yeye kwa kile alichodai kukimbilia mahakamani huenda kukafanya wasipate haki.

Makonda alisema wananchi huenda wasipate haki katika chombo hicho kwa kuwa huko kuna aliowaita "wajanja wanaoweza kutumia mbinu kushinda kesi".

"Mimi mwenyewe hapa kuna mtu alinidhulumu nyumba, halafu wajanja wakaniambia 'nenda mahakamani'. Nikapiga mahesabu mahakamani kwa jinsi huyu mtu alivyo na hela (fedha) nitatoboa? 

"Nikasema Mungu atanipa mlango na Mungu amenipa. Kwahiyo, msikimbilie wapi… msikimbilie mahakamani, wale wajanja wana mbinu zao.

"Wanasheria kazi yao ni kumtetea mteja wao, hata awe ameua, (wakili) jukumu lake amtetee mteja wake na yeye ni lazima aoneshe ni wakili bingwa. Kwahiyo, ukiwa huna wakili bora, unaweza kupoteza haki yako.

"Ndiyo maana unashangaa watu wengi maskini kesi zao zina miaka 10, miaka 20, miaka 15 inapigwa tarehe, inatubidi tubanane huku huku kwa wateule wa Dk. Samia Suluhu Hassan," Makonda alisema.

BAVICHA katika taarifa yao ya jana kwa vyombo vya habari, wanashauri uongozi wa Mahakama kutoa kauli ili kurejesha imani ya wananchi kwa muhimili huo kuhusu utoaji haki bila kujali hali ya kipato aliyonayo mtu wala hadhi yake katika jamii.

BAVICHA kupitia taarifa yake hiyo iliyotiwa saini na Apolinary Boniface, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa baraza hilo, inasisitiza kuwa Taifa likikosa imani na mahakama, nchi haitatawalika.  

"BAVICHA tunatoa wito kwa muhimili wa Mahakama kutoa kauli kuhusu alichokisema Mwenezi wa CCM, ni vyema umma ukajua kama ni kweli muhimili huo unatoa haki kwa wenye fedha tu na siyo kwa wananchi wa hali zote.

“Mahakama isipotoa kauli ya kukemea na kukanusha kauli hiyo ya Makonda, itawaaminisha wananchi kujichukulia uamuzi mkononi kutokana na kukosa imani kwa muhimili huo kama utawatenda haki,” BAVICHA inaeleza katika taarifa yake hiyo.

Mwandishi wa Habari Mkongwe, Ndimara Tegambwage pia ameshauri Mahakama na Bunge kutoa kauli kuhusu suala hilo ili kutokufifisha misingi ya haki na utawala bora na kutegemea wateule wachache kupata haki zao.

"Mahakama ina cha kusema hapa juu ya kauli ya CCM kuwa wananchi wasiende mahakamani, Bunge lisimame na kusema inatosha na kukemea yule anayelenga kuleta utawala wa mfukoni usio wa sheria na wa kidhalimu.

“Chama cha Wanasheria (TLS), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), asasi hai za kijamii, vyombo vya habari na wote wenye mapenzi mema kwa Tanzania, wana kitu cha kusema. Wakiseme wapinge ‘ushetani’ huu.

“Ninatambua vyama vya siasa ni asasi za kijamii, tuone na tusikie kauli zao kwa hili... Mkoa wapi magwiji wa sheria – binafsi na kampuni na wapigania uhuru na haki kazini, mitaani na vyuoni? Mnakaa kimya ili iweje?” Ndimara alihoji.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe alisema jana kuwa kauli ya Makonda inaweza kuwa na tafsiri tofauti kuhusu mfumo wa utoaji haki wa Mahakama kwa watanzania hasa kwa wale wasiokuwa na fedha.

Alisema kuwa mtu anaweza kupata haki kwa kutumia njia zisizokuwa rasmi kuliko zile zilizo rasmi.

"Kauli ya Makonda inaweza kuwa na tafsiri tofauti. Moja ikiwa ni kutaarifu umma wa watanzania kuwa mfumo wa Mahakama si salama katika kupata haki, hususani kwa watu wasiokuwa na fedha na pili tafsiri kuwa unaweza kupata haki kupitia njia zingine zisizokuwa rasmi," alisema.