Elimu yawakwamua, waanzisha kiwanda

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:10 PM Mar 28 2024
Wanawake kutoka Kikundi cha kutengeneza bidhaa zitokanazo na Ngozi cha Kalangale Kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu.
PICHA: MARCO MADUHU
Wanawake kutoka Kikundi cha kutengeneza bidhaa zitokanazo na Ngozi cha Kalangale Kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu.

WANAWAKE kutoka kikundi cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Kalangale kilichopo katika Kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, wajengewa uwezo katika nyanja ya ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo hayo yanawafanya wanakikundi hao kufanya shughuli za kujiingizia kipato bila kuwa na utengemezi kwa waume zao.

Hayo yamebainisha na wanawake hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu, huku wakibainisha kupewa mafunzo hayo na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP).

Makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho Rejina Emmanuel, amesema awali wanawake kijijini humo walikuwa tegemezi kutoka kwa waume zao pamoja na kukabiliwa na maisha duni sababu walikuwa wa mama wa nyumbani,lakini sasa hivi wanajishughulisha na ujasiriamali na siyo tegemezi tena.

“Tunawashukuru kwa kutupatia elimu ya ujasiri sisi wanawake wa hapa Kiloleli, kwa kweli sasa hivi tunafanya shughuli za kiuchumi pamoja na wanaume kupitia vikundi, ikiwamo kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi kama vile viatu, mikoba, na mikanda, kazi ambazo awali tulidhani ni za wanaume pekee,”amesema Rejina.

Mwanamke mwingine Malta Ngwelu, amesema baada ya kupewa elimu hhiyo ndipo wakaamua kuthubutu na kuunda kikundi chenye kujumuisha watu wa jinsia zote na kufungua kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi, ambacho kimewasaidia kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wa Joseph Soleya, ambaye pia ni mwanakikundi, amesema wamefurahia kufanya kazi pamoja na wanawake sababu ni wachapakazi wazuri na kwamba wanajituma na pia ni waaminifu, na kwamba tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho, hapajawahi kutokea migogoro.

Katibu msaidizi wa kituo cha taarifa na maarifa kutoka TGNP wilayani Kishapu, Zacharia Pimbi, amesema baada ya wananchi hao kupewa elimu ya ubunifu na kuibua miradi, ndipo wakaona watumie fursa ya kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa za ngozi na kuungana Jinsia zote.

Amesema kupitia kikundi hicho ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, kupitia mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi vijijini (EBBAR), kikundi hicho kiliwezeshwa Sh.milioni 95.6 kwa ajili ya kuanzisha kiwanda hicho.

“Kikundi hiki kina jumla ya wanachama 17, kati yao; wanawake wapo 10 na wanaume 7, na ofisi ya Makamu wa Rais ilitupatia fedha ili wananchi wajishughulishe na biashara zitokanazo na bidhaa za ngozi, na kuacha kufanya biashara za kuuza mkaa ili wasikate miti hovyo na kusababisha uharibifu wa Mazingira,” amesema Pimbi.

Aidha, amesema pia Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wameendelea kuwa nao bega kwa bega na hata hapo awali ili kuwapatia Sh.milioni 10 zitokanazo na mikopo ya asilimia 10.

Aidha, Pimbi amebainisha kuwa kwa sasa changamoto kubwa inayowakabili ni kutokuwa na mashine ya kuchakata ngozi, na hivyo kulazimika kufuata malighafi hiyo jijini Mwanza.