Mpango kabambe matumizi nishati safi kupikia

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 07:27 AM Apr 13 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

WIZARA ya Nishati imesema imeweka mikakati kuhakikisha ifikapo mwaka 2033 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alisema hayo jana wakati akizungumzia maonyesho ya sekta ya nishati.

Maonyesho hayo yanatarajiwa kuanza keshokutwa na yatafanyika kwa siku tano katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.

“Wizara imeamua kwa dhati kabisa kulibeba suala la nishati safi ya kupikia kama ajenda maalum ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na matumizi ya nishati isiyo safi  na wahamie kwenye matumizi ya nishati safi,” alisema.

Biteko alisema kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani miaka ya karibuni, bei ya mafuta imeendelea kupanda na kufanya matumizi ya fedha za kigeni kuwa makubwa kwa ajili ya kuagiza nishati hiyo.

 Alisema wizara ina mikakati kabambe ya kupunguza utegemezi wa mafuta, hivyo nia ni kuhimiza matumizi ya gesi asilia kuendesha magari na  mitambo inayotumika viwandani.

Biteko alisema maonyesho hayo yamekuwa yakiwapa fursa ya kuonyesha dira na mwelekeo wa sekta ya nishati na kwamba mwaka huu ajenda kuu ni nishati safi ya kupikia ambayo imemng’arisha Rais Samia Suluhu Hassan katika bara zima la Afrika.

Desemba 2, mwaka jana, Rais Samia alizindua mradi wa nishati safi ya kupikia itakayowasaidia wanawake barani Afrika katika mkutano uliofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kando ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28).

Biteko alisema maonyesho hayo ni fursa kwa wabunge na watanzania wengine kufahamu utekelezaji wa sera ya nishati kwa mwaka 2024/25 na mwelekeo wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.

Alisema Wizara ya Nishati ambayo imepewa wajibu wa kusimamia masuala ya umeme, mafuta, gesi na utafutaji wa gesi kwenye maeneo mbalimbali nchini, imekuwa na kawaida ya kufanya maonyesho hayo kila mara wakati wa Bunge la Bajeti.

“Tumekuwa na utaratibu huu wa kukutana na wadau wetu kila mwaka kutupa maoni ya maeneo ya kufanya maboresho na waseme maeneo ambayo wanaona tunafanya vizuri pia,” alisema Biteko.

Aidha, alisema kwa miaka yote ambayo wizara imekuwa ikifanya maonyesho hayo kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wadau kuibua hoja ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi ikiwemo kutoa ufafanuzi kwa mambo ambayo hayakuwa yakifahamika.