Wazazi wakumbushwa wajibu malezi kwa familia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:11 PM Apr 29 2024
Malezi ya familia.
PICHA: MAKTABA
Malezi ya familia.

KUELEKEA kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia Mei 15, mwaka huu, wazazi wameombwa kuishi katika hali ya upendo, kuvumiliana ili kunusuru ndoa na kuimarisha malezi ya watoto.

Mwinjilisti Godfrey Nyange kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa mji mpya Daiyosisi ya Morogoro, amezungumza na Nipashe Digital amewaomba wazazi kukiishi kiapo cha ndoa na kumwomba Mwenyezi Mungu kuwasaidia kuwalea watoto vyema.

Amesema ndoa nyingi huvunjika hasa kwa vijana na kusababisha athari kubwa katika jamii kutokana na watoto kushindwa kupata uangalizi sahihi kutoka kwa wazazi wote wawili.

“Ni vyema wazazi wakielewana kwani itakuwa rahisi kuwalea watoto, wakitelekezwa wengi huishia kuiga maadili yasiyofaa,” amesema.

Aidha, amewashauri wazazi kukaa katika nafasi zao ili kutimiza jukumu la malezi ya watoto wapate misingi sahihi itakayowawezesha kukua katika maadili mema. 

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Doroth Gwajima Aprili 18, mwaka huu kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024  jumla ya mashauri ya kifamilia14,600 yaliripotiwa ikiwamo migogoro ya ndoa 5,306 sawa na asilimia 36, migogoro ya matunzo ya watoto, 5,944 sawa na asilimia 41.

Mashauri ya matunzo ya watoto wa nje ya ndoa, 3,350 sawa na asilimia 23 kati ya mashauri hayo 3,411, ngazi ya ustawi wa jamii na 1,642 yalifanyiwa kazi na yaliyo patiwa rufani kwenda mahakamani ni 921 kati ya hayo 443 yakiendelea kufanyiwa kazi na yaliyokabidhiwa kwenye mabaraza ya kata na jumuiya yakiwa 405.

Emmaculate Ephrahim, mkazi wa kata ya mji mpya Manispaa ya Morogoro,  amesema yeye ni mzazi jukumu lake ni kuimarisha upendo, amani, mshikamano kama nguzo kuu ya upendo, ambayo huileta pamoja familia na kuwa na umoja.

Hamis Othman mkazi wa Mtawala, Manispaa ya Morogoro, amewataka kinababa kuwa mstari wa mbele katika ulezi na uangalizi wa familia ili kujenga heshima baina mzazi na mtoto.

Kaulimbiu ya mwaka huu kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia inasema, ‘Tukubali tofauti zetu katika familia kuimarisha malezi ya watoto’.