Maandalizi ya Twiga Stars fainali CAF yaanze mapema

Nipashe
Published at 10:59 AM Apr 09 2024
Timu ya Twiga Stars.
Picha: Maktaba
Timu ya Twiga Stars.

WAKATI mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania unatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 15, mwaka huu, kikosi cha Timu ya Taifa (Twiga Stars), kitaenda kupeperusha bendera ya nchi kwenye mashindano ya Afrika (WAFCON), hivi karibuni.

Michuano ya WAFCON itafanyika baadaye Juni, mwaka huu huko Morocco na Twiga Stars imekata tiketi ya kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili.

Kwa mara ya kwanza Twiga Stars kushiriki fainali hizo zinazoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ilikuwa ni mwaka 2010 jijini Johanesburg, Afrika Kusini na kikosi kilikuwa chini ya nyota wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Boniface Mkwasa 'Master'.

Kuelekea mashindano ya WAFCON mwaka huu, Twiga Stars inahitaji kwenda katika fainali hizo ikiwa imara, kwa maana inakwenda kushindana kusaka rekodi mpya na si kwenda kushiriki au kukamilisha ratiba.

Ili Twiga Stars iende kufanya vizuri katika fainali hizo, Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inatakiwa iangalie vyema programu za timu hiyo kwa ajili ya maslahi ya nchi.

Inafahamika wazi idadi kubwa ya wachezaji wanaounda kikosi hicho wanatoka katika Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake, na kwa maana hiyo, kama kuna jambo la muhimu la kufanyia kazi wakati mzunguko wa pili wa ligi hiyo unatarajia kuanza, ni vyema likatazamwa kwa umakini.

Wachezaji wanahitaji kuwa na mazingira mazuri katika klabu zao ili baadaye waje kuipa matokeo chanya timu ya taifa, huu ni wakati wa TFF kuongeza na kuimarisha mahusiano na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake kwa ajili ya kuwasaidia kuwa kwenye mazingira rafiki wakati wanashiriki ligi.

Tunahitaji kuona kila kitu kinachohusiana na soka la wanawake kinakwenda vizuri kwa sababu huko ndio maandalizi rasmi ya Twiga Stars yanapoanza, na pale wanapoingia kwenye kambi ya Kocha Mkuu, Bakari Shime, wanakwenda kumalizia na kurekebisha mapungufu machache yaliyobainika.

Ili timu hiyo iende Morocco kwa kujiamini, huu ndio wakati wa TFF, serikali, taasisi, makampuni na wadau mbalimbali wa michezo kuungana kwa vitendo kusaidia maandalizi ya mabinti zetu ambao tunaamini wanaweza kwenda kuiletea heshima Tanzania.

Ni wazi Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka fungu kwa ajili ya kuhudumia timu za taifa, lakini ikumbukwe gharama zinazohitajika, na ili kufikia ndoto za kuvuna matokeo chanya, ni lazima michango ya ziada ipatikane kutoka kwa wadau.

Twiga Stars inahitaji kupata kambi yenye ubora pamoja na kutafutiwa michezo ya kirafiki na timu zilizo katika ubora ili kuwajenga wachezaji kwa kuwapa uzoefu wa kucheza mechi ngumu.

Mechi hizo si tu zitawapa uzoefu au kuwajenga, lakini zinawaondolea hofu wachezaji wa Twiga Stars pale watakapokwenda kushiriki fainali za WAFCON, wao ni tofauti, nyota watakaokwenda kushiriki fainali za mwaka huu, hakuna hata mmoja ambaye alikuwepo kwenye fainali za mwaka 2010. 

Kama ambavyo wanawake wamekuwa wa kwanza kushiriki fainali za Kombe la Dunia (Timu ya Taifa ya Wasichana ya umri chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Girls), za U-17 zilizofanyika mwaka juzi huko India na kutolewa kwenye hatua ya robo fainali, tunaamini hata kwa dada zao wanaweza kuweka rekodi ya kufika mbali au kurejea na kikombe cha ubingwa wa Afrika.

Pia huu ndio wakati muhimu kwa wachezaji kujituma kwenye mazoezi ili kuimarisha viwango vyao kwa sababu fainali za WAFCON zitawaweka upya sokoni kwa sababu makocha na mawakala kutoka sehemu mbalimbali watafuatilia michuano hiyo ili kusaka nyota kwa lengo la kwenda kuboresha klabu zao.