Kunywa maji mpaka Makamu wa Rais atishie kung’oka?

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 11:10 AM Mar 29 2024
news
Mchoraji: Muhidin Msamba.
Mchoro wa katuni ukionesha majadilioano kuhusu makala hii juu ya uwajibikaji wa viongozi.

MKO nyumbani mmetulia kama familia, ghafla baba anaingia na kupiga kelele huku akijiapiza: “Haki ya Mungu huyo kuku asipopikwa leo familia ikala, nitajinyonga!”

Anamwelekea msichana wa kazi na kumtazama kwa hasira na kurudia kiapo. Mzee anaonekana kumaanisha, kwamba haiwezekani kuku kaletwa na kila kitu kipo kuanzia vyombo, jiko na viungo, lakini kuku asipikwe na akaliwa. 

Lazima mtashangaa na kumtazama baba kama yuko sawa au la? Lakini, kumbe baba anataka familia yake ifurahie na pengine alishamwangalia msichana wa kazi na kubaini kuwa ana uzembe fulani hivi katika kutekeleza majukumu yake ya msingi na sasa amechoka kumvumilia.

 Nanyi kama wanafamilia, mnajiuliza hivi kwa nini asimtimue tu akatafutwa mwingine kuliko kutaka kuhatarisha maisha yake, sasa baba akijitoa maisha nani mtamtegemea kama familia? 

Polepole ili kutaka kuokoa hali, mnamfuata baba na kumwuliza kulikoni mpaka aamue kuchukua hatua nzito na ya hatari kama hivi, anakwambieni si mara ya kwanza kuleta vitu nyumbani lakini havishughulikiwi kama anavyotaka.

 Msichana wa kazi anaona hatari mbele yake na anajitokeza na kumhakikisha baba, kuwa hakuna litakaloharibika, kwani kuku atapikwa na familia itafurahia kama anavyotaka na kama inavyotakiwa.

 Pande zote zinakubaliana na kubaki sasa kufuatilia kitakachofanyika kwa msichana wa kazi, ama kumpika kuku yule au kufukuzwa yeye ili kuokoa maisha ya nguzo ya familia na kuchelea kuitikisa familia.

 Simulizi hii inakuja baada ya kumsikia hivi karibuni Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango akiwa kijijini Kiria, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, akifuatilia mradi mkubwa wa maji wa Mwanga/Same/Korogwe.

 Maana yake huko anakuta madudu, anapoona mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300 unaofadhiliwa na serikali pamoja na mashirika ya misaada ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ukisuasua.

 Kwa kulitambua hilo lakini na uzito wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa maeneo hayo wenye kero sugu ya maji, Dk Mpango anaamua kujitoa mhanga na kuweka rehani wadhifa wake.

 Anasema, yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake endapo mradi huo unaohudumia watu 438,000 utakuwa haujakamilika ifikapo Juni mwaka huu. 

 â€śSina uso wa kuja kutazama wananchi walioahidiwa maji kwa miaka 19 sasa…nitajiuzulu, ila sijui kitatokea nini kwa walio chini yangu…!” anatamka.

 Sasa basi, ili mradi huo ukidhi mahitaji ya watu hao kisawasawa ni mpaka mwaka 2038, yaani miaka 14 ijayo! Nampa pole sana kiongozi wangu huyu kwa kuonyesha ni jinsi gani anaumizwa na matatizo ya wananchi wa maeneo hayo.

 Lakini labda turudi kwenye matatizo ya jumla ya maji katika nchi hii iliyopata uhuru mwaka 1961, nchi ya Maziwa Makuu, ikiwa imezungukwa na maziwa matatu makubwa Afrika, achilia mbali Bahari ya Hindi, mito, vijito na mabwawa.

 Watanzania sijui tulijikwaa wapi, kwa sababu miaka ya awali ya uhuru, maji yalikuwa ya kumwaga, yakipatikana mijini tena kwa kuingiza sarafu ya chapa kwenye bomba na maji kutoka, lakini leo tumerudi kuchimba visima vilivyotumiwa na mababu zetu.

 Tungekuwa makini katika majukumu yetu, na kama wizara za maji zilizokuwapo tangu uhuru, zingefanya kweli majukumu yao kwa maslahi ya Taifa na si ya viongozi, tusingekuwa na haja ya Wizara ya Maji leo, kwani maji yangekuwapo bila hata kusimamiwa.

Ngoja tusubiri, tukiona kwa wa Mwanga, Same na Korogwe mwaka 2038 maji yanapatikana bila matatizo kutokana na tishio la Makamu wa Rais kuachia ngazi, basi Makamu atakeyakuwapo wakati huo, naye atishie hivyo mwaka huo, ili Tanzania iwe na maji ya uhakika kila kona. Kazi Iendelee!