TASAC yawataka watoa huduma za usafirishaji majini kufuata sheria

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 06:30 PM Apr 29 2024
Selina Mokiti, Ofisa Usafirishaji Idara ya Udhibiti Huduma za Usafiri Majini wakati akielezea majukumu ya TASAC.
Picha: Cynthia Mwilolezi
Selina Mokiti, Ofisa Usafirishaji Idara ya Udhibiti Huduma za Usafiri Majini wakati akielezea majukumu ya TASAC.

SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) imewaagiza watoa huduma za usafirishaji majini ikiwemo mawakala wa uondoshwaji na uondoaji mizigo bandarini, kuhakikikisha wanafuata sheria na taratibu za usafirishaji mizigo ili kuondoka usumbufu.

Hayo yamesemwa leo na Selina Mokiti Ofisa Usafirishaji Idara ya Udhibiti Huduma za Usafiri Majini wakati akielezea majukumu ya TASAC katika utoaji huduma na bidhaa kwa watoa huduma bandarini na bandari kavu kwenye maonesho yanayoendelea jijini Arusha  yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya (OSHA).

Amesema  watoa huduma na bidhaa ni vizuri wafuate viwango vinavyotakiwa, ili wateja waweze kuhudumiwa kwa wakati  na uhakikikisha wasafirishaji wanapata huduma kwa wakati na kuondoka usumbufu.

"Changamoto kubwa wanazopitia ni kwa wateja kutofahamu haki zao hivyo TASAC hivi sasa inasajili wateja ili kubaini mizigo yao inapopotea na kuifuatilia lakini  tunaendelea kuelimisha watoa huduma kufuata vigezo na masharti yaliyoanishwa kisheria katika usafrishaji,"amesema

Naye Ofisa Uhusiano Mwandamizi kutoka TASAC,Amina  Miruko  amesema  shirika hilo linasimamia usalama wa vyombo,abiria ,mizigo yao pamoja na mazingira yote ya usafirishaji.

Aidha amesema  mazingira ya usafirishaji ni pamoja na kaguzi mbalimbali ili kuhakikikisha vyombo hivyo vya majini vinakidhi viwango vya kimataifa ikiwemo vifaa vya kujiokoa pale inapotokea ajali na  kuratibu utafutaji na uokoaji pale inapotokea dharura yoyote.

Awali Kisamo Mandari ambaye ni  ofisa Ugomboaji na Uondoshwaji wa Sheheha kutoka TASAC amesema shirika hilo linajukumu la kipekee katika ugomboaji wa bidhaa tano ambazo ni kemikali zinazotumika migodoni, madini katika makinikia,nyaraka za serikali ,wanyama hai pamoja na vilipuzi pamoja na silaha.