TAWLAE; kinamama wa kilimo na mazingira watembelea wenzao waliowekeza bustanini · Darasa kitaalamu, zawadi mbegu, ofa, ahadi tele…

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:31 AM Mar 29 2024
Baadhi ya wanachama wa TAWLAE, katika picha ya pamoja.
Picha: Vidah Mwihava.
Baadhi ya wanachama wa TAWLAE, katika picha ya pamoja.

INAPOTAMKWA msamiati TAWLAE, ni kifupi cha msamiati wa Kiingereza, Tanzania Association of Women Leaders in Agriculture and Environment.

Ni taasisi iliyoanzishwa rasmi mwaka 1995, ikiwakusanya wataalamu wanawake katika ufugaji, kilimo na mazingira, ikiwa na matawi mikoa yote ya nchi.

Ndani ya miaka 29 iliyopita, imeongozwa na safu ndefu, ikianza na Mwenyekiti Mama 

Rhoda Kweka. Badauara akafauatiwa na Mama Ada Mdessa Mwasha; Halima Chande, Dk. Maria Mashingo, Christina Lyimo, kisha Sophia Mlote. 

Kwa sasa Mwenyekiti ni Mama Elde Kimaro na Mkurugenzi wa Miradi katika kipindi kirefu amekuwa, Mary Liwa.  

Ndani ya safari yake hiyo, TAWLAE imekuwa na mafanikio makubwa katika jukumu lake kuhudumia jamii, ikiwamo kusaidia udhamini wa masomo kwa watu mbalimbali, pia mafunzo ya kilimo, ufugaji na mazingira kwa kinamama, vijana na vikundi.  

Hiyo imeendana na kusaidia sana kupunguza utumikishawji wa watoto kwenye mashamba ya wakulima wadogo wa tumbaku.  

Kilichofanyika sasa, wamehamasisha vijana wa kike na kiume kufanya kazi katika mashamba darasa, ili kujifunza kwamba ‘kilimo ni ajira.;  

Mjumuiko huo sasa umeanzisha vikoba kwa wanawake, sasa ikipanuka katika sura pana na huduma za benki ya wanawake vijijini, ambayo sasa inawawezesha kukopa na kuongeza mitaji katika vikoba.  

Hali inayoendelea sasa wanawake wengi wamepiga hatua wako kwenye biashara kupitia mikopo na vikoba walivyoanzisha.  

Vilevile,  imekuwa mstari wa mbele katika vita kutambua na kukabili unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake wa pembezoni, ikijiweka  kwenye utetezi wa masuala ya kijinsia, katika tafsiri pana iliyopo. 

SIKU YA WANAWAKE 

Katika kuungana na kimataifa, kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani Mwaka 2024 yenye kaulimbiu ‘Wekeza katika Wanawake Kuharakisha Maendeleo’, TAWLAE mkoa wa Dar es Salaam iliadhimisha kwa namna yake. 

Hapo ilifanya ziara kutembelea kikundi kiitwacho cha Kijani Kibichi – Kinyerezi, wilayani Ilala, vilevile kuzuru kwa wakulima wa mboga, Kunduchi  mboga Ununio, wilaya Kinondoni. 

 Ni vikundi vilivyofanyiwa ziara hiyo, kwa kupewa elimu ya kilimo bora cha mboga, pia nao wakaeleza changamoto zao na mafanikio waliyopata kupitia shughuli hizo za kilimo. 

Kijani Kibichi ni kikundi chenye wanachama hai wanawake 20, wanaojihusisha na kilimo hai cha mboga za majani, wakiwa na kaulimbiu yenye salamu inayowaongoza “Afya Bora kwa kila Familia na Biashara”.  

Wanakikundi hao huzalisha mboga zao kwa kutumia teknolojia hai ya kutumia mbolea zisizo na kemikali, pia wakizuia wadudu na magonjwa kwa njia hai. 

Utaratibu wao katika kuzalisha wanaeleza, hutumia vitunguu swaumu na pilipili kukinga wadudu na magonjwa shambani.  

Pia, wanataja kilimo cha kutumia kinachoitwa kitalamau shambani ‘greenhouse’. Hapo lengo wanataja ni kutunza mazingira, huku wakiwa na uhakika wa kupata chakula na kipato, hata kipindi cha nje ya msimu wa kilimo.  

Katika tukio hilo, mdau Mama Sophia Mlote, akakazia kuwa wanawake wana sifa ya kufanya mambo yaliyoshindikana, ikiwamo kuwa na mazingira mazuri, chakula cha kutosha na kilicho salama.  

Anaeleza historia ya kuanzishwa kikundi cha Kijani Kibichi, Mama Mlote anasema elimu aliyoipata nchini Uhispania ndio iliyompa chachu ya kukusanya wanawake pamoja na kuanzisha kikundi hicho kuelimishana na kutekeleza malengo yao. 

Hap kunmatajwa kuwapo kutunza familia, kufanya biashara na kuwa na kipato endelevu, yaani ‘Mama awe na fedha mfukoni’.  

Kwa sasa anasema wana shamba kubwa la ng’ombe wanalofanyia shughuli za kilimo, ila bado wana uhitaji kukamilisha taratibu za usajili wa kikundi chao, hata wakawa na shamba maeneo wanakoishi. 

Diwani wa Kinyerezi, Leah Mgitu na Ofisa Kilimo wa Kinyerezi, Helena Ihonde, waliohudhuria tukio hilo walipokea changamoto na kuahidi kuzitatua.  

Kukazia hoja hiyo, Diwani huyo akawashauri wana - kikundi kuwa na meza yao katika Soko la Kinyerezi, kuwawezesha kuuza mboga zao na kuweka bango kuonyesha upatikanaji wa mboga zilizozalishwa kwa njia ya kilimo hai.  

Wakawaambia, ni namna ya kukuza soko la mboga zinazozalishwa, akiwaambia “hakuna kinachoshindikana na ardhi itapatikana kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga cha pamoja kwa kufuata utaratibu.” 

Ofisa Kilimo akawaribisha wanakikundi cha Kijani Kibichi kufika katika Kituo cha Mafunzo ya kilimo na Mifugo, Pugu Kinyamwezi, wilayani Ilala, kujifunza teknolojia mbali mbali, kama za kilimo cha uyoga, nyanya na mazao mengine, pia kupata la uzalishaji. 

Hapo anarejeshja ujumbe pana kuwa serikali ya sasa inayoongozwa na mwanamama Dk.Samia Suluhu Hassan, inatoa kipaumbele kikubwa kwenye kilimo.

Hapo akawajulisha wadau hao, kwamba zipo mbolea ya ruzuku, wakiwaomba wakulima hao wakajiandikishe kwake, ili huduma ya mbolea ruzuku iwafikie. 

 DARASA KILIMO

 Dk.  Ruth Minja, Mwenyekiti wa TAWLAE mkoa wa Dar es Salaam, aliyekuwa Mkuu wa Msafara na mwanachama Violeth Mwaijande, Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni, walitoa elimu ya kilimo cha mboga kilivyo, kuanzia kitaluni hadi shambani. 

 Hapo wakajadili aina tano za mbegu bora za mboga, ambazo ni mchicha yenye aina tatu; nyanya chungu na mnavu, aina mpya kila moja. Vyote hivyo baadaye wakavigawa kwa wanakikundi na wadau 29.

 Pia, Mtafiti Vidah Mahava, kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni, Dar es Salaam, na mwanachama wa TAWLAE akawapa elimu ya kilimo cha mazao mchanganyiko. 

Hapo akatumia fursa ya eneo lake la kitaalamu na huduma kwenye kilimo cha minazi, inapochanganywa mazao mengine ya muda mrefu kama miembe, michungwa na malimau.

 Pia, ni michanganyiko ya muda mfupi kama mboga mboga, mihogo, viazi, mahindi na mananasi. 

 Sambamba na mbegu bora za mboga, Mama Martina Polepole, mwanachama wa TAWLAE na mmiliki wa kampuni ya Dondwe, aligawa mbegu za karanga miti (chestnuts) na kuelezea namna upandaji, utunzaji na faida za matunda hayo. 

 Wadau wengi walifurahia elimu hiyo na kuahidi kupanda kwenye mashamba yao, wakatumia ili kuboresha afya zao.

 KIKUNDI CHA UNUNIO

Wakulima wa mboga Ununio Wakulima, eneo la Songambele wengi wao wanalima mazao ya nyanya, bamia, mchicha, mnavu, loshuu, maboga na matembele.

 Pia, kukashuhudiwa kuwapo wakulima wachache wanaolima mpunga. Hapo kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume, wakijipatia vipato na mlo kwa ajili ya familia zao.

 Walipoulizwa kuhusu umiliki wa ardhi, wakulima hao wakalifafanua kila mmoja huonana na walinzi wa eneo husika na kuomba kutumia sehemu ya eneo kwa ajili ya kilimo. 

 Mkulima husika hufanya makubaliano na mlinzi wa sehemu hiyo na kufanya shughuli alizoziomba. 

 Rai yao sasa, wanahitaji eneo rasmi kwa ajili ya kilimo cha bustani. Faida nyingine, wakulima wakaeleza shughuli hizi za kilimo zinawaondolea msongo wa mawazo, zinawapa uwezo wa kujifunza na kuwafundisha wengine wanapotembelea mashamba yao. 

 Katika sura ya changamoto, wakulima hao wanalalamikia uwapo wa mbolea, mbegu na, viuatilifu feki, ukosefu wa elimu bora ya mboga kwa wakulima na ukosefu wa eneo rasmi la kulima mboga.

 Hapo wakapatiwa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto hizo, Dk. Ruth Minja na wanachama wengine wa TAWLAE wakieleza umuhimu wa kutumia pembejeo bora za kilimo na kwa njia sahihi, wakisisitiza matumizi ya mbolea ya samadi.

 Hiyo wakaitaja inaendana na mzunguko wa mazao, kutotumia miche ya jirani isiyo salama, iliyoathirika na kutofukia mabaki ya nyanya, nyanya chungu kwenye eneo unalotaka kupanda jamii ya nyanya, ili kuzuia madhara ya mnyauko na magonjwa mengine. 

Katika kilio cha mbegu, wakulima na wadau waliokuwapo Ununio, wakapewa zawadi ya mbegu bora za mchicha, nyanya chungu na mnavu na walielimishwa uoteshaji wake, jinsi ya kuandaa kitalu na utunzaji mboga hizo. Jumla ya wadau 45 walipatiwa mbegu hizo.

Mtaalamu Mama Sophia Mlote, akaeleza umuhimu wa kupunguza matumizi ya kemikali hasa kwa mboga, akishauri matumizi ya kilimo hai, ili kutunza afya ya mlaji na mazingira yaliyopo. 

Akafafaua kwa rai kwamba, ikiwa kila mmoja anampenda mwenzake hatataka kumlisha kemikali kupitia mboga.

MENEJA KIWANDA

Bwana Mkenda, Meneja wa kiwanda cha Mboji – Mabwepande, akawaonyesha wakulima mbolea ya mboji wanayoitengeneza, faida na upatikanaji wake. 

Kiwanda hicho kiko chini ya usimamizi wa Manispaa ya Kinondoni na lengo lake ni kupunguza ombwe la upatikanaji, ubora na gharama za mbolea nchini. Hapo wakulima walivutiwa na teknolojia hiyo na wakapewa mboji kiasi, kwa ajili ya majaribio.

Ofisa Kilimo, Agatha Mushi, akaahidi kuzichukua changamoto zinazohusika na manispaa na kuzipeleka sehemu husika. 

Akawaeleza wakulima uwapo wa mbolea ya ruzuku na kuwaomba wajiandikishe kwake, wale ambao hawajaandikishwa

· Mwandishi kitaaluma pia ni mtafiti kilimo.